Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 15Article 542818

Maoni of Tuesday, 15 June 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Dhana ya PPP katika kukuza uchumi

Dhana ya PPP katika kukuza uchumi Dhana ya PPP katika kukuza uchumi

AKIWASILISHA Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2021/22 bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alieleza umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia miradi ya maendeleo ambayo inakusudiwa kutekelezwa na serikali.

Katika hotuba yake hiyo, Dk Mwigulu alieleza kuwa serikali itaendeleza jitihada za kuimarisha mazingira wezeshi kwa kutumia vyanzo bunifu ili kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Vyanzo hivyo ni pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi kwa utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), uwekezaji wa moja kwa moja unaolenga kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi ya uwekezaji na hatifungani za uendelezaji wa miundombinu.

“Serikali itaendelea kutangaza fursa za uwekezaji wa moja kwa moja na kuandaa miongozo kwa ajili ya vivutio vya wawekezaji katika miradi ya maendeleo. Aidha, serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia uwekezaji hususan katika viwanda vya kuongeza thamani vya malighafi zinazopatikana nchini katika maeneo ya dawa

na vifaa tiba, uunganishaji wa magari na mitambo pamoja na uzalishaji wa mafuta ya kula,” alieleza Dk Mwigulu.

Kwa mujibu wa waziri huyo, sekta binafsi nchini imeendelea kukua ikiwa na zaidi ya asilimia 70 ya wajasiriamali katika sekta isiyo rasmi.

“Katika kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu, taifa linahitaji sekta binafsi yenye uwezo wa kuchangia katika utekelezaji wa mpango na kumudu ushindani wa kibiashara. Licha ya uwepo wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) katika ngazi ya taifa, wizara, mikoa na wilaya; na taasisi za uwakilishi wa sekta binafsi zikiwemo TPSF, CTI na TCCIA bado zipo changamoto za uwasilishaji wa taarifa muhimu zinazohitajika katika kufanya mapitio ya mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi ili kuboresha mazingira ya utekelezaji wa mpango,” alieleza.

Aliongeza, “Kwa kuzingatia changamoto hizo, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 umetoa msukumo kwa sekta binafsi kwa ajili ya kuwezesha kufikiwa kwa malengo yake kupitia Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka mmoja mmoja ikiwemo wa mwaka 2021/22.

Licha ya hayo, alieleza kuwa serikali inaendelea kuweka utaratibu wa ukusanyaji wa taarifa za uwekezaji na utekelezaji ili kutoa taswira ya maendeleo yanayowezeshwa na sekta binafsi.

Alieleza kuwa utaratibu huo utajumuisha hatua kadhaa zikiwamo kuhamasisha sekta binafsi kutoa takwimu ili zitumike kupanga mipango na kuandaa sera na mikakati itakayoboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika mijadala kupata maoni yao na kuboresha hatua za kutekeleza mipango na kuleta maendeleo;

Hatua nyingine ni kuiwezesha sekta binafsi kuwa na mifumo ya taarifa ambazo zitasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi; na kuhimiza taasisi za kijamii zikijumuisha mashirika na taasisi za dini zenye mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kuioanisha na Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini.

Dk Mwigulu anafafanua kuwa katika mpango huo kwa mwaka 2021/22, shughuli zitakazotekelezwa ni kuwezesha wizara, taasisi na wakala za serikali nne kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi ya PPP; kuwezesha malipo ya miradi ya PPP; kufanya mafunzo juu ya dhana za PPP kwa taasisi 120 zinazotarajia kuingia mikataba ya PPP; na kuanzisha Kituo cha Ubia (PPP Centre). Alieleza kuwa jumla ya Sh bilioni 3.3 fedha za ndani zimetengwa.

Serikali iliandaa Sera ya PPP ya mwaka 2009 kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya kuishirikisha sekta binafsi kutekeleza miradi ya umma na kuhakikisha miradi hiyo inaandaliwa vizuri.

Kwa mujibu wa Kamishna wa PPP, Dk John Mboya, chimbuko la uamuzi huu, ulitokana na maandalizi hafifu ya miradi kulikosababisha kuwa na miradi isiyokuwa na manufaa na iliyoleta hasara kubwa kwa taifa.

Dk Mboya anaeleza kuwa Sheria ya PPP Sura 103 ilitungwa mwaka 2010 ambayo pamoja na mambo mengine, ilianzisha vitengo viwili – Kitengo cha Uratibu chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Kitengo cha Fedha chini ya Wizara ya Fedha.

Akizungumza hivi karibuni jijini Arusha wakati wa mafunzo kwa wahariri wa vyombo vya habari kuhusu elimu ya utekelezaji wa miradi ya PPP iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Mboya alisema zipo sababu za chimbuko la Sera ya PPP ambayo ilianzaa sheria, kanuni na miongozo.

