Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 24Article 539419

xxxxxxxxxxx of Monday, 24 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

DARASA LA NDOA… Sababu za kuchokana kwenye ndoa

Takriban katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti.

Kama ulivyo umri wa binadamu, ndoa hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na uzee, na kila kipindi kina mambo yake na taratibu zake ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa hiyo ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.

UTOTO WA NDOA

Hiki ni kipindi cha fungate au wenzetu hukiita Honey Moon na tutafanya tafsiri sisisi ni 'mwezi wa asali'.

Ni kipindi cha raha, utulivu, mapenzi na maelewano baina ya wanandoa. Si lazima kiwe mwezi mmoja kama watu wengi wanavyoamini, bali kinaweza kikawa chini ya mwezi mmoja au zaidi ya mwezi mmoja.

UJANA WA NDOA

Hiki ni kipindi kinachofuatia baada tu ya utoto wa ndoa. Ni kipindi ambacho kila mmoja miongoni mwa wanandoa anakuwa tayari ameshamtambua mwenzake katika shaksia yake (personality) kwa maana ya jinsi anavyoangalia mambo, jinsi anavyofikiri, mitazamo yake, mielekeo yake na matarajio yake.

UZEE WA NDOA

Kipindi hiki ni kipindi ambacho wanandoa wanakuwa tayari wameishaingia katika majukumu ya kulea kwa kupata matunda ya ndoa yao ambayo ni mtoto au watoto.

Kuchokana mara nyingi hutokewa katika kipindi hiki adhimu ambacho, kwa bahati mbaya, ndicho wanatakiwa kushikamana sana katika kulea watoto wao kwa pamoja, katika mahaba na raha.

Kuchokana kwa wanandoa ni tatizo ambalo linatokea kwa familia nyingi, na kusababisha migogoro mingi na hata kufikia familia kuvunjika au kuishi kwa ajili tu ya kulea watoto na si vinginevyo.

Utakuta katika baadhi ya familia, baba na mama wanaishi katika nyumba moja, ukiwaona utadhani ni mume na mke wanaopendana, kumbe wanaishi kwa ajili tu ya kuwalea watoto wao na kuogopea maneno ya watu.

Hali hii ni hali ya talaka ya kimapenzi (emotional divorce) na ni hali mbaya ambayo mara nyingi humpa msukumo mwanamume wa kuoa mke wa pili katika harakati za kutafuta utulivu na sehemu ya kukimbilia.

Tatizo hili la kuchokana kwa wanandoa linasababishwa na wanandoa wote wawili kutokuwa na kukosa uelewa wa kutosha juu ya haki za mume na mke kama zilivyobainishwa na baadhi ya vitabu vya dini.

Katika makala haya nitafanya marejeo zaidi kwa kutumia vitabu vya dini ya Kiislamu lakini kila mwanandoa, bila kujali dini yake, ninaamini akisoma makala haya hadi mwisho atanufaika.

Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani (30:21): Na katika ishara zake ni kuwa; Amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika haya zimo ishara kwa watu wanaofikiri.

Aya hii ambayo ni miongoni mwa aya zinazosomwa mara nyingi katika ndoa za Kiislamu lakini pengine ni wachache wanaopata mazingatio inatuwekea bayana nguzo zinazosimamisha nyumba ya ndoa, nazo ni nguzo kuu tatu: utulivu, mapenzi na huruma.

Hapa inaonesha utulivu huletwa na mwanamke, na ndio maana aya ikatafsirika “ili mpate utulivu kwao”.

Utulivu huzaa mapenzi na huruma baina ya wanandoa, kwa maana nyingine, mwammke ana nafasi kubwa ya kujenga au kubomoa ndoa.

Hii haina maana kuwa mwanamume hana nafasi ya kuharibu, bali nafasi ya mwanzo inachukuliwa na mwanamke anaposhindwa kuleta utulivu kwa mumewe.

Kwa hekima za Mwenyezi Mungu, amewaumba wanawake tofauti na wanaume kimaumbile (physical), kihisia (emotional), na kinafsi (psychological), hii yote ni kwa ajili ya wadhifa na majukumu yao katika jamii.

Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani 3:36: “Na Mwanamume si sawa na Mwanamke.”

Hivyo basi, sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yake.

Na katika muktadha huu nitajaribu kujadili baadhi ya visababishi vinavyopelekea kuzeeka kwa ndoa au kuchokana, visababishi ambavyo huwa vinadharaulika na kuonekana vitu vidogo vidogo hususan kwa wanawake wengi.

