Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 30Article 544825

Maoni of Wednesday, 30 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Mlango sahihi wa Manji kurudi Yanga huu hapa

HISIA ZANGU: Mlango sahihi wa Manji kurudi Yanga huu hapa HISIA ZANGU: Mlango sahihi wa Manji kurudi Yanga huu hapa

YANGA wanampenda Yusuph Manji. Tajiri wao wa zamani. Juzi walimshangilia alipotua ukumbini wakati wakikaribia kufanya mabadiliko ya katiba yao. Wakataka atoe neno. Ni ishara ya shukrani kwa mengi aliyowahi kuwafanyia huko nyuma.

Kumbe Yanga wana shukrani bwana. Kuna watu huwa wanasema hizi timu mbili kubwa za Kariakoo hazina shukrani. Kupitia ujio wa Manji ukumbini juzi tukakumbushana kwamba kumbe bado wana ubinadamu na shukrani.

Labda kwa sababu Manji ni mtu aliyewapeleka juu halafu ghafla akawaacha maskini na hivyo huwa wanakumbuka kipindi chake cha neema mara kwa mara. Huwa inatokea, hasa unapojikumbusha kwamba hakuondoka Yanga kwa ubaya. Alikorofishana na wakubwa zaidi wa nchi hii na sio Yanga.

Ilikuwa faraja kumuona Manji mwenye afya njema akiwa ukumbini kuungana na Yanga wenzake. Kuna watu wanatamani kumuona Manji akirudi Yanga. Swali ni moja tu baada ya mabadiliko yao ya Katiba. Anarudi klabuni kama nani?

Nadhani itabidi arudi kama sehemu ya wawekezaji klabuni katika mfumo mpya wa klabu hiyo. Kuondoka kwake Yanga kumetoa funzo kubwa. Hakuiacha Yanga kama taasisi. Kumbe Yanga ilikuwa inatumia nguvu zake binafsi tu na sio za klabu.

Alipoondoka Yanga ghafla timu ikawa hoi. Ikasajili wachezaji wa ovyo. Kocha mzuri kama, George Lwandamina akarudi zake Zambia. Wakaendelea kusajili wachezaji wa kawaida. Muda wote huo Simba walitumia mwanya huo kutengeneza pengo ambalo mpaka leo lipo.

Alipoondoka mishahara ikakosekana klabuni. Kina Lamine Moro walikimbia klabuni. Kina Ibrahim Ajibu na kocha wao, Mwinyi Zahera wakaibuka kuwa mashujaa wa kuchangisha kila walichonacho kwa ajili ya timu kusafiri, kula na kukaa kambini.

Kila kitu kikaenda ovyo hadi walipotokea hawa jamaa wa GSM. Wakati huu Yanga wakishangilia ujio wa Manji inabidi wawe wanatoa shukrani kubwa kwa GSM ambao wamepambana na wanaendelea kupambana kuirudisha Yanga katika njia. Yanga walikuwa wamepotea.

Simba wapo juu yao kwa sababu GSM walichelewa kuichukua timu na kuiendeleza kuanzia pale Manji alipoondoka. Kama wangefanya mapema si ajabu leo hii wangekuwa wanabanana na Simba katika mafanikio. Timu haijengwi siku moja.

Yanga wana kila haki ya kumshangilia Manji kutokana na pesa alizotumbukiza lakini pia wana bahati mbaya kwamba Manji akitumbukiza hizo pesa kuwanunua akina Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Obrey Chirwa na wengineo, Simba walikuwa hoi kweli kweli. Ghafla waligeuka kuwa maskini licha ya kuwa na lile kundi la Friends of Simba.

Ni katika kipindi hicho Simba hawakuwa na Clatous Chama, Luis Miquissone, John Bocco, Fraga, wale staa yoyote mkubwa. Walikuwa wamejaza makinda wakiamini katika njozi ya kusubiri Simba imara ya baadaye.

Ndani ya misimu mitano Yanga walichukua ubingwa mara nne, huku Azam akichukua mara moja. Na katika mara hizo, Yanga na Azam walishika nafasi mbili za juu kwa misimu mitano huku Simba wakiambulia nafasi ya tatu.

Hii ilikuwa bahati kwa Manji na Yanga ile lakini hawa kina GSM wamekumbana na Simba iliyopitia mabadiliko, ikaingiza pesa nyingi katika kikosi na kutanua pengo lililopo. Haishangazi kuona licha ya kuendelea kupambana hapa na pale lakini pengo lilishakuwa kubwa na wanajitahidi kuliziba.

Kama Manji angekuwepo nyakati hizi inawezekana hali ingekuwa tofauti na nyakati zile lakini hili si la kujadili kwa sasa. Suala la kujadili ni nafasi ya Manji pindi atakapoamua kurudi Yanga. Atarudi katika nafasi gani klabuni katika katiba mpya.

Kwa nilivyoichunguza katiba hii nadhani inaenda kuondoa utegemezi klabuni. Labda baada ya katiba hii huenda mtu mmoja akaamua kuondoka Yanga na bado ikaendelea kuwa imara tofauti na ilivyokuwa wakati Manji akiondoka mara ya mwisho.

Hapa ndipo Yanga wanapaswa kujifunza kitu. Manji, kama ilivyo kwa GSM au Rostam Aziz inabidi waingie Yanga kama wafanyabiashara na sio wafadhili. Waingie Yanga kwa ajili ya kujinufaisha na kuinufaisha Yanga. Ni kama biashara ya jezi inayoendelea kati ya GSM na Yanga. Kila mmoja anapata.

Matajiri waingie katika klabu ya Yanga kwa muundo wa hisa na watengeneze taasisi imara ambayo inaweza kuiacha klabu ikiwa na nguvu hata kama wakiondoka. Hiki kitu kinaendelea mpaka sasa. Unaweza kuona namna gani ambavyo GSM wanagharamika kwa kiasi kikubwa kuiendesha Yanga kuliko pesa wanazopata katika mauzo ya jezi. Huu ni ufadhili ambao tunapaswa kuondokana nao.

Lakini hapo hapo tunasubiri kuona namna gani mafahali wengi wanaweza kuishi kwa pamoja. Katika asilimia 49 zilizobaki za hisa za Yanga baada ya zile 51 za klabu, ni nani atanunua nyingi zaidi na kupata leseni nzuri zaidi ya kuwa na kauli kubwa klabuni.

Nadhani hili linawapa wakati mgumu hata wanachama wenyewe wa Yanga. Kuna wale ambao wanampenda Manji na kuna wale ambao vile vile hawajasahau namna gani GSM walivyowaokoa katika fedheha iliyokuwa inaendelea kuwepo klabuni.

Bila ya GSM hawa kina Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Yacouba, Carlinhos wasingