Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 19Article 543391

Maoni of Saturday, 19 June 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Chipukizi wa ngumi, mateke kuweni makini

Chipukizi wa ngumi, mateke kuweni makini Chipukizi wa ngumi, mateke kuweni makini

MCHEZO wa ngumi na mateke ‘Kickboxing’ ulivuma zaidi miaka ya 2000 kisha hapo katikati ukapotea kidogo na sasa umerejea tena baada ya kupata wadhamini.

Kurejea kwake kwa sasa chini ya muandaaji wa Kichina Fu Guo Dong na mdhamini wao Azam Media kumelenga kuwaibua vijana chipukizi wenye uwezo wa kuucheza.

Gazeti hili lilipata fursa ya kutembelea mashindano hayo yanayofanyika kila Alhamisi katika klabu ya Black Panthers Oyster bay.

Mashindano hayo hakika ni mazuri kwasababu vijana wengi wamepata ajira kwani ushinde au ushindwe huondoki bure ni lazima upate chochote kidogo cha kujikimu kwa siku hiyo.

Changamoto niliyoiona kwa vijana wengi washiriki ni kwamba wanaonekana kutofanya mazoezi ya kutosha na yanayostahili kulingana na uzito wa mchezo wenyewe.

Wapo baadhi walikuwa wakitoka jukwaani hawajiwezi kwasababu wanakutana na mtu mwenye nguvu na aliyefanya mazoezi kushinda yeye na matokeo yake huhemea juu juu kana kwamba anataka kukata roho.

Kuna bondia mmoja baada ya kutoka kwenye mechi yake yalimkuta na kuanza kupepewa na namna alivyokuwa akihema, hakika kwa mtu usiyejua mchezo huo unaweza kuogopa sana.

Lakini ukimtizama muonekano wa muhusika mwenyewe anaonekana dhaifu haendani na kile anachokifanya.

Ila mwenyewe ndio amechagua mchezo huo pengine hupenda au mkwanja ndio uliomvutia kulingana na hali iliyopo ya maisha.

Mbali na huyo, wengine pumzi hukata mapema kwenye ulingo. Hilo ni jambo ambalo mabondia wengi ukiacha hao chipukizi hata wale wazoefu hawajakipa nafasi kubwa ya kukifanyia mazoezi.

Ukimuuliza Hassan Mwakinyo huwa anafanya programu gani ya mazoezi lazima atakwambia kuna muda anakimbia milimani kutafuta pumzi, kuna wakati anakuwa gym na kwingineko.

Huyo anafanya hivyo kwasababu anajitambua na anautambua mchezo anaokwenda kucheza sio wa kitoto.

Jambo lingine ni kwamba, wanahitaji kuwa na watu wa kuwashika mkono. Inapendeza kujiunga na klabu zinazohusika na mchezo huo ili kujifunza mambo mengi yanayohusiana nayo, ikiwemo sheria na nini cha kufanya kuwa bora.

Nasema hivi kwasababu sio kwamba mimi ni mzoefu sana na mchezo huo ila nilichokiona kwa mtizamo wangu wapo ambao walikuwa wanacheza ilimradi wanarusha miguu ovyo, hawajui walenge upande gani wenye pointi, wengine mikono namna wanavyorusha unasikitika moyoni na kucheka.

Sio kwamba nawabeza, pengine washiriki wengi ni wageni wa mchezo, wapo ambao wanafikiri kufanya mazoezi ya ‘gym’ peke yake na kupata mwili kidogo inatosha yeye kushinda sivyo hata kidogo.

Kama kweli wana ndoto ya kuwa mabondia wazuri watafute watu sahihi wanaojua michezo hiyo wawasaidie kutimiza kile wanachokusudia.

Jambo lingine ni kwamba mchezaji anapofanya mazoezi kuna vyakula anatakiwa ale kujenga mwili na vijana wa kisasa pengine hawatambui hilo au wakati mwingine mazingira magumu anayoishi hawawezi kumudu vyakula vinavyotakiwa.

Kabla ya kwenda kwenye mashindano wanahitaji watu wa kuwaandaa kimichezo, kiafya na kisaikolojia, je hayo wanayazingatia?

Kwa mtizamo wangu, nawashauri mabondia ambao asilimia kubwa ni vijana chipukizi wanaokuja kwa kasi kuwa makini kwa kuzingatia mambo mahimu ili kuwa mchezaji mzuri. Wasikurupuke ikiwa hawana mazoezi ya kutosha wala maandalizi kwani inaweza kuwagharimu.