Uko hapa: NyumbaniBurudaniAina za Muziki

Bongo Flava

Bongo Flava ni jina badala la muziki wa Hip hop ya Tanzania. Mtindo huu ulianzishwa kwenye miaka ya 1990, hasa ukiwa kama mwigo au utokanaji wa hip hop kutoka Marekani, ikiwa na ongezeko la athira ya muziki wa reggae, R&B, afrobeat, dancehall, na mitindo ya asili ya Kitanzania kama vile taarab na dansi, muunganiko ambao umeunda mtindo wa pekee wa muziki.[1] Mashairi kwa kawaida huwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza.

Leo, bongo flava ndio mtindo maarufu wa muziki miongoni mwa vijana wa Tanzania. Aina hiyo inahusiana na mtindo wa Amerika wa hip hop na mtindo wa R&B. Aina hiyo iliundwa miaka ya 1990, kama mchanganyiko wa hip-hop ya Amerika, na ushawishi wa ziada kutoka kwa reggae, R&B, afrobeat, dancehall na mitindo ya kitamaduni ya Kitanzania kama vile taarab na densi ya hapa.

Mtindo wa Bongo Flava kawaida huimbwa kwa Kiswahili au Kiingereza, ingawa wasanii wachache wameweza kuuimba kwa lugha za kienyeji. Muziki umejitokeza nje ya nyumba yake ya kihistoria ya Tanzania; inaenea Afrika Mashariki na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Muziki una nafasi muhimu sana karibu katika jamii zote za ulimwengu, na kwa kweli, ni asili ya mwanadamu. Mataifa yanaelezea hisia zao za kawaida katika muziki. Afrika ni tajiri haswa katika muziki na kila kabila limekuza aina yake. Muziki ni moja wapo ya mambo muhimu ya mila yetu.

Muziki nchini Tanzania una aina anuwai, kama vile pop, taarab, densi na injili na imefanya maendeleo makubwa kama inavyoonekana katika kuibuka kwa vikundi vingi vya kisanii ambavyo mara nyingi huvutia watazamaji wengi. Wasanii wengi wa Tanzania wametunga ripoti kubwa ya nyimbo za hali ya juu za kisanii.

Wakati wa miaka ya mapema ya harakati za Ukombozi wa Kiafrika kama vile Ngoma ilitumika kuomba msaada kwa mapigano ya ukombozi, kutangaza itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea - mfano mzuri ni mwimbaji maarufu Mbaraka Mwaruka Mwinshehe na Moro Jazz ambao walikuwa na nyimbo zinazouza ujanibishaji; wengine walikuwa Marijan Rajab na Cuban Marimba, kutaja wachache.

Mbali na kuwa nyenzo ya mapambano ya ukombozi, muziki umewanufaisha vijana wengi kupitia aina mpya maarufu kwa jina la Bongo Flava. Ilifungua uwanja mkubwa wa ajira katika uhandisi wa sauti na mchanganyiko, nafasi anuwai katika kuelekeza na utengenezaji, uandishi wa maandishi, taa, kamera na ujenzi wa seti na kadhalika. Bongo flava imeleta umaarufu na utajiri wa wastani kwa vijana wengi wa kitanzania. Kwa kipato wanachopata wameweza kujenga nyumba na kusaidia wazazi na ndugu zao.

Jina la "Bongo Flava" ni tokeo la matini yaliyoharibiwa kutoka "bongo flavour", ambapo "bongo" ni wingi wa neno ubongo, ambapo mara nyingi huchukua nafasi ya kutaja jina la utani la Dar es Salaam, jiji ambalo aina ya mtindo huu inatokea na wakati mwingine humaanisha pia nchi ya Tanzania. Katika bongo flava, sitiari ya "bongo" inaweza kutaja zaidi maana ya ujanjaujanja wa mtaani, ya msela au masela wingi wake.[2]

Istilahi ya "Bongo Flava" ilitajwa kwa mara ya kwanza mnamo 1996 na Radio One 99.6 FM (moja kati ya redio za kwanza kabisa za binafsi nchini Tanzania) DR wa Redio Mike Mhagama ambaye alikuwa akijaribu kutofautisha kati ya muziki wa R & B na hip hop wa Marekani kupitia lipindi chake maarufu cha redio - 'DJ Show' ambapo enzi hizo vijana chipukizi walikuwa hawajaanza kutamba kwa mitindo yao wenyewe. DJ Show kilikuwa kipindi cha kwanza cha redio kukubali wanamuziki vijana wa Kitanzania wenye athira ya muziki wa Marekani - wakijieleza wenyewe kupitia uimbaji wa rap. Alisema hewani, "Baada ya kusikiliza kibao cha "R & B Flava" kilichoitwa 'No Diggity' kutoka Marekani, sasa inakuja "Bongo Flava" kutoka kwa Unique Sisters, kutoka hapa nyumbani." Baada ya kusema hivyo katika kipindi, istilahi hii ya "Bongo Flava" ikanasa hadi leo hii.

Asili ya mwanzo kabisa na jinsi "Bongo flava" ilivyoanzishwa nchini Tanzania ni kutokana na Taji Liundi akiwa kama kiini cha hadithi hii. Kifupi hakuna asili bila yeye. Taji Liundi pia anajulikana kama Master T, mwasisi, mwanzilishi na vilevile mtayarishaji wa kipindi cha Dj Show alishaanza kupiga nyimbo za wasanii wa ndani tangu mwishoni mwa miaka ya 1994. Mike Mhagama baadaye akajiunga na kipindi akiwa chini ya ukufunzi wa Master T. Aliendelea na kutangaza kipindi hicho peke yake hata baada ya Master T kuondoka Radio One mnamo 1996.

"Bongo flava" ilikaa vizuri sana hata kabla ya rekodi za video au sauti. Vijana mjini Dar es salaam walikuwa wakirap ufukweni mwa bahari kupitia matamasha mbalimbali (yameandaliwa na Joseph Kusaga ambaye anamiliki Mawingu Discothèque, baadaye Mawingu Studios na sasa ni Clouds Media Group), matamasha ya ndani yaliyochukua sura mpya rasmi baada ya kuanzisha mfululozo wa shindano la Yo!Rap Bonanza ambalo lilikuwa likichochewa na DJ Kim "And the Boyz" Magomelo.

Baadhi ya vijana walikuwa wakijipanga au kujiita majina ya kutunga au kundi fulani, baadhi yao walikuwa wakijitegemea au kujiweka katika kikundi fulani katika tukio hilo ilimradi wapate nafasi ya kukamata mic. Moja kati ya waliowahi kutamba katika mashindano ya kushika mic mwanzoni mwa miaka ya 1990 ni pamoja na Adili au Nigga One. Msanii maarufu wa kwanza wa mtindo huu aliyewahi kuiga ngoma za Marekani ni Saleh Jabir ambaye alirap kwa Kiswahili kupitia biti ya Vanilla Ice, "Ice Ice Baby", yeye ndiye aliyeanza kuweka Kiswahili katika rap. Toleo lake lilikuwa maarufu, ilivunja rekodi na kuweza kupigwa hata katika Redio ya Taifa la Tanzania. Ulikuwa wimbo wa kwanza wa rap ya Kiswahili kupaa anga ya Tanzania.

Moja kati ya makundi ya mwanzo kabisa kurekodi na kupeleka CD Radio One ili irushwe ilikuwa bendi ya Mawingu, kundi ambalo lilitamba sana mwanzoni mwa miaka ya 1994. Walirekodia katika Studio za Mawingu. Wanachama wake walikuwa kina Othman Njaidi, Eliudi Pemba, Columba Mwingira, Sindila Assey, Angela, Robert Chuwa, Boniface Kilosa (a.k.a. Dj Boni Love) na baadaye Pamela ambaye aliimba kibao chao kilichovunja rekodi cha RnB/Rap "Oya Msela". Wimbo ulikuwa maarufu mno na baadaye hilo neno likabaki hadi leo. Bendi ya Mawingu hujadilika kama waanzilishi wa ladha aina ya RnB ya Bongo flava. Dar Young Mob lilikuwa kundi la kwanza la hip hop ya kweli kurekodi na Mawingu Studios chini ya utayarishaji wake Dj Boni Love. Lilikuwa kundi la kwanza kupigiwa kibao chao katika redio ya binafsi nchini Tanzania.

Wasanii maarufu

Mwanzilishi wa hip hop ya Tanzania ni Mr. II (pia anajulikana kama Sugu au 2-Proud), ambaye alitoa kibao chake cha kwanza maarufu cha Bongo flava, Ni Mimi mnamo 1995. Mr. II bado yupo hadi leo (rekodi yake ya mwisho ni Coming of Age, ilitolewa mnamo 2007). Kundi la kwanza la hip hop la Tanzania, Kwanza Unit, 1993. Awali walikuwa wanaimba kwa Kiingereza lakini hatimaye wakawa wanaimba kwa Kiswahili. Moja kati ya wanachama wa zamani wa kundi hili ni Professor Jay, kwa ni moja kati ya wasanii maarufu wa hip hop nchini Tanzania. Vilevile kundi la Diplomate lililokuwa na kina Saigon.

Miongoni mwa wasanii maarufu wa Bongo Flava kwa sasa ni pamoja na Ali Kiba, Juma Nature, Lady Jaydee, Mzungu Kichaa, Geezy Mabovu, Q Chillah, TID, Diamond Platnumz, Dknob na wasanii wapya wa Bongo Flava kama vile Nay wa Mitego, Ben Pol, Dogo Fani na wengine wengi. Majina mengine maarufu ni pamoja na Gangwe Mobb, Dully Sykes, na Daz Baba.

Taarab

Kundi la waimbaji wa muziki wa Taarab Zanzibar

Taarab (pia: tarabu, taarabu) ni aina ya muziki ya Afrika ya Mashariki yenye asili yake katika utamaduni wa Waswahili. Neno lenyewe limetokana na Kiarabu "tarab" (???) linalomaanisha "uimbaji, wimbo".

Tabia za taarab

Taarab ni muziki wa Waafrika wa pwani uliopokea athira kutoka tamaduni nyingi, hasa muziki wa Waarabu na Wahindi. Kimsingi ni uimbaji wa mashairi unaofuata muziki wa bendi.

Bendi hizi hutofautiana kieneo: katika taarab ya Unguja vinanda vya kulingana na tarab za Kiarabu hupendelewa; katika taarabu ya Mombasa aina za ngoma ni muhimu; katika taarab ya Tanga gitaa inapendwa. Siku hizi vyombo vya kisasa vimetumiwa pia.

Historia

Neno "taarab" laaminiwa lina asili katika Unguja ambako mnamo 1870 Sultani Sayyid Bargash alialika kundi la wanamuziki kutoka Misri kuja Zanzibar walioleta uimbaji wao aina ya "tarab". Alipopenda muziki huu sultani alimtuma Mzanzibari Mohammed bin Ibrahim kwenda Misri ajifunze vyombo vya huku. Mohammed aliporudi alikuwa mwanashairi wa Sultani akaendelea kuwafundisha marafiki vinanda vyake. Pamoja waliunda kundi la Nadi Ikhwani Safaa linalosemekana ni bendi ya kwanza iliyotumia jina la "taarab".[1]. Kundi limeendelea hadi leo na kujulikana sasa kwa jina la "Malindi Taarab"[2].

Hata hivyo muziki wa Waswahili unaojulikana leo kwa jina la taarab lina asili ya kale kushinda jina hilo ambalo ni kawaida siku hizi. Kuna kumbukumbu kutoka Lamu ya muziki iliyoitwa "kinanda" iliyounganisha uimbaji pamoja na chombo cha kibangala na ngoma ndogo na waimbaji wake walihamia Zanzibar wakaitwa "taarabu" huko.

Taarab katika utamaduni wa Uswahilini

Katika utamaduni wa Waswahili taarab ilikuwa utamaduni wa pekee kwa sababu ilikuwa mahali pekee ambapo wanawake walifika kwenye jukwaa pamoja na wanaume na kuimba. Kwa sababu hiyo taarab imepingwa mara kwa mara na viongozi wa dini walioona aina kadhaa za taarab ni haramu, hazilingani na masharti ya Uislamu, hasa wakati wa mwezi wa Ramadhani na kama watu wanaanza kucheza.[3]

Miaka ya nyuma muziki wa taarab umesambaa hata barani, nje ya utamaduni wa Waswahili: unavuta wasikilizaji katika miji mikubwa kote Afrika ya Mashariki hadi Burundi na Rwanda.

Bendi mbalimbali zimeingiza vyombo vya kisasa vya muziki katika mtindo wao kama vile keyboard na gitaa ya umeme.

Taarab ya Tanga na asili ya Taarab ya kisasa (Modern Taarab)

Waziri Ally akipiga kinanda Lucky Star.

Katika miaka ya 1950 wanawake tisa wa Tanga walijikusanya na kuanzisha kikundi cha kuimba walichokiita Raha til Fuad maana yake Raha ya Moyo. Akina mama hawa chini ya bibie aliyeitwa Mama Akida au aka Mama Lodi, waliendesha kikundi chao wakiwa wanaimba nyimbo za Siti Binti Sadi na tungo zao ambazo waliimba katika melody ya nyimbo za Kihindi zilizotamba wakati huo. Kundi hili liliendelea na kuanza kuruhusu wanaume kujiunga hasa wakiwa wapiga vyombo, akiwemo mtoto wa Mama Akida, Akida Jumbe hatimaye alijiunga na kundi hili kama mpiga accordion kwenye mwaka 1962. Kundi hili ambalo baadaye lilikuja kuitwa Young Noverty, liliendelea mpaka kukaweko na mgawanyiko uliozaa kundi la Shaabab Al Waatan.

Hapa ndipo kukaanza mtindo wa kuweko kundi pinzani jambo ambalo kwa njia ya ajabu sana likawa linadumu kiasi cha miaka kumi kumi. Miaka ya 1960 Young Noverty na Shabaab al Waatan, miaka ya 1970 Lucky Star Musical Club na Black Star Musical Club, miaka ya 1980 Golden Star Taarab na White Star Taarab, miaka ya 1990, Babloom Modern Taarab na Freedom Modern Taarab. Taarab ya Tanga ndo haswa inastahili kuitwa modern Taarab, kwani wao hawakufuata taarab ile iliyoletwa Zanzibar enzi ya Sultan Seyyid Barghash, makundi la taarab ya Tanga yalikuwa madogo na vyombo vyake vilikuwa pamoja na Gitaa la besi, gitaa la solo, drums bongos, akodion au kinanda, nyimbo zao zilikuwa fupi na si ndefu kama za Kizanzibari.

Nyimbo zilitegemea mipigo ya ngoma za asili za kumbwaya na chakacha na hata baadaye mitindo kama rumba, bossa nova ilitumika kama mapigo. Na Taarab ya Tanga ndio iliyoanzisha moto wa vikundi vya taarab Tanzania Bara. Moshi kulikuwa na New Alwatan, AzimioTaarab, na Blue Star Taarab , Arusha-Blue Star Taarab, Dodoma-Dodoma Stars, Kondoa –Blue Stars, Mbeya-Magereza Kiwira, Mwanza-Ujamaa Taarab, Bukoba wakiwa na Bukoba Stars, na muendelezo huu uliingia mpaka Burundi kutokana na mwanamuziki mmoja aliyejulikana kama Athmani Mkongo, alitoka Burundi na bendi yake kufika Tanga akawa mwanamuziki mahiri wa Taarab na hata kuipeleka kwao Burundi na kukaanzshwa huko vikundi kadhaa vya Taarab