Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 25Article 553594

Maoni of Wednesday, 25 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Mhilu, Metacha na Waziri maisha yapo kasi

Aliekuwa Mshambuliaji wa Yanga, Waziri Jr Aliekuwa Mshambuliaji wa Yanga, Waziri Jr

Tuanze na nani? Yusuph Mhilu. Mshambuliaji mahiri sijui niseme wa timu gani, Kagera Sugar au Simba? Mpira wetu ni mgumu sana. Simba imemtambulisha mchezaji mwenye mkataba na timu yake Kagera Sugar kiasi kwamba tunapata picha ngumu kutambulisha Mhilu ni wa timu gani.

Suala lake lina sura mbili kubwa. Sura ya kwanza ni kwamba Mhilu anaingia katika orodha ya mastaa waliowahi kuachwa na timu kubwa kisha wakaenda timu ndogo. Wakafanya makubwa halafu wakarudi katika timu kubwa. Kumbuka aliwahi kucheza Yanga.

Alipoenda Kagera Sugar, Mhilu inaonekana amerudisha makali yake na Simba wameisaka saini yake kwa udi na uvumba. Watu wa Simba wana matumaini makubwa na Mhilu. Iliwahi kutokea hivyo kwa Hassan Dilunga. Alichemsha Yanga akaenda Mtibwa Sugar akafanya makubwa akasajiliwa na Simba.

Iliwahi kutokea hivyo kwa Waziri Junior. Alicheza vyema Toto United ya Mwanza. Akasajiliwa na Azam, akachemsha. Akaenda Mbao FC akarudisha makali yake na Yanga wakainasa saini yake. Yeye hakuweza kufanya kama Dilunga. Alichemsha kwa mara ya pili.

Mhilu anarudi timu kubwa tena kujaribu bahati yake. Matumaini ni makubwa na kila la heri kwake. Ana mtihani mmoja tu kwa Simba na soka letu la ndani. Kurithi makali ya John Bocco ndani ya Simba na ndani ya soka letu. Washambuliaji wanaomfuatia Bocco katika soka letu la ndani ni hawa kina Mhilu, Waziri, Charles Ilamfya, Reliant Lusajo na wengineo. Hata hivyo pengo kati yao na Bocco ni kubwa.

Kitu kingine cha pili katika uhamisho huu wa Mhilu ni namna ambavyo Simba imechemsha vibaya. Kwanini umtangaze mchezaji ambaye haujamalizana na klabu yake? Simba inaonekana kuwa kinara wa mabadiliko katika uendeshaji wa soka nchini ngazi ya klabu inafanyaje kosa la kitoto kama hili?

Zamani tulizowea makosa haya kisha yakaondoka. Hata kina Polisi Tanzania, Coastal Union, Mtibwa na wengineo hawafanyi makosa kama haya. Kwanini Simba wafanye kosa la kitoto kama hili ambalo kama Kagera Sugar wataamua kukomaa basi wanaweza kufungiwa na Fifa na Caf kutosajili wachezaji kwa madirisha kadhaa.

Tuhame kwa Mhilu. Twende kwa nani? Kipa Metacha Mnata. Majuzi nimesoma mahala kwamba amechukuliwa na KMC baada ya Yanga kutangaza kuachana naye. Metacha ajifunze kitu.

Nipo na watu wa Yanga huku Morocco wamenieleza matukio mengi ya utovu wa nidhamu ambayo Metacha amewafanyia klabuni kwao kabla ya kuamua kuachana nao. Sikupenda sana kusikiliza stori za upande mmoja lakini naweza kumhukumu Metacha kwa tukio moja. Lile la kuwaonyesha kidole cha kati mashabiki wa Yanga pale Uwanja wa Mkapa katika pambano ambalo lilikuwa la mwisho kwake kuvaa jezi ya Yanga.

Baada ya lile tukio tu nilijiuliza swali moja. Kwa mfano kama Metacha akiachwa na Yanga atakwenda katika timu gani kubwa nchini? Jibu lilikuwa labda nje ya nchi. Simba wana kipa wao namba moja panga pangua na kwa kweli ndiye kipa anayemuweka benchi Metacha pindi timu ya taifa ikiitwa.

Azam wana kipa wao namba moja panga pangua. Ingekuwa enzi za kina David Kissu wangeweza kumfikiria. Kabla ya upuuzi wake wowote ule Metacha alipaswa kujua kwamba kama hakuwa na mpango wa kwenda nje ya nchi, basi hakukuwa na timu kubwa ambayo angeweza kucheza.

Bahati mbaya kwake ameangukia KMC. Nasema bahati mbaya kwake kwa sababu sidhani kama ni timu ambayo angependelea kucheza baada ya kufaidi uhondo wa kucheza timu kubwa kama Yanga. Maisha yameenda kasi kwake. Kasi ya ajabu.

Baada ya kumaliza matanuzi ya pesa aliyopewa kusaini mkataba na KMC atajikuta ameangukia timu ambayo inakwenda Mbeya, Mwanza, Kagera na kwingineko kwa usafiri wa basi. Atajikuta katika timu ambayo haifikii katika hoteli kubwa. Atajikuta katika timu ambayo hakuna mechi watashinda halafu wakapewa Sh10 milioni kila mchezaji. Wachezaji wa Simba na Yanga huwa wanapewa pesa hizo wakishinda pambano la watani.

Maisha ya Simba na Yanga yanalemaza vijana wetu kiasi kwamba unapoondoka Simba au Yanga unapata wakati mgumu wa kwenda kucheza hizi timu kama Namungo au KMC. Matokeo yake unajikuta ni mchezaji unayeongoza makundi ya migomo.

Kama umeweza kurudi umelewa katika kambi ya timu kubwa kama Yanga na kuporomosha matusi kwa viongozi, utashindwaje kufanya hivyo ukiwa mchezaji wa KMC ambako huduma za wachezaji haziwezi kuridhisha kama Simba na Yanga?

Tuachane na Metacha. Twende kwa Waziri Junior. Mmoja wa wachezaji ambao Yanga walikuwa na matumaini nao makubwa wakati wakiwasajili kutengeneza kikosi kabambe msimu uliopita. Inaonekana maisha yamekuwa magumu tena kwake katika timu kubwa.

Jaribio lake la mwisho kabisa kubaki Yanga lilikuwa katika michuano ya Kagame wiki chache zilizopita Uwanja wa Mkapa. Waziri hakuna kitu cha maana alichoonyesha. Hata bao ambalo alitaka apewe katika pambano la kwanza la Yanga iligundulika kwamba lilikuwa ni la kujifunga kwa wapinzani wao.

Waziri na Yanga wamekubaliana kuachana katika mataa. Waziri ndiye shujaa zaidi kwa sababu ndiye aliyeomba mkataba uhitimishwe. Sijui ana mipango gani, lakini kabla hatujaenda mbali lazima tujiulize nani wa kulaumiwa kati ya Waziri au Yanga.

Kuna nyakati ambazo Waziri alipata dakika za kutosha. Ndani ya dakika hizo hakuna maajabu aliyofanya. Katika mechi moja ya kirafiki pale Chamazi alikosa bao akiwa peke yake na nyavu. Ilikatisha tamaa. Kila alipojaribu bahati yake kwa dakika alizopewa siku zilizofuata bado hakuwa na madhara.

Mpaka ilipofika michuano ya Kagame ilikuwa nafasi nzuri kwa Yanga kujiridhisha upya. Kina Yacouba Sogne hawakuwepo. Bado hakuna alichoweza kufanya na alicheza kwa dakika nyingi. Nadhani pale hata Yanga wenyewe walikata tamaa. Inawezekana kama Waziri angekuwa mfungaji bora michuano ya Kagame labda leo angekuwepo hapa Morocco.

Unawezaje kushindwa kupenya katika Yanga yenye washambuliaji kama Michael Sarpong na Fiston Abdulrazak wakati Bocco anapenya kule Msimbazi akiwa na wakali kama Meddie Kagere na Chris Mugalu? Waziri kabla hajailaumu Yanga inabidi ajilaumu mwenyewe.

Sijui atakwenda wapi au ana mipango gani, lakini anaonekana kujiamini. Hata hivyo maisha yamekwenda kasi sana kwake. Toto, Azam, Mbao halafu Yanga. Ndani ya misimu mitano anasaka timu ya tano. Tusubiri na kuona.