Uko hapa: NyumbaniBurudani2021 11 22Article 573559

Burudani of Monday, 22 November 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Penalti ya Yanga utata mpya

Penalti ya Yanga utata mpya Penalti ya Yanga utata mpya

ILE penalti iliyopewa Yanga kwenye mechi yao ya juzi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo bado ni gumzo na sasa refa wa zamani ameibua utata mpya juu ya namna ilivyopigwa na kukubalika huku wachezaji wa timu zote wakiwa ndani ya boksi la lango la Namungo.

Yanga ilipata penalti dakika ya 70 baada ya kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuonekana kama ameanguswa na beki Emmanuel Charles aliyekuwa akimnyang’anya mpira na mwamuzi Abel William kuamuru pigo hilo na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ akaipiga na kuisawazishia timu yake.

Hata hivyo wakati pigo hilo linapigwa ilionekana wachezaji zaidi ya wanne wa Yanga na wa Namungo wakikimbilia kwenye boksi kabla Saido hajapiga, kitu ambacho kwa sheria ya sasa ya penalti inakizana na tukio hilo kwa kuonekana kama wamemzonga kipa na kushindwa kuona mpira.

Licha ya utata huo, mwamuzi alilikubali bao hilo na kufanya matokeo kuwa bao 1-1 na sasa baadhi ya wachambuzi na marefa wa zamani wameibua utata mpya juu ya kukubaliwa kwa penalti hiyo.

Mwamuzi wa zamani Erick Onoka, alisema tukio la wachezaji kuingia ndani ya boksi mpira ukiwa bado haujaguwa lina faida mbili kwa wahusika wa mchezo huo.

“Faida ya kwanza kwa timu pinzani inayopigiwa kama mchezaji wake ndio ametangulia mbele na penalti ikakoswa, mwamuzi anarudia tena pigo hilo, ila kama mchezaji ni wa timu inayopiga faida itakuwa kwa wanaopigiwa kwa vile waliokuwa wanapiga wamefanya kosa, hivyo itaamuliwa adhabu (friikikii) ipigwe kuelekea langoni mwao,” alisema Onoka bila kuifafanua kwa undani penalti hiyo ya Yanga ila aliongeza;

“Kitendo cha mpigaji kutoka timu moja akaingia katika boksi ni wazi ameingia kumchanganya kipa, hivyo faulo inapigwa kwao ni sawa na mpigaji kumtishia kipa hiyo haiwezi kuwa penalti ni faulo, inayohamia kwenye lango lao na kama mpira ukatoka na wachezaji wa timu zote walikuwa ndani inaamuliwa pigo huru,” alisema Onoka, huku mwamuzi mwingine wa zamani Samuel Mpenzu alifafanua zaidi.

Alisema ni makosa kwa penalti kukubaliwa ikiwa imeingiliwa. “Wachezaji hawatakiwi kuingia ndani ya boksi mpigaji wa mpira kabla hajagusa mpira na ikitokea hivyo mwamuzi anatakiwa kuamuru irudiwe,” alisema Mpenzu na kuongeza;

“Wachezaji wakiingia ndani ya boksi unaangalia aliye mbele zaidi kama ni wa timu iliyopata pigo la penati inatakiwa penalti isirudiwe kupigwa na badala take kuwa pigo huru kuelekea kwao, lakini kama ni mchezaji wa timu inayoshambuliwa basi penalti inarudiwa kama imekoswa.”

Mwamuzi mwingine aliyekataa kutajwa jina lake, alisema penalti ya Yanga haikustahili kukubaliwa kuwa bao na mwamuzi Abel akifafanua kuwa, hakuna mchezaji anatakiwa kuingia ndani ya boksi wala kiduara kilichopo ndani ya eneo la 18.

“Ni aibu kubwa hasa kipindi hiki ambacho mpira wetu unarushwa kwenye televisheni na kuangaliwa na mataifa mengi ukiangalia vizuri kuna mchezaji alimzidi hadi mwamuzi lakini bado akaruhusu kuwa bao sio sawa, ilipaswa kurudiwa na wachezaji kuelekezwa vizuri,” alisema mwamuzi huyo.

Naye nyota wa zamani wa kimataifa wa Yanga, aliye mchambuzi kwa sasa, Ally Mayay alisema kilichotokea jana ni uelewa mdogo kwa wachezaji kuhusiana na sheria za soka hasa upigaji wa penalti.

“Wachezaji wa timu zote mbili waliingia eneo wasiloruhusiwa kabla ya mchezaji aliyepaswa kuwa hapo kugusa mpira kisheria haipo, hiyo ni makosa na endapo mpigaji angekosa ingerudiwa,” alisema.

Mayay alisema kitendo kilichotokea jana ni makosa wachezaji wanapaswa kupewa semina kuhusiana na sheria za upigaji wa penati kwani kwa jana imeonyesha uelewa wao wote upo chini.

“Sio kwa sheria ya penalti tu, bali mabadiliko ya sheria zote ili wajue.”