Uko hapa: NyumbaniBurudani2021 11 21Article 573184

Burudani of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Sababu Wizkid Kumgaragaza Tena Diamond

Wizkid Wizkid

KWA mara nyingine, msanii wa Nigeria, Wizkid amenyakua tuzo mbele ya msanii Diamond Platnumz wa Tanzania.

Kule Budapest nchini Hungary wikiendi iliyopita, Wizkid alitwaa Tuzo ya MTV Europe Music Awards (EMA) katika Kipengele cha Msanii Bora Afrika kwa mwaka 2021 huku akiwapiga za uso wenzake; Amaarae wa Ghana, Focalistic wa Afrika Kusini, Tems wa Nigeria na Diamond Platnumz wa Tanzania.

Utoaji wa tuzo hizo ulifanyika usiku wa Jumapili iliyopita, Novemba 14 ambapo mastaa wakubwa wa muziki kutoka nchi tofauti duniani walialikwa kupafomu huku kubwa zaidi ikiwa ni msanii kutoka Tanzania, Rayvanny au Chui akiwa mmoja kati ya mastaa walioalikwa kupafomu usiku huo.

Kwa wale tuliofuatilia tukio hilo kubwa barani Ulaya, tulimshuhudia Rayvanny akifanya shoo yenye ujazo wake akiwa na msanii Maluma kutoka nchini Colombia ambapo walitumbuiza kwa pamoja ngoma yao mpya Mama Tetema; hili ni jambo kubwa kwa Tanzania na Afrika kwa jumla.

Rayvanny anatajwa na waandaaji wa tuzo hizo kwamba amekuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika kuitwa kupafomu katika utoaji Tuzo za MTV EMA 2021 tangu kuanzishwa kwake Novemba 24, 1994; yapata miaka 26 iliyopita.

Hakuna shaka na uwezo wa Diamond kwenye muziki barani Afrika, lakini kwa mwaka huu Wizkid alistahili kunyakua Tuzo ya Msanii Bora Afrika.

Kwa kuwa ndilo tukio kubwa linalozingumzwa, IJUMAA SHOWBIZ inakuletea uchambuzi wa sababu kubwa iliyosababisha Wizkid kumgaragaza Diaomond kwenye Tuzo za MTV EMA 2021, twende pamoja;

REKODI ZA DIAMOND 2020/2021

Ukiachana na ngoma mbalimbali kubwa alizowahi kufanya Diamond, lakini Ngoma ya Waah inaonekana kuwa ni sababu kubwa ya kumfikisha kwenye Tuzo za MTV EMA mwaka 2021.

Ngoma ya Waah aliyomshirikisha Maestoro wa Rhumba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide au Le Grand Mopao Mokonzi aliiachia rasmi Novemba 25, 2020 huku video akiiachia Novemba 30 kwenye Mtandao wa YouTube; video ya ngoma hiyo ilifikisha jumla watazamaji zaidi ya milioni 1 kwa muda wa saa 8 tu, huku ikiwa na zaidi ya watazamaji milioni 2 ndani ya saa 24 tu.

Ngoma ya Waah ilivunja rekodi iliyowekwa na mkali kutoka Nigeria, Davido ambaye kupitia ngoma yake ya Fem alifanikiwa kupata watazamaji zaidi ya milioni 1 kwa saa 9 pekee huku Diamond akifikisha idadi kama hiyo ya watazamaji ndani ya saa 8 pekee!

Hadi sasa kwenye Mtandao wa YouTube, ngoma hiyo ya Waah ina jumla ya watazamaji zaidi ya milioni 91 ikiwa na miezi 11 tangu kuachiwa kwake. Ukweli ni kwamba, Waah imemfikisha Diamond sehemu kubwa.

REKODI ZA WIZKID 2020/2021

Wizkid aliachia albam yake inayokwenda kwa jina la Made in Lagos, Oktoba 30, 2020 huku ndani yake kukiwa na Ngoma ya Essence aliyomshirikisha mkali mwingine wa Nigeria, Tems.

Ngoma ya Essence imefanya maajabu kiasi cha staa mkubwa wa muziki duniani, Justin Bieber akamuomba Wizkid wafanye remix ya ngoma hiyo. Essence ya Wizkid aliyomshirikisha Tems imetunukiwa cheti cha Certified Platinum nchini Marekani, huku akiweka rekodi ya kuwa Mwafrika na Mnigeria wa kwanza kufika hatua hiyo.

Pia ngoma hiyo ya Essence ilishika nafasi ya 54 kwenye Bill Board Hot100; yaani kati ya noma 100 kali duniani.

Pia Essence Remix aliyofanya na Justin Bieber hadi sasa inapepea kwenye nafasi ya 12, ikiwa imewahi kukamata nafasi ya 9 wakati ikiwa na wiki 19 tu kwenye chati za Billboard Hot100.

Kwa upande wa Billboard Global200; ngoma hiyo hadi sasa inakamata nafasi ya 84, ikiwa umewahi pia kushika nafasi ya 28 na kudumu kwenye chati kwa muda wa wiki 17.

Kama ulikuwa hujui, Billboard ni mtandao mkubwa duniani unaopanga wasanii kulingana na ukubwa wa mauzo ya ngoma na idadi ya wasikilizaji duniani kote. Hivyo hatua hiyo aliyofika Wizkid siyo ya kuchukulia poa.

KWA NINI WIZKID KAMGARAGAZA DIAMOND?

Hakuna asiyejua balaa la Diamond kwenye muziki, lakini ni kama Wizkid alistahili kunyakua tuzo hiyo kwa mwaka 2021 kutokana na rekodi za ngoma yake hiyo ya Essence.

Baadhi ya wadau wa muziki Bongo hawaamini kwamba Wizkid ana uwezo mkubwa wa kuimba na kupafomu zaidi ya Diaomond.

Wanaamini Wizkid kupitia ngoma yake ya Essence ndiyo iliyomgaragaza Diamond na kusababisha kukosa Tuzo za MTV EMA kwa mwaka 2021.

Kwa balaa la Wizkid kwa mwaka huu, hakukuwa na msanii yeyote wa kumshinda kati ya wale waliokuwa wanashindania tuzo hiyo akiwemo Diamond Platnumz. Ukweli ni mchungu, lakini ni lazima tuuongee, Diamond anastahili kabisa kupata Tuzo ya MTV EMA, lakini hakustahili kwa mwaka huu mbele ya Wizkid ila huko mbeleni atachukua tuzo hizo mfululizo! Kila la heri!