Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 21Article 580069

Maoni of Tuesday, 21 December 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

EAC unganeni kukataa uzushi Corona

EAC unganeni kukataa uzushi Corona EAC unganeni kukataa uzushi Corona

Takribani wiki mbili zilizopita, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alikuwa katika Kongamano la 21 ya Biashara na Uwekezaji lililofanyika Dar es Salaam likikutanisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Majaliwa aliitaka sekta binafsi nchini kuitetea Tanzania kwa kuwa kuna vita kubwa ya kibiashara inayowafanya baadhi ya watu kuitangaza vibaya Tanzania kuwa ni moja ya nchi hatari kutembelea kwa madai kuwa, kuna wimbi la nne la kirusi cha corona aina ya Omicron kitu ambacho si kweli kwa kuwa Tanzania hakuna mgonjwa wa kirusi hicho hata mmoja.

Juzi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi, alisema kwa takwimu zilizopo nchini hadi sasa, Tanzania haijawa na kisa chochote kuhusu kirusi cha Omicron.

Hili ndilo linanifanya niziambie nchi za EAC kuwa, mwenzio akinyolewa, wewe tia maji.

Majaliwa akasema: “Sisi (Tanzania) hatuna mgonjwa hata mmoja wa wimbi la nne (Omicron) hospitalini... Yote hii ni vita ya biashara kwa hiyo sekta binafsi mtusaidie kuyasema haya; tukiacha watu watapotosha na kuharibu sura ya nchi.”

Ikumbukwe kuwa, miongoni mwa nchi ambazo hazikuathiri kwa kiwango kikubwa na madhara ya corona kiuchumi, zimo hizi za EAC ikiwamo Tanzania, hivyo baadhi ya watu hawakufurahia hali hiyo.

Hivi karibuni, vyombo vya habari vya India vilichapisha taarifa iliyoenea katika mitandao ya kijamii ikidai kuwa India, imegundua abiria mmoja anayerudi nyumbani (India) mwenye virusi hivyo akitokea Tanzania.

Kwa mara ya kwanza kirusi hicho kinachobadilika kwa haraka kiligunduliwa nchini Afrika Kusini na kuripotiwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mintarafu suala hilo, Profesa Makubi aliweka bayana akisema: “Bado haijajulikana kama abiria huyu alitokea Tanzania moja kwa moja, au alipitia Tanzania kuelekea India. Haijulikani pia alipita wapi kabla ya kufika India.”

Kwangu mimi, huenda taarifa hizo “zimepandikizwa sumu ya mchezo mchafu ili kujeruhi uchumi wa Tanzania na EAC” kwa jumla ndio maana ninasema, nchi za EAC ziungane kukataa uzushi huu ambao kwangu mimi, unalenga kudhoofisa uchumi wa Tanzania na majirani zake kupitia uwekezaji, utalii na biashara.

Nchi za EAC zijue kuwa, adui anayeizuishia Tanzania leo, kesho ataizushia nchi nyingine yoyote jirani na Tanzania na kesho kutwa, ataizuishia EAC nzima maana hii ni vita ya kiuchumi na kibiashara kama alivyosema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Dawa ya uzushi wowote dhidi ya EAC, ni nchi wanachama kuungana kusema ukweli daima dhidi ya uongo na uzushi.