Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 27Article 581461

Maoni of Monday, 27 December 2021

Columnist: Mwanaspoti

Biashara United inavyoshindwa biashara ya soka

Matokeo ya siku za karibuni sio ya kuridhisha Matokeo ya siku za karibuni sio ya kuridhisha

Mkoani Mara pale mjini Musoma kuna timu ya soka inayoitwa Biashara United Mara inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Hii ni miongoni mwa timu ambazo katika miaka ya hivi karibuni ikiwemo msimu uliopita imekuwa ngumu kufungika na kujipatia jina la ‘Wanajeshi wa Mpakani’.

Jina hilo halikuja kizembe, lilikuja kutokana na ubabe waliouonesha Biashara kuwa wanaweza kufanya biashara ya soka kwa ‘level’ kubwa na kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita nyuma ya Simba, Yanga na Azam.

Sifa kubwa ya Wanajeshi ni uvumilivu, wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wadau na mashabiki wa wanajeshi hao wa mpakani msimu uliopita walikuwa wavumilivu kweli na kufikia malengo yao.

Mishahara ilikuwa tabu kulipwa kwa wakati, safari za kwenda kwenye vituo vya mechi zilikuwa za kusuasua, kambi ndio usiseme lakini walivumilia na kutoboa hadi kufikia malengo yao lakini msimu huu Biashara inaonekana kushindwa biashara asubuhi kabisa.

Upambanaji wa msimu uliopita uliifanya kushiriki katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu lakini licha ya wachezaji kupambana ndani na nje ya uwanja kupata matokeo chanya lakini wenye Biashara yao (Uongozi), walishindwa biashara ile ya kimataifa na kurudi kudunduliza ndani ya nchi.

Timu inayowakilisha nchi inashindwa kusafiri kwenda Libya kucheza mechi ya marudiano hatua ya mtoano ambayo ilihitaji sare au ushindi kusonga hatua ya mtoano kisha makundi ambapo ingepata pesa zaidi ya 50 milioni. Inasikitisha sana.

Sahau kuhusu hilo la kimataifa, labda viongozi na wadau wa timu hiyo walipima maji yale kwa kijiti wakaona hawawezi kuogelea ikabidi warudi masikani kupambania ugali wao kwenye Ligi Kuu lakini cha kusikitisha zaidi na huku wamechemka hadi sasa.

Biashara sio wanajeshi shupavu tena kwani ndani ya vita (mechi), tisa walizopigana hadi sasa wameshinda moja tu kutoshana nguvu na mpinzani mara tano na kuchapika mara tatu, lakini hadi leo baadhi ya wanajeshi wanaendelea kuwakimbia na wengine wapo njiani kuhamia katika majeshi mengine (timu).

PICHA LIKO HIVI

Jumapili hii timu hiyo itakuwa ina mechi na Yanga pale Uwanja wa Mkapa lakini hadi sasa kikosini mambo si mambo japo wenyewe hawataki kuthibitisha hilo. Taarifa za kuaminika ni kwamba licha ya timu kupata pesa za mgao wa udhamini wa Azam Media, GSM na mikataba mingine lakini asilimia 75 ya watumishi wa timu hiyo wanadai.

Sio makocha, wachezaji na baadhi ya viongozi, kila mmoja anaidai Biashara. Hadi tunaingia mitamboni tulikuwa hatujafahamu kama Kocha mkuu wa timu hiyo Mkenya Patrick Odhiambo na msaidizi wake Marwa Chamberi kama wamesafiri na timu kuja Dar es Salaam.

Zinaelezwa sababu nyingi za wao kutokuwepo kikosini lakini kubwa ni kwamba Odhiambo amepata ofa ya timu ya hapa hapa Bongo moja wapo ikitajwa kuwa ni Geita ambayo inaweza kumlipa vizuri na kwa wakati hivyo yupo kwenye hatua za mwisho za kumalizana nayo na kwa siku chache zilizopita timu imefanya mazoezi bila kocha mkuu.

Achana na hizo za kocha ishu nyingine inayoonesha kuwa Biashara imeshindwa Biashara ya Soka msimu huu ni baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kuomba kuondoka kutokana na kutopewa stahiki zao kwa wakati na wengine kupata timu nyingine.

Hilo pia litupilie mbali, kuna hili la wachezaji wa kigeni ambao walisajiliwa mwanzo wa msimu na kocha kuwaweka kwenye mipango yao lakini hadi leo hawajapata vibali vya kucheza ambavyo kiuhalisia kwa taasisi kama Biashara United yenye wadhamini na wafadhili tofauti ni suala dogo tu, lakini wao wameshindwa.

Biashara tayari imemuuza nyota wake Denis Nkane kwa Yanga, mshambuliaji wake tegemeo Deogratius Judika ‘Mafie’, yupo Uarabuni kwenye majaribio ambayo yanakaribia kutiki, nahodha wake AbdulMajid Mangalo yupo mbioni kujiunga na timu nyingine akihusishwa na Azam, Polisi Tanzania na Kagera Sugar.

Kuna kauli ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Hassan Suluhu aliwahi kutoa katika moja ya shughuli zake za kila siku kwa kusema “Ukishindwa sema tukusaidie,” sasa Biashara inaonekana kushindwa lakini haitaki kusaidiwa kwani upatikanaji wa taarifa za uendeshaji wa klabu umekuwa mgumu.

Sio shida kwa timu kuomba msaada, shida ni kukaa kimya ilhali kuna matatizo mengi ndani yake.

WASIKIE WADAU

Mdau wa soka nchini ambaye pia ni mmiliki wa timu ya African Lyon inayoshiriki Ligi ya Championship Rahim Kagenzi ‘Zamunda’ amekichambua kinachoendelea kwa Biashara na kudai hayo lazima yatokee kwa timu ambazo hazina uimara wa uchumi.

“Kwa Tanzania ni ngumu zaidi kwa timu za wanachama kukaa muda mrefu kwenye kiwango na ubora ule ule. timu za hivyo kama Biashara nyingi zina siasa ndani yake, watu wanaingia kufanya kitu ili wanufaike jambo ambalo kwa baadae huleta shinda na ndio kinatokea kwa timu hiyo kwa sasa,” anasema Zamunda.

“Mpira wetu unapaswa kusimamiwa na wajuzi wa mpira sio kila mtu anaweza kusimamia hivyo sera zetu na viongozi kushindwa kuwa wabunifu na kuijua vyema Biashara ya Soka,” anasema Zamunda.

Naye moja ya kiongozi wa zamani wa timu hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema kuwa kinachoikwamisha Biashara ni kushindwa kusimamia vyema dhana ya soka Biashara na kuifanya kuwa timu ya watu kadhaa.

“Ndani ya Biashara kuna mambo mengi ambayo hayaendi kiweledi, kuna baadhi ya viongozi hawashauriki, wanaamini kuwa wanajua kila kitu kuhusu mpira na timu ni yao pekee hivyo mambo yakiwawea magumu ndio wanaanza kujitokeza nje na kuomba msaada,” anasema kiongozi huyo.

Walipotafutwa viongozi wa Biashara kuzungumzia hili, hawakuwa na ushirikiano na baadhi yao walidai wapo kwenye vikao hivyo hawawezi kuzungumza kwa wakati husika.