Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 07Article 555676

Maoni of Tuesday, 7 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Diamond na Tanasha mabonde, milima ya mapenzi

Diamond na Tanasha Diamond na Tanasha

Jina halisi kwenye hati ya kusafiria ni Tanasha Donna Oketch, baba yake ni raia wa Italia, mama akitokea Kenya, majina anayotumia ni ya upande wa mama yake kutokana hakuishi na baba.

Kabla ya kuanza utangazaji wa redio na muziki, Tanasha alikuwa akifanya mitindo (commercial modeling) chini ya Dominique Model’s Agency huko Brussels nchini Ubelgiji. Mrembo huyo mwenye elimu ya shahada (degree) katika mambo ya utalii, anaweza kuzungumza lugha tano duniani kwa ufasaha, nazo ni Kiingereza, Kispania, Kifaransa, Kiholanzi na Kiswahili.

Awali kabisa Tanasha alitumia jina la Zahara Zaire kwenye kazi zake lakini upande wa mitandao ya Instagram na Twitter ili kujitambulisha ametokea Afrika baada ya kuishi Ubelgiji kwa kipindi kirefu.

Tanasha ni mwanamke wa pili nchini Kenya mwenye wafuasi (followers) wengi Instagram, akiwa nao milioni 3.2 akiwa ametanguliwa na Mcheza Filamu, Lupita Nyong’o mwenye watu milioni 9. Tanasha aliyezaliwa katika jiji la London, Uingereza alipata umaarufu mkubwa Tanzania mwaka 2015 alipotokea kwenye video ya wimbo wa Alikiba na Christian Bella ‘Nagharamia’ ikiwa ni video yake ya kwanza kufanya.

Inaelezwa video ya wimbo huo ilishakuwa imefanyika na mrembo mwingine ila haikutoka kwa kiwango kinachotakiwa, hivyo ikarudiwa.

Kabla Kiba na Bella hawajamnasa, Tanasha alihitajika kwenye video ya wimbo wa msanii kutoka Nigeria, Runtown uitwao Mad Over You lakini wakashindwana upande wa malipo.

Desemba 2018 ziliibuka tetesi kuwa msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz amezama katika penzi jipya na Mtangazaji wa kituo cha redio, NRG nchini Kenya ambaye ni Tanasha.

Penzi likamea na kushamiri, wakagonga vichwa vya habari runingani, redioni, wakatawala kurasa za burudani kwenye magazeti na kuteka mazungumzo mtandaoni.

Januari 13, 2019 Diamond alimtambulisha Tanasha kwa mama yake mzazi, Bi. Sandra maarufu kama Mama Dangote, pamoja na ndugu zake wengine akiwemo dada yake, Esma Platnumz.

Tanasha amezaliwa siku moja na mama yake Diamond, tarehe zao za kuzaliwa zinasoma Julai 7, Tanasha akiwa amezaliwa mwaka 1995, huku Mama Dangote ikiwa ni 1971. Kutokana na hilo, Julai 7, 2019 siku ya kuzaliwa kwao, Diamond aliwazawadia magari mapya aina ya Toyota Land Cruiser V8.

Kufika Oktoba 2, 2019, Diamond alitangaza kuwa yeye na Tanasha wamejaliwa kupata mtoto wa kiume na kumpa jina la Naseeb Jr. Huyu alikuwa mtoto wa nne kwa Diamond ingawa amekuwa akisema ana zaidi ya wanne. Akiwa na Diamond, Tanasha alianza kujikita zaidi kwenye muziki, kila wikiendi alikuja Tanzania, akaamua kuandaa Extended Playlist (EP ) yake iitwayo DonnaTella EP.

Uzinduzi wa EP hiyo ulipangwa kufanyika Februari Mosi 2020 katika ukumbi wa Sarit Centre Expo Jijini Nairobi, hata hivyo uzinduzi huo uligeuka fedheha kubwa kwa mashabiki na Tanasha mwenyewe mara baada ya Diamond aliyetarajiwa kuwepo kutangaza hatokuwepo zikiwa zimesalia saa chache kabla hafla hiyo kuanza.

“Kutokana na tatizo la ghafla lilotokea nyumbani, imenibidi niruke Dar es Salaam mara moja kwa ajili ya kulitatua, hivyo naweza fika nimechelewa au kutohudhuria hafla ya uzinduzi maalumu wa EP ya mpenzi wangu Nairobi usiku wa leo” alisema Diamond.

Februari 14, 2020 Tanasha aliachia EP hiyo yenye nyimbo nne ambazo ni La Vie akimshirikisha Mbosso, Gere akishirikiana na Diamond, Ride akimshirikisha Khaligraph Jones tokea Kenya, na Teamo aliyofanya pekee yake.

Licha ya kuwa wapenzi, Diamond na Tanasha walitoa gharama sawa kuhakisha video ya wimbo wao ‘Gere’ iliyotoka Februari 18, 2020 inakamilika kwa kiwango cha juu na kuvutia watazamaji.

Mwishoni mwa mwaka 2020 video ya Gere iliingia katika orodha ya video 10 zilizotazamwa zaidi Afrika kwenye mtandao wa YouTube ikikamata nafasi ya saba.

Video hiyo iliweza kutazamwa zaidi ya mara milioni 22 ikiwa ni video ya tatu kutazamwa zaidi Tanzania kwa mwaka huo.

Kitendo cha Diamond kutohudhuria uzinduzi wa EP ya Tanasha, iliibua tetesi kuwa penzi lao limekalia kuti kavu. Aprili Mosi 2020 Tanasha akiongea True Love Magazine East Afrika alithibitisha kuachana ana Diamond kwa kile alichodai mama yake mzazi, Bi. Sandra alikuwa akiingilia sana mahusiano yao kiasi cha kumkera.

Hata hivyo, upande wa Diamond kupitia watu wake wa karibu wakadai ugomvi wao ni kwamba Tanasha alikuwa akitaka kuongozana na Diamond hadi Marekani ambapo alikuwa na shoo.

Januari 23, 2021 Tanasha alifika nyumbani kwa Diamond kwa kile kinachodaiwa ni kumleta mtoto wake, Naseeb Jr kuja kuonana na baba yake. Wikiendi hiyo wakaenda club na kwa mara ya kwanza walitumbuiza pamoja wimbo wao ‘Gere’ ikiwa ni zaidi ya miezi 11 tangu utoke. Sasa kila mmoja ana maisha yake.