Uko hapa: NyumbaniBurudani2019 11 05Article 486979

Burudani of Tuesday, 5 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

Pensel ya Kiba aliyodai imeibiwa na Diamond, aliyeichonga sio Dimpoz?

Pensel ya Kiba aliyodai imeibiwa na Diamond, aliyeichonga sio Dimpoz? Pensel ya Kiba aliyodai imeibiwa na Diamond, aliyeichonga sio Dimpoz?

SHIDA ni mwandiko. Jinsi penseli ilivyochongwa na mchararango ulivyotokeza, imekuwa vigumu kukubali kuwa mchongaji na mwandishi ni Ali Kiba.

Kweli Ali Kiba ni wa kusema, Diamond Platnumz anamfanyizia mambo ya darasa la pili, anamuibia penseli halafu anajifanya kumsaidia kutafuta? Kisha akamtwanga; Unikome!

AliKiba tunayemjua, mwingi wa kujitenga na malumbano, yatakuwa yalimfika wapi mpaka kuamua kusema alichosema? Kuna mtu atakuwa alichukua ile penseli iliyoandika. Ule mwandiko si wa Ali Kiba tunayemjua. Huyu AliKiba ni tofauti kabisa.

Au Ommy Dimpoz? Maana Kiba na Dimpoz wote wapo Rockstar. Halafu ni watoto wa Gavana wa Mombasa, Hassan Joho. Inashindikana kupasiana simu na kutenda kilichotendeka huko Instagram?

Dimpoz kwa malumbano hajambo. Tena huwa hana simile. Wakati fulani alikwidana na Diamond kwenye vyombo vya habari na mitandaoni. Nini kilitokea? Dimpoz akamuingiza mama Diamond kwenye malumbano yao. Mambo yakawa moto kabisa.

Tena sio mmoja, Dimpoz mtoto wa Kiswahili kweli. Za kimjinimjini anazijua mpaka na nyongeza. Muulize Nay Wamitego alipomchokonoa kwamba eti hana demu. Walikwenda sawa mpaka mbabe wa Manzese mwenye kithembe akaamua kuuchuna. Dimpoz anashindwa vipi vita? Aliambiwa hana demu, basi akaibua mademu mpaka Wazungu, akawa anapiga nao picha mnato na video kisha zikatanda Instagram.

Aisee Dimpoz yule mtoto haramia asikwambie mtu. Akasema eti Nay aliwaonea wivu mademu zake, ndio maana alimsakama. Eti, Nay alikuwa anamtaka.

Sasa basi, Dimpoz ana hulka za kupenda ‘bato’. Swali ni je, Dimpoz alimchongea Kiba penseli na kumwacha aandike mwenyewe, au alimsadia vyote viwili kwa maana ya kumchongea na kumwandikia?

Au simu ya Kiba iliibwa, ikatua kwenye mikono ya Dimpoz, halafu mtoto wa Kiswazi akaamua kuchararanga kilichochararangwa? Tunashindwa kumpa maksi Kiba ili kuamua ufaulu wake wa bato, kwa sababu mwandiko ambao umetumika sio wake.

Dimpoz naye kakaa kimya. Bila shaka anajaribu kukwepa kuambiwa ni yeye ndiye kaandika. Tatizo Kiba hafuti kilichoandikwa, wala hasemi sio yeye. Hatangazi akaunti yake kudukuliwa. Sijui karidhia kilichofanyika? Inashangaza kwelikweli.

Kwa namna yoyote, iwe aliandika mwingine au yeye mwenyewe, jawabu ni moja; bubu yakimzidia hutaka kusimulia. Wakimya wanapovunja ukimya, ujue wameshanyamazia mengi. Hapo ndipo namwona Kiba.

Diamond na Ali Kiba kwa muda mrefu wamekuwa wakigombea ukubwa. Kila mmoja anataka aonekane ndiye papa wa muziki Tanzania. Nani kingpin wa Bongo Fleva?

Iwe mashabiki wao ndio wameng’ang’aniza huo ushindani au wao wenyewe, ukweli unabaki huo, kwamba kuna ushindani wa yupi samaki mkubwa kati yao.

