Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 29Article 560314

Maoni of Wednesday, 29 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: “Angekuwepo Chama...” haina maana kwa sasa Simba

Clatous Chama na Luis Miquissone Clatous Chama na Luis Miquissone

Bahati nzuri uamuzi wa kuwauza mastaa wa Simba, Clatious Chama na Luis Miquissone ulifanyika chini ya utawala wa tajiri, Mohammed Dewji.

Kama ungefanyika chini ya viongozi wa kawaida wa miaka yote wa Simba si ajabu mashabiki wangenyanyua sauti zaidi ya kuwakandamiza viongozi.

Ni baada ya kipigo cha Jumamosi jioni kutoka kwa watani zao Yanga. Kuna wanaoongea sauti za chinichini kuhusu pengo la Chama na Miquissone katika pambano la juzi. Kuna wanaoongea kuhusu ‘ujinga’ wa kuwauza pamoja mastaa hawa wawili.

Faraja kubwa inakuja pale baadhi yao wanapojikumbusha kwamba Simba imewahi kuchapwa zaidi ya mara moja ikiwa na Chama na Miquissone. Pamoja na hilo kuna watu ambao wanaamini Simba imekosea kuwauza Chama na Miquissone kwa pamoja. Hasa wanapojikumbusha kuhusu mechi za kimataifa zinazokuja.

Nataka kuwakumbusha mashabiki wa Simba. Licha ya kichapo kutoka kwa watani, uamuzi wa mabosi wa Simba kuwauza Chama na Miquissone ulikuwa sahihi. Kulikuwa na sababu mbili za msingi za kufanya hivyo.

Kwanza kabisa Simba imelazimishwa na mfumo wa soko. Imelazimishwa pia kutokana na uchumi wa nchi yetu kulinganisha na uchumi wa nchi ambazo wachezaji wamekwenda. Kwetu sisi Tanzania klabu zetu zinapaswa kulisha (feeder clubs) kwenda katika timu kubwa.

Staa wa Misri au Morocco hawezi kuuzwa kwenda Tanzania. Ni ngumu. Hatuna uchumi huo. Lakini staa wa Tanzania au Kenya kuuzwa kwenda Misri na Morocco ni kitu cha kawaida sana kwa mujibu wa soko lilivyo. Jiulize wameuzwa kwa kiasi gani na kama kiasi hicho kinakatalika.

Kitu cha pili ni pale linapokuja suala la mchezaji binafsi. Wakati ofa ikiwa mezani kwa klabu kumbuka na mchezaji anapelekewa ofa yake binafsi. Kwa mfano Al Ahly waliweka mezani kiasi cha Dola 18,000 kama mshahara kwa Miquissone. Endapo Simba wangemkatalia mchezaji huyu kwenda Al Ahly wangepaswa pia kumlipa dau kama hili. Simba wana bajeti hii kwa mchezaji mmoja? Na kama kwa Chama ni hivyohivyo, Simba walikuwa na bajeti kama hii?

Sababu hizi mbili zimeilazimisha Simba. kitu cha msingi kwa sasa ni namna ya kutazama mbele. Hapa kuna mengi ya kufanya. Ikumbukwe kwamba mchezaji anapoacha alama katika timu kuna mambo mengi ya kufanya kuziba alama.

Kitu cha kwanza ni kununua wachezaji wenye ubora.

Tatizo ni nadra kununua wachezaji wenye ubora uleule kulinganisha na wachezaji walioondoka. Wanaweza kuwa chini kidogo kwa umri au ubora. Kitu cha msingi kwa hapa ni muda.

Tatizo kubwa ni kwamba huwa hatujali muda hasa suala hili linapoangukia kwa timu kubwa. Siku zote kutakuwa na presha ya mashabiki kama ambavyo imekuwa katika timu mbalimbali kubwa zenye mashabiki wengi.

Lakini tazama namna ambavyo Chama na Miquissone walitumia muda kuingia na kuwa muhimu zaidi katika kikosi. Kulikuwa na muda mrefu ambao waliutumia kuwasahaulisha mashabiki wa Simba kuhusu mchezaji anayeitwa Emmanuel Okwi ambaye alama yake ilikuwa kubwa kikosini.