Alizitaja kuwa ni kukosekana kwa mifumo ya kisera, sheria na kitaasisi inayotoa miongozo na taratibu za kuendeleza na kutekeleza miradi ya PPP; kukosekana kwa uwezo wa uchambuzi wa maandiko ya miradi ya uwekezaji kunakopelekea kuwa na miradi isiyokuwa na tija; na kukosekana kwa mazingira wezeshi ikijumuisha nyenzo za muda mrefu za kugharimia miradi na mgawanyo sahihi wa vihatarishi vya miradi.

Nyingine ni uwezo duni wa kufanya majadiliano ya miradi, ununuzi, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya PPP na mifumo duni ya mgawanyo usio sahihi wa vihatarishi hasi vya miradi kunakosababisha sekta ya umma kubeba vihatarishi hasi kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa Dk Mboya, maana ya dhana ya PPP ni “Mkataba wa muda mrefu kati ya sekta ya umma na mbia wa sekta binafsi, kwa ajili ya ujenzi na/au uendeshaji na usimamizi wa mradi kwa niaba ya serikali, ambapo mbia wa sekta binafsi anabeba kwa kiasi kikubwa vihatarishi vya mradi na jukumu la usimamizi kwa muda wote wa mradi, na malipo yanaendana na utendaji wa mbia, na/au mahitaji ya mradi au huduma husika.”

Alifafanua kuwa PPP ni makubaliano kati ya mamlaka ya serikali na mbia ambayo mbia anatekeleza jukumu la mamlaka ya serikali kwa niaba ya mamlaka ya serikali kwa muda maalum; anabeba vihatarishi hasi vya fedha, ufundi na uendeshaji katika utekelezaji wa jukumu kwa niaba ya serikali au matumizi ya mali ya serikali.

Aidha, alisema analipwa kutokana na utekelezaji wa jukumu la serikali au kutumia mali ya serikali kwa njia ya fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya serikali; tozo zitakazokusanywa na mbia kutoka kwa watumiaji wa huduma husika na malipo kutokana na fedha za bajeti na watumiaji huduma.

Anaongeza kuwa lengo la mkataba wa ubia ni kutumia ubunifu, utaalamu na rasilimali za sekta binafsi kutoa huduma ya umma kwa gharama nafuu kwa mlipiaji wa huduma hiyo; huduma inayotolewa ni dhamana yaani serikali ina jukumu la kuhakikisha ubora wa huduma ya umma inayotolewa ni sawa kama ingetolewa na serikali yenyewe.

“Kwa hiyo kuna ufuatiliaji wa utekelezaji wa makubaliano hayo katika hatua ya ujenzi, uendeshaji, na urejeshwaji wa ‘Asset’ husika. Ni muhimu mradi wa ubia uwe katika Mpango-Kazi wa taasisi ya serikali, uingizwe katika bajeti, upate msukumo wa kisiasa, na uungwe mkono na wadau muhimu ikiwa ni pamoja na wananchi wahusika,” anasema.

Dk Mboya anaeleza kuwa ubora wa mkataba wa ubia unapimwa kwa vigezo vitatu muhimu ambavyo ni je, mianya hasi inakubalika kubebwa na sekta binafsi kwa kiasi cha kuridhisha; je, mlipiaji wa huduma (yaani serikali, mtumiaji au wote kwa pamoja) wana uwezo wa kulipia huduma kwa muda wote wa mkataba.

Na tatu je, ubia unaokusudiwa una manufaa kwa serikali na umma kwa jumla?: huduma bora kwa gharama nafuu, kupanua ajira, kodi kwa serikali, utunzaji mazingira, kuongezeka Pato la Taifa.

Anayataja mambo muhimu ya kuyazingatia katika mkataba wa ubia kuwa ni mkataba ni makubaliano ya miaka mitano hadi 30 au zaidi kumwezesha mwekezaji kurejeshwa gharama zake pamoja na faida; mwekezaji binafsi huwajibika kutafuta fedha kugharamia mradi, usanifu wa mradi, ujenzi; mwekezaji binafsi huwajibika kutafuta fedha kugharamia mradi, usanifu wa mradi, ujenzi na uendeshaji wake.

Mengine ni vyanzo vya mtaji mwekezaji hutokana na mikopo na mitaji ya wanahisa kwa uwiano wa asilimia mfano 70:30, na malipo kwa SPV (kampuni inayoanzishwa na mjasiriamali mkuu) hufanyika pale tu huduma imetolewa kwa ubora na viwango vilivyokubalika.

Usikose kusoma Jumanne ijayo kuhusu manufaa, faida za PPP na miradi iliyokwisha andaliwa chini ya PPP.