Uko hapa: NyumbaniBurudani2021 07 22Article 547900

Burudani of Thursday, 22 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Zuchu, Nandy kupanda jukwaa moja

Zuchu, Nandy kupanda jukwaa moja Zuchu, Nandy kupanda jukwaa moja

WASANII wa kike wanaofanya vizuri kwa sasa, Zuhura Othman ‘Zuchu’ na Faustina Charles ‘Nandy’ ni miongoni mwa nyota 18 wanaotarajiwa kupanda jukwaa moja kutumbuiza katika tamasha la muziki litakalofanyika Kiroka mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Mdau wa burudani na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Hamis Taletale ‘Babu Tale’ kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram, nyota hao watatumbuiza katika tamasha maalumu linalojulikana kama ‘Waukae Fest’ litakalofanyika mwezi ujao.

Katika orodha aliyotoa, inaonesha Zuchu na Nandy watapanda jukwaa moja kutoa burudani, sambambasa na wasanii wengine wengi.

Wasanii hao kila mmoja akiwa na uongozi wake na mashabiki wake wamekuwa ni habari ya mjini wakishindana kutoa nyimbo zinazovutia masikio ya mashabiki wengi.

“Nimeona nishirikiane nanyi katika kutumia sanaa na michezo kama fursa kwa kuanza na tamasha la Waukae Fest’ ambayo ni ya kwenu Wana Morogoro Kusini Mashariki,”Babu Tale aliandika ujumbe huo.

Alisema matamanio yake makubwa ni kutekeleza majukumu ya heshima waliyompatia Wana-Morogoro Kusini Mashariki kwa kufanya Jimbo hilo kuwa sehemu ya dunia.

“Fahari pekee kwangu ni kuihusisha jamii yetu na kila fursa njema kwenye kila nyanja ikiwemo Uchumi, Siasa, Sanaa na Michezo, mimi naamini Sanaa na Michezo inafungua milango ya uchumi,”alisema.

Mbali na wasanii hao baadhi ya wengine walioko kwenye orodha hiyo ni Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, Mbwana Kilungi ‘Mbosso’, Abdul Idd ‘Lavalava’, Mwanahawa Abdu; ‘Queen Darleen’, Mzee wa Bwax, Dulla Makabila na Lulu Diva.