Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 22Article 552943

Maoni of Sunday, 22 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Buriani Mwalimu, tangulia Kashasha

Aliekuwa Mchambuzi wa Masuala ya Soka, Mwalimu Kashasha Aliekuwa Mchambuzi wa Masuala ya Soka, Mwalimu Kashasha

Kiumri alikuwa zaidi ya baba, lakini ukweli ni kwamba alikuwa ni zaidi ya mwalimu. Namzungumzia mtaalamu, Theogenes Alex Kashasha a.k.a Mwalimu Alex Kashasha.

Ngoja niseme, watu wengi walikuwa wanamuona Mwalimu Kashasha kama mtu anayependa kunogesha au kutia chumvi nyingi kwenye uchambuzi wake wa soka kutokana na maneno mengi ya Kiingereza aliyokuwa anayatumia. Alikuwa ni mtu mwenye ‘teminoloji’ za kipekee katika uchambuzi.

Mashabiki wa soka waliofuatilia mechi zilizotangazwa na TBC wanamuelewa zaidi kwani aliwapa zaidi ya burudani. Misamiati yake ya kiufundi ilikuwa burudani zaidi kwao. Kwa hakika Kashasha aliwafunika wachambuzi wengine wengi wa soka, kwani alijitofautisha nao.

Katika siku za mwanzoni nilipopata bahati ya kufanya naye kazi ndani ya TBC kabla ya kutua Mwanaspoti, aliwahi kuniambia siri ya kutumia maneno haya. Nakumbuka nilitoka kuchambua mechi yangu ya kwanza redioni iliyozikutanisha Tanzania Prisons na Simba mwaka 2019 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Muda mfupi baada ya matangazo kumalizika alinipigia simu na nilipopokea tu alianza kwa kunipa pongezi. kisha mwishoni akanimbia mbali ya yote Mtupa nimeona una shida ya kukosa misamiati ya kiufundi.

Akasema mpira ni sayansi kama unavyoona udaktari au fani nyingine - kuna maneno ambayo huwa tunayatumia kuuelezea. Yeye alipenda kuishi mpira kama taaluma, ndio maana hata alipokuwa anauelezea ilikuwa lazima aingize taaluma hiyo kwenye uhalisia wa alichosimulia..

ALIKUWA MWALIMU

Nakumbuka 2019 nilipopata nafasi ya kufanya uchambuzi kwenye vipindi mbalimbali katika redio ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC Taifa), nilipata fursa ya kuchambua mechi kadhaa pale yeye alipokuwa hayupo.

Kabla ya kuanza uchambuzui huo ilibidi niwe nakwenda kumuangalia anavyofanya ili siku nikiachiwa jukumu nisishindwe. Hapa ndipo nilipogundua sifa hii ya ualimu. Alijaribu kula muda wake ili kunifundisha kile alichoona kitanijenga.

Kuna wakati ilikuwa nikimaliza matangazo alinipigia simu na kunirekebisha zile sehemu nilizokosea, akinitaka nisome sana machapisho yanayoelezea kuhusu soka ili kuelewa maana halisi ya mchezo huo na sio kukariri.

Jambo kubwa alilonisisitiza ilikuwa kuangalia mpira kwa jicho la kiufundi, kwani wasikilizaji wanataka kusikia zaidi kwa mrengo huo baada ya kuelezwa na mtangazaji nini kilichotokea.

MZALENDO

Sifa yake ya uzalendo niliijua kwenye michuano ya soka Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Cosafa) mwaka 2019, upande wa wanawake ambapo kwenye mechi ya fainali iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex - Chamazi, nilikuwa naye kwenye kijichumba kidogo cha matangazo pamoja na mtangazaji, Jesse John.

Mechi ile iliisha kwa Twiga Stars kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka timu ya wanawake Kenya.

Baada ya mechi kumalizika na watu kuanza kutoka uwanjani, sambamba na fundi mitambo kuanza kufunga vifaa vyao Mwalimu Kashasha aliendelea kusalia kwenye kichumba akiwa kama mtu aliyepigwa butwaa asiamini kilichotokea kwa taifa lake alilopenda. Ilimchukua dakika kadhaa kabla ya kunyanyuka na kutoka ndani.

MTOAJI

Mbali ya mambo mengi mengine, Kashasha alikuwa mtu wa kusaidia. Mojawapo hilo ni pale nilipokuwa naishi Mbagala, ingawa tuliishi maeneo tofauti, lakini ilikuwa kila baada ya kumaliza majukumu Uwanja wa Benjamin Mkapa lazima anichukue kwenye gari lake.

Na kila mara mahali aliponishusha ili yeye aendelee na safari yake ilikuwa lazima aite bodaboda iliyo karibu na kulipa pesa ili inipelekee nilipokuwa naishi. Kumbuka nyakati hizo ndo naanza anza maisha baada ya kutoka masomoni.

HISTORIA YAKE

Mwalimu Kashasha alizaliwa 1957 mkoani Kagera na alianza kucheza soka tangu akiwa mdogo akimudu nafasi ya kiungo mshambuliaji, yaani namba nane na 10 kiasi cha kubatizwa jina la Pele kutokana na jinsi anavyokuwa akiupiga mwingi.

Mbali na kucheza soka, Kashasha pia alikuwa mwalimu kitaaluma wa mchezo huo aliyesomea sayansi ya michezo katika Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza ambako ndiko alikokutana na Waziri Mkuu na kutengeneza timu tishio, kisha alitua Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikohitimu shahada ya sayansi ya michezo.

Kashasha alifundisha shule mbalimbali na vyuo vya ualimu katika masuala ya michezo, hususan soka kabla ya kujifunza kozi tofauti za ukocha kisha akafundisha timu kadhaa na kuibua vipaji mbalimbali.

Mojawapo wa vipaji vilivyowahi kunolewa na Kashasha ni Paul Rwechungura, kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na timu ya Pamba anayeishi nchini Marekani, Riziki Mchumila na Nico Bambaga aliowanoa ndani ya timu ya Mkoa wa Mara.

Katika mahojiano enzi za uhai wake, Kashasha aliwahi kusema amewahi kucheza pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambapo yeye alizungusha dimba la juu na Majaliwa akikipiga winga ya kulia.

Pia alisoma kozi mbalimbali na makocha maarufu nchini kama Sunday Kayuni, Charles Mkwasa na Mohammed Adolf Rishard.

Mwalimu Kashasha alianza kuugua wiki mbili zilizopita na kulazwa Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na figo na kazi yake ya mwisho kusikika redioni ilikuwa ni uchambuzi wa pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kati ya Simba na Yanga lilipoigwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Kwa upande wa gazeti la Mwanaspoti alikuwa mmoja wa wachambuzi kila Jumamosi katika ukurasa wa 12, na mada yake ya mwisho ilitoka ikiwa na kichwa cha maneno ‘Niyonzima, Lamine Moro wameacha alama’. Tangulia Mwalimu, tangulia Kashasha. Hakika umeacha alama katika familia ya michezo.