Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 14Article 557428

Maoni of Tuesday, 14 September 2021

Columnist: globalpublishers.co.tz

Askofu Gwajima, Wenzake Waachwe, Mawaziri Wajiuzulu

Wabunge Jerry Silaa na Askofu Gwajima. Wabunge Jerry Silaa na Askofu Gwajima.

Wabunge watatu wa CCM, Jerry Silaa (Ukonga), Askofu Josephat Gwajima (Kawe) na Humprey Polepole (mbunge wa kuteuliwa), Septemba 3, 2021 walifika mbele ya kamati ya maadili ya wabunge ya CCM na kuhojiwa ikiwa ni kuitikia agizo la Bunge.

Askofu Gwajima na Silaa waliitwa na kamati kwa agizo la Bunge, wakidaiwa kusema uongo na kushusha hadhi ya Bunge, ingawa haikufahamika Polepole ameitwa kwa agizo la nani.

Tayari bunge la Tanzania limewapa adhabu ya kuwasimamisha wabunge wawili Gwajima na Silaa kuhudhuria mikutano miwili ya bunge.

Binafsi sikuona sababu ya Bunge kuhamisha shauri hilo kutoka kamati ya haki na kuiagiza tena kamati ya maadili ya wabunge wa CCM kuwahoji baada ya kukutwa na hatia ya kusema uongo na kushusha hadhi ya bunge na kamati ya Maadili na Haki za Bunge.

Akizungumza mbele ya wandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya CCM Dodoma mara baada ya kumaliza kwa mahojiano na wabunge hao, mwenyekiti wa kamati ya maadili ya wabunge wa CCM Hassan Mtenga, amesema kuwa kamati yake imewahoji wabunge hao kufuatia agizo la bunge.

Aidha Mwenyekiti huyo wa kamati ya maadili ya wabunge wa chama cha mapinduzi CCM, ameweka hadharani sababu ya mbunge wa kuteuliwa wa chama hicho Hamphrey Polepole, kuwa amefikishwa katika kamati hiyo kutokana na kauli zake mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na chanjo ya corona na mafundishi yake ya kibayolojia kupitia mitandao ya kijamii hivyo kuzua taharuki miongoni mwa jamii.

Adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya bunge kwa wabunge Askofu Gwajima na Silaa ilitolewa hivi karibuni na Bunge ikielekeza chama cha CCM kuwahoji wabunge hao kutokana tuhuma zinazowakabili.

Hapo najiuliza; Mbona Bunge limeshatoa adhabu? Kwani inawezekana mtu akitenda kosa kuhukumiwa mara mbili kwa kosa hilohilo?

Askofu Gwajima alifikishwa mbele ya kamati hizo kufuatia kauli zake kuhusiana na chanjo dhidi ya COVID-19 ambazo amekuwa akizitoa katika kanisa lake la ufufuo na uzima kuwa hazifai huku akiwahimiza waumini wa kanisa lake ulimwenguni kote ikiwemo Tanzania kutokuchanja hadi pale serikali itakapotoa ufafanuzi wa kutosha kuhusiana na usalama wa chanjo hiyo.

Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa akikutwa na kosa la kusema uongo ikiwemo kauli yake ya kuwa Wabunge wa Tanzania hawalipi kodi hivyo wanapaswa kulipa kodi kama wafanyavyo wananchi wengine.

Masuala hayo yameshajadiliwa Bungeni sasa kila Mtanzania ameelewa. Lakini Rais Samia Suluhu Hassani alishasema kwamba suala la chanjo ni la hiari sioni sababu ya kuwashupalia wabunge hao.

Kwa kuwa kamati ya wabunge wa CCM ni miongoni mwa wabunge walioshiriki kutoa adhabu kwa akina Gwajima bungeni sidhani kama kulikuwa na sababu ya kuwaita tena baadi ya wabunge kusikiliza hoja ambazo wameshazitolea uamuzi bungeni.

Ningepata nafasi ya kuonana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyepelekewa ripoti na wabunge ningempa ushauri kuhusiana na suala hili. Ningemshauri aachane nalo kwa sababu wameshahukumiwa na Bunge.

Lakini Waziri wa Afya, Dk Doroth Gwajima na naibu wake, Godwin Mollel binafsi nawabebesha lawama kwa sababu wao wakiwa ni wanasayansi mwaka jana waliwaaminishaje wananchi kwamba ‘kupiga nyugu’ kunaipotezea corona? Hii ina maana walisema moja jumlisha moja ni mbili.

Wataalamu hao hao mwaka huu wanasema moja jumlisha moja ni tatu, nani atawaamini? Hakika mawaziri hao wanapaswa kuwajibika kwa kupotosha umma.

Pili; wizara hiyo hiyo awali walitangaza kwamba watu wanaopaswa kuchanjwa ni watu wenye umri kuanzia miaka 50 kwenda juu na wenye magonjwa sugu na kweli ikawa hivyo. Vijana na wasio na magonjwa sugu walifika vituoni kuchanjwa wakanyimwa chanjo.

Serikali ilidhani watakaofika kuchwanjwa watakuwa wengi lakini mambo yamekuwa tofauti; hadi naandika makala haya waliochanjwa wamevuka kidogo laki tatu! Kwa nini tumefeli?

Jawabu linaweza kuwa hakukutolewa elimu juu ya chanjo hiyo ya corona au bado wananchi wameaminishwa na wizara ya afya mwaka jana kwamba unaweza kujikinga na corona kwa kupiga nyungu kama walivyokuwa wakisisitiza mawaziri wake.

Katika utafiti wangu nimegundua kuwa wananchi wengi wamekosa imani na Waziri Gwajima na Naibu Mollel wanaoongoza wizara ya afya kutokana na kauli zao kugeukageuka kama kinyonga kuhusu janga hili la corona.

Wakati wa utawala wa Rais John Magufuli waziri wa afya na naibu wake waliwaaminisha wananchi kwamba chanjo ni mbaya, hili halina ubishi, hawakuwa na ujasiri kama wa Dk Faustine Ndugulile ambaye alisimamia taaluma ya afya, akatumbuliwa.

Sasa je kwa hali ilivyo nani wa kulaumiwa? Inawezekana Askofu Gwajima na Polepole nao waliingia kwenye kubukua wakagundua kitu; nakuweka misimamio waliyonayo sasa.

Ukweli ni kwamba chanjo zinaokoa maisha lakini kusuasua kwa wachanjwaji walaumiwe hao waliopewa dhamana na kusimamia wizara ya afya kwa kuyumbisha watu.

Ningekuwa na uwezo wa kumshauri waziri mkuu, Kasim Majaliwa ningemuomba aachane na akina Askofu Gwajima; awageukie mawaziri hao wa afya, wakiri kwamba walikosea mwaka jana kuaminisha watu nyungu!  

Na Elvan Stambuli