KUZOENA

Kuzoeana baina ya wanandoa ni jambo zuri, kwa maana ya kila mmoja kumfahamu mwenzake, lakini kuzoeana huku kunaweza kuzalisha dharau hususan kwa upande wa mwanamke kwa kutojali usafi wake, mavazi anayovaa, chakula anchopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla.

Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia hizo, ambazo huenda ikawa hazitokani na dharau, bali kuzoeana.

Kwa mfano: siku za utoto wa ndoa mwanamke huwa anajali sana usafi wa mwili wake, umaridadi wa nguo anazovaa, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu, upishi wa chakula unaozingatia vionjo na ubunifu.

Katika kipindi hiki mapokezi huwa ni yenye bashasha na wakati mwingine hata kumkumbatia mumewe arudipo kutoka kazini.

Lakini baada ya kuzoeana, yote hayo hubadilika. Mwanamke huhisi kuwa hana jipya la kumwonyesha mumewe, hujiona wameishakuwa watu wazima sasa, na mara nyingi utakuta mwanamke huyu anashinda na sare (uniform) moja kuanzia asubuhi hadi anapopanda kitandani usiku.

Mambo ya hina, nguo za fashion, salon, manukato, kujipamba na dhahabu huyafanya pale anapotoka kwenda harusini, sokoni na kwenye mialiki na sio anapokuwa nyumbani.

Kwa mfano, hata baadhi Waislamu hawajui kwamba mahala ambako mwanamke anatakiwa kuvaa kimini ni ndani kwake, akiwa na mumewe!

Huku ndio kuzoena, na tafsiri sahihi ni kudharau. Mtume Muhammad (SAW) Anasema: Mwanawake bora (wake zenu) ni yule ambae ukimwangalia anakufurahisha, na ukimuamrisha anakutii (An-Nasaaiy).

Katika kipengele cha utii, Biblia pia inasema mume ni kichwa cha nyumba.

Mazungumzo

Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na kuiimarisha. Aidha ni njia ya mkato ya kuchokana na kuchukiana.

Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini na wakati gani asiseme, hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake.

Kwa mfano: Mwanamke ambaye kila anapoongea na mume wake huanza mazungumzo yake na matatizo na lawama humfanya mumewe awe na woga kila anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba chungu, kwa sababu hakuna binadamu anayependa kusikia matatizo tu wakati wote.

Mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe kwa hamu kubwa, na anapofika tu na kabla hata ya kupata riziki, anaanza kumsomea orodha ya matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa, shangazi yako amepiga simu mjomba kalazwa hospitali na kadhalika na kadhalika. Nyumba ya aina hii huzeeka haraka na wanandoa kuchokana.

Mtume Muhammad (SAW) anausa: Fanyeni wepesi msiwatie (watu) uzito, na toeni habari za furaha, wala msiwakimbize (Al-Bukhaariy).

KUSOMANA TABIA

Ni udhaifu mkubwa kwa wanandoa ambao wana mwaka mmoja katika ndoa yao wakawa bado hawajasomana tabia, au wakawa wameshasomana tabia, lakini kila mmoja akawa anataka tabia zake ndio ziwe dira.

Kwa mwanamke mwenye busara na mwenye kuithamini ndoa yake, husoma tabia za mumewe na kuangalia jinsi gani anavyoweza kuzioanisha na zile zake ili kuepusha migongano. Aidha hutafuta fursa mwafaka ya kumkinaisha mumewe juu ya fikra fulani au tabia fulani ambayo yeye haridhiki nayo.

Ni muhimu kwa mwanaume vilevile kuzisoma tabia za mke wake, vitu gani vinamuudhi, na vitu gani vinamfurahisha. Maisha ya ndoa ni kuwa tayari kuacha hata mambo unayoyapenda kama ni karaha kwa mwenzio.

Mtume Muhammad alikuwa anajua tabia za mkewe Aisha wakati gani anakuwa amekasirika na wakati gani amefurahi, kama ilivyokuja katika hadithi Mtume akimwambia mkewe:

Hakika mimi najua wakati ukikasirika na ukifurahi, (‘Aisha) akasema; unajuaje? Ukiwa na furaha husema, Laa naapa kwa jina la mola wa Muhammad, na ukiwa umekasirika husema, Laa naapa kwa jina la mola wa Ibrahimu.

Mwandishi wa makala haya ni shehe na msomaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni 0784 448 484

Itaendelea

Join our Newsletter