Inapendeza kuishi kati ya upande mmoja, iwe baridi au moto. Sio kuwa katikati. Kujifanya vuguvugu. Kiba ameonesha kuwa maisha ya kujifanya viguvugu wakati anaumia, mwisho yangemtoa roho. Akaamua kubomoka au kuomba msaada kwa mtu ambomokee kwa niaba yake. Sijui ni Dimpoz?

Kwa kukariri alichokitamka ni kwamba Kiba anayo mengi ambayo hufanyiwa na Diamond. Tena, amesema siku akiyaweka wazi, itakuwa sawa na kumvua nguo. Pengine na Diamond naye ana ya kwake, ila kauchuna tu kwa sasa!

Kumbe sasa, kwa muda mrefu Kiba alikuwa vuguvugu lakini amekuwa akiumizwa na mengi kutoka kwa Diamond. Na kama ni kweli Diamond humtendea au anasingiziwa, yeye huamini kila kitu kipo sawa.

Sasa, kama Diamond humtendea mambo yasiyofaa Kiba, lakini anajifanya hamna shida, huo ndio uvuguvugu. Hayo ndio mambo yaliyomfanya Tupac zisiive na Notorious BIG na lebo yao nzima ya Bad Boy.

BIG akalalama: “When everything is cool, he talks again,” Kwamba Tupac alikuwa anaongea hata nyakati ambazo hakukuwa na tatizo. Tupac alitaka kama hakuna tatizo, kweli lisiwepo. Sio kila kitu kionekane kipo vizuri, lakini chini kwa chini kuna uchawi unafanyika. Haipendezi.

Tupac aliona mwenzake anashiriki au anamtendea mambo ya kinyama. Halafu wakikutana wanachekeana. Mwaka 1994, Tupac alipigwa risasi tano. Eneo la tukio akamwona BIG.

Kabla ya kumtuhumu kuhusika, aliuliza, BIG kama rafiki, kwa nini hakumjulisha uwepo wa njama za yeye kupigwa risasi? Kwa namna yoyote ile, aliona hata kama hakushiriki, lakini aliujua mpango uliokuwepo. Mbona hakumtaarifu? Aliridhika yeye ashambuliwe na hata auawe?

Kwa Tupac, bora uwe adui akujue kuliko kuwa rafiki unayemtakia mabaya. Halafu mbele yake uwe unajifanya mtu mwema. Hiyo haipo!

Penseli ya Kiba, iwe aliichonga na kuandika mwenyewe, au alichongewa na kuandikiwa, inafikisha ujumbe kuwa kama ni maadui bora kuendelea hivyo, kuliko kuchekeana kwenye vyombo vya habari na mitandaoni, wakati chini kwa chini kinachofanyika ni kutegeana misumali.

Hata kama penseli iliyoandika “unikome” kwa herufi kubwa Instagram kwenye akaunti ya Ali Kiba, haikushikwa na mwenyewe, kwa vile hajakanusha, bila shaka hayo ni maneno yake na ameyaunga mkono.

Kimantiki, Kiba anashika falsafa ya Tupac, kwamba uadui utendewe haki kama ilivyo maana yake, na urafiki uende hivyohivyo. Kinyume chake ni unafiki, na ameukataa.

Hata kama hakuandika yeye, iwe kaandikiwa na Dimpoz au mwingine yeyote, tafsiri ni hiyo kuwa uadui ubaki kuwa uadui na urafiki ulelewe kulingana na misingi yake.

Aliimba MwanaFA katika wimbo Show Time, “mikono isipige makofi ilhali noyo umenuna”. Ni mateso makubwa kuigiza furaha, wakati moyoni unaugulia maumivu.

Kama Kiba angeshangilia mwaliko wa Diamond, ilhali moyoni mwake anamwona adui, angekuwa anajitesa bure. Tena mateso yasiyo na sababu yoyote. Kusema ni kupumua, ni kuondoa sumu mwilini.

Mimi naendelea kuamini ule mwandiko sio wa Kiba, tena namhisi swahibu wake Dimpoz. Pamoja na kutopenda migogoro ya wasanii, lakini kuna usahihi kulisema tatizo kuliko kukaa nalo.

Baada ya kutamka, kama ni waungwana watakaa mezani na kusuluhisha. Maisha ya kugiza hakuna migogoro wakati ipo ni uchawi. Unasemaje hamna tatizo wakati lipo, suluhu itapatikana vipi? Kwa kurogana usiku?

Changamoto haitatuliwi kwa kujidanganya kuwa haipo.