Majuzi Okwi alikuwepo Dar es Salaam na akahudhuria pambano la Simba Day dhidi ya TP Mazembe. Mashabiki hawakutaka arudi tena kikosini kwa sababu pengo lake lilishazibika na mashabiki kisaikolojia wamekubali kwamba muda wake umekwisha.

Kama ingekuwa ni Miquissone au Chama nadhani ambacho kingefuata ingekuwa ni mashabiki kupiga kelele za kuwaomba kurudi. Maisha ya soka ndivyo yalivyo na inabidi tukubali tu. inachukua muda kidogo kwa mashabiki kukubali ukweli.

Na sasa inabidi ichukue muda tuwaache kina Sadio Kanoute, Pape Ousmane Sakho na Peter Banda watengeneze ufalme wao na ukubwa wao ndani ya Simba. Wachezaji hupita lakini klabu inabaki palepale ilipo. Haiwezekani watu wakawa wanaomboleza kila siku kwa watu ambao hawapo klabuni.

Kuna mpito huwa unapita labda kiwango cha timu kinakwenda chini kidogo, lakini isisababishe kuishi kwa kumbukumbu za zamani badala ya kuimarisha kilichopo. Kitu kizuri ambacho Simba wamefanya ni kuchukua wachezaji wenye umri mdogo kuliko walioondoka.

Hii ina maana Simba wana nafasi ya kutengeneza timu kali ijayo, lakini pia wachezaji wakitiki katika mfumo wa timu basi wana muda mrefu wa kuitumikia timu huku wakiwa na nguvu zaidi. Mfano mzuri ni kinda kama Banda. Kama mambo yakikubali basi atakuwa na nguvu zaidi kuliko Chama.

Hata hivyo, angalizo ni kwamba kuna nafasi kubwa ya wakubwa kuendelea kuitazama Simba kwa mara nyingine kwa jicho la karibu. Zamani ilikuwa haifikiriki sana kwa timu kama Al Ahly kumchukua mchezaji wa Simba. Tulishazoea kuona wakitamba katika soko la Afrika Kaskazini, lakini kumbe wamegundua kwamba hata Afrika Mashariki linaweza kuwa soko lao.

Tujiandae kwa wakubwa kurudi tena na tena katika kikosi cha Simba au watani zao Yanga. Ilimradi tu wajitokeze wachezaji wa maana kama ilivyotokea kwa Miquissone. Na endapo hili likitokea mashabiki wajiandae kwa hadithi ileile ya Chama na Miquissone.

Mwishoni kwa kuwakumbusha tu mashabiki wapya ni kwamba Okwi ni mfano wa mwisho mwisho wa namna ambavyo mchezaji anaondoka kikosini na maisha yanaendelea. Kwa mashabiki wa kizazi kipya wanaweza kuuliza tu ufalme ambao walikuwa nao wachezaji wa zamani ndani ya kikosi cha Simba.

Walikuwepo kina Hamis Gaga, Mtemi Ramadhani, Nico Njohole, Zamoyoni Mogella, Hussein Marsha, George Masatu, Madaraka Suleiman na wengineo. Usingeweza kudhani kwamba siku moja kina Chama na Simba wangeifikisha Simba robo fainali ya Afrika bila ya hawa kina Mogella.

Majuzi nilikuwa naongea na Madaraka Suleiman ambaye aliniambia jinsi alivyoirithi nafasi kutoka kwa mchezaji kama Edward Chumila. Simba wasingeweza kuamini kwa jinsi ambavyo Chumila alikuwa mkubwa klabuni lakini hatimaye Madaraka aliziba pengo.

Nachelea kuona tusipoelewa mauzo ya Chama na Miquissone huenda tukawapa wakati mgumu viongozi bila ya sababu ya msingi hasa pale ambapo wiki chache baadaye timu inafungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya TP Mazembe na watani Yanga.

Ni rahisi kuvurugana na kuwatisha viongozi. Hata hivyo ukweli ni kwamba wachezaji huja na kuondoka. Kuna ambao wanauzwa, kuna ambao wanaumia na kuna ambao wanastaafu baada ya viwango kwisha. Lazima maisha yaendelee.

Tuwaache kina Sakho waitengeneze Simba yao. Mambo ya “angekuwepo Chama….” au “angekuwepo Miquissone” hayana maana kwa sasa.