Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 09Article 541693

xxxxxxxxxxx of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Bandari ndogo ya Mkwaja na fursa zake lukuki

PILIKA za watu zinaakisi shughuli mbalimbali katika harakati za kujitafutia kipato kutokana na fursa kubwa ya uwepo wa bahari. Hiki ndicho kitu cha kwanza kinachoitambulisha bandari ndogo ya Mkwaja ambayo ipo chini ya Mamlaka ya Bandari Tanga.

Nilipofika katika bandari hiyo nilikuta magunia mengi ya dagaa waliochemshwa na kuanikwa wakakauka vizuri yakiwa yamepangwa vyema yakisubiri muda wa kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Niliambiwa kwamba soko kubwa la dagaa hawa wa baharini ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mashua kadhaa zilizojipanga katika mwambao wa bandari hii ndogo zinathibitisha kuwa haipo nyuma katika kuliingizia mapato taifa kwa sababu zinaonesha kuwa kuna mizigo inasubiriwa kwa ajili ya kusafirishwa.

Hisia hizo zote zinathibitishwa na Mhasibu wa Bandari ya Mkwaja, Silas Mbwambo, ambaye anasema bandari hiyo, mbali na shughuli za uvuvi, ni mashuhuri kwa usafirishaji wa mifugo hususani ng’ombe na mbuzi pamoja na mazao ya msituni kama mkaa na mbao kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.

Anasema hiyo ndiyo shughuli kubwa katika bandari hiyo inayoingiza fedha ingawa miundombinu yake ni changamoto kwani bado haina gati la kuwezesha kazi hiyo kufanyika kirahisi.

Mbwambo anasema Bandari Ndogo ya Mkwaja inapitisha asilimia 90 ya mkaa wote unaokwenda Visiwani Zanzibar. “Bandari hii ndio hasa inayotumiwa kwa kiasi kikubwa kupitisha mkaa wa Zanzibar ambapo zaidi ya asilimia 90 ya mkaa wote wa Zanzibar kutoka Tanzania Bara unapita hapa,” anasema Mbwambo.

Vivyo hivyo anase,a wanyama karibu wote wanaoelekea Zanzibar kutoka Tanzania Bara wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kuku wanapitia katika bandari hiyo. Sababu ya bandari hiyo kupata bahati ya kupokea mizigo hiyo ni kutokana na ukaribu uliopo kati Mkwaja na Zanzibar.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Bandari Tanga, bandari ndogo ya Mkwaja imefanikiwa kusafirisha jumla ya mifugo 5,906 katika robo ya kwanza ya mwaka 2020 ambapo Januari 20, 2020 ilisafirisha mifugo 2,690, Februari 20 (2,183) na Machi 20 (1,033).

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa katika robo ya pili ya mwaka 2020 Bandari ya Mkwaja ilifanikiwa kusafirisha mifugo 2,374, robo ya tatu mifugo 2,570 na robo ya mwisho ya mwaka 2020 mifugo 3,473 ilisafirishwa kutoka Bara kwenda Zanzibar.

Kutokana na takwimu hizo, Bandari ndogo ya Mkwaja kwa mwaka 2020 ilifanikiwa kusafirisha jumla ya mifugo 19,271 kutoka Tanzania Bara kwenda Visiwani Zanzibar. Kwa mujibu wa Mbwambo hayo ni mafanikio makubwa kwa sababu serikali imefanikiwa kupata fedha nyingi kutokana na ushuru unaokusanywa.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Ngaile anasema kwamba huko nyuma, Bandari ya Mkwaja ilitumiwa na wafanyabiashara kama kichochoro cha kupitishia magendo lakini juhudi za kuwashawishi wananchi kuachana na vichochoro badala yake wapitishe mizigo yao katika bandari kuu zilishindikana.

“Tuliamua tusiwakatishe tamaa na ili kuepuka mivutano tuliamua kufungua bandari ndogo ya Mkwaja ili wakija kupitisha mizigo yao hapo wanatukuta tunamalizana na biashara ziendelee,” anasema Meneja wa Bandari ya Tanga.

Meneja anasema kwa kuwa katika bandari hiyo hakuna miundombinu ya msingi kama ilivyo Bandari ya Tanga, gharama za kupitisha mizigo katika Bandari ya Mkwaja zinatofautiana.

Katika Bandari ya Mkwaja ili kupitisha mzigo wenye uzito wa tani moja mfanyabiashara atatakiwa kulipa kiasi cha dola za Marekani mbili ambazo ni takribani Shilingi 5,000 za Tanzania.

“Bandari ya Mkwaja kuna kipindi kwa wiki inaingiza kati ya shilingi milioni nne mpaka tano, hususan kwa kipindi ambacho mizigo imechanganya kidogo,” anaendelea kufafanua Ngaile.

Kwa takwimu hizo Bandari ya Mkwaja ni kituo muhimu katika kukusanya mapato kutokana na upekee wake katika usafirishaji wa mifugo na mkaa pamoja na mbao. Ikiwa kwa wiki bandari hiyo ndogo inaingiza kiasi cha shilingi milioni tano, maana yake ni kuwa kwa mwezi inaweza kuingiza zaidi ya shilingi milioni 20.

Katika kipindi cha mwaka mzima Bandari ya Mkwaja kwa kuzingatia takwimu za kila wiki na kila mwezi, inaweza kuingiza kiasi kinachofika shilingi milioni 240.

Mhasibu wa Bandari ya Mkwaja, Silas Mbwambo anasema ingawa bandari hiyo inafanya kazi kwa ufanisi, inakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile kukosekana kwa majengo kwa ajili ya maofisa wa bandari.

“Hapa hatuna jengo tunaloweza kulitumia kama ofisi zetu, tunakaa katika mazingira ya wazi mvua yetu jua letu. Tuliahidiwa na meneja kuwa tutaletewa kontena lakini mpaka sasa hatujaletewa hali inayotufanya kufanya kazi katika mazingira magumu,” anafafanua Mbwambo.

Mbali na changamoto hiyo, Mbwambo anasema utendaji wa kazi katika bandari hiyo ni changamoto kutokana na kukosekana kwa mitandao ya simu ambao kwa kiasi kikubwa inatumika katika malipo.

Anasema kuna wakati ofisa wa bandari anatoka kwenda kutafuta mtandao ili kuharakisha ulipaji wa ushuru na kuepuka kuchelewesha mizigo ya wateja kwenda Zanzibar.

Maelezo hayo na biashara kubwa inayoendelea katika bandari hii ndogo inaonesha kwamba makampuni ya simu za mkononi ikiwemo Kampuni ya Simu Tanzania, bado wamelala katika kuchangamkia fursa za kupeleka mawasiliano katika eneo hili la Mkwaja. Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) nao unapaswa kuliangalia eneo hili ili kulipelekea mawasiliano kama itaonekana kwamba bado halizivutii kampuni nyingi za simu kupeleka mawasiliano.

Wananchi wanaofanya shughuli zao katika eneo linalozunguka bandari hiyo wanafurahia maisha kutokana na uwepo wa bandari hiyo ndogo katika eneo lao. Ernest Mlanzila anasema awali mji huo haukuchangamka lakini baada ya kuanzishwa kwa bandari hiyo mji umechangamka.

Mlanzila ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo katika eneo hilo anaishukuru Mamlaka ya Bandari Tanga kwa kuanzisha kuirasimisha bandari ndogo ya Mkwaja kwani watu wengi sasa hivi wanakuja kuuza na kununua vitu hapo.

Kwa upande wake, Sophia Juma maarufu kama Mama Dagaa ambaye anajishughulisha na kazi ya kukaanga na kuuza dagaa anasema ujio wa bandari ya Mkwaja ulikuwa ni ‘Mgeni Njoo Mwenyeji Apone’ kwa kuwa bandari hiyo imefungua fursa nyingi za maisha Mkwaja.

“Wananchi wengi tunamudu maisha yetu kwa kusomesha watoto na kulipia pango la nyumba kutokana na Bandari ya Mkwaja kutuletea watu wengi wakiwemo wa nje ya nchi na ndani ya nchi. Hiyo yote ni fursa,” anasema Mama Dagaa.

Bandari ni eneo lolote ambalo chombo cha majini, hata kama ni mtumbwi, kinakwenda, inaweza kuwa kwa madhumuni ya kufanya biashara lakini pia inaweza kuwa kwa sababu ya kujihifadhi dhidi ya upepo mkali. Kipindi kile chombo kimesimama pale, kwa mujibu wa sheria, eneo hilo ni bandari.

Kwa mujibu wa sheria namba 17/2004 iliyoanzisha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), bandari zote zinatakiwa kuwa chini ya mamlaka hiyo.

Join our Newsletter