Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 11 14Article 487573

Maoni of Thursday, 14 November 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

ANTI BETTIE: Aliniacha, akaolewa ameachika sasa anataka turudiane

ANTI BETTIE: Aliniacha, akaolewa ameachika sasa anataka turudiane

Nina mpenzi na tunapendana, tatizo lake hataki kunihudumia kwa kisingizo cha kusoma.

Nifanyeje?

Mbona umesema kisingizo kwani hujajiridhisha kuwa anasoma? Kama anasoma inawezekana mambo yamekuwa magumu kiasi. Kwa kuwa kusoma kuna muda mvumilie akimaliza masomo utapima kama ilikuwa kweli au alijificha kwenye hicho kichaka cha kusoma.

Unapoambiwa kitu siku nyingine omba ufafanuzi wa kina ukifanya hivyo itakusaidia kujua kama kinachosemwa ni kweli au uongo, ukikubali bila kuhoji unamrahisishia kazi anayekudanganya.

Nasisitiza hatasoma milele na uvumilivu wako wakati huu utakuweka kwenye nafasi nzuri moyoni mwake siku zijazo.

Pia hujaniambia anasoma kwenye daraja gani la elimu, ikiwa chuo sawa lakini kama anasoma sekondari tafadhali jipe shughuli ya kufanya muache kijana wa watu amalize masomo yake kwa amani, usimpe majukumu yanayopaswa kufanywa na wazazi wako.

Kama na wewe unasoma jikite kwenye masomo badala ya kufikiria kuhudumiwa na mwanaume anayesoma na hana kazi, hizo huduma zitakuja kama mana kutoka mbinguni?.

Ameachika anataka turudiane

Nilikuwa na uhusiano na mwanamke kwa miaka minne, akapata mwanaume mwingine akaolewa, wameshindwana sasa anataka turudiane.

Nifanyeje?

Hiki ni kichekesho, mwanamke alikuacha na akapata tu mwingine akaolewa ameachika anataka mrudiane, labda ungenipa sababu nyingine ningekushauri vinginevyo tofauti na hapo atakusumbua,.

Labda aliolewa kwa shinikizo la familia na alifanya hivyo kuiridhisha. Na ulikuwa unalijua hilo na hatari ambayo angeipata iwapo angekataa ulikuwa unaijua, vinginevyo tafuta mwanamke mwingine mtakayependana kwa bahati na siyo usanii kama huu.

Hujaniambia uliishi naye miaka minne bila kumuoa kwa sababu zipi? Inawezekana alifanya hivyo kukukumbusha kuwa anastahili kuolewa. Wanaume acheni ubabaifu unamtumia mtoto wa watu miaka minne kirejareja tu hii siyo sawa. Kama mwanamke unampenda fuata taratibu muishi kihalali, unaweza kuonja kwa bahati mbaya, huoni aibu mkubwa mwenzangu miaka minne!.

Muhimu mwanamke asikufanye nguo ya mtumba, anazurura madukani akishindwa bei anakurudia. Akupe sababu za msingi kwa nini aliamua kuolewa na kukuacha kama hana achana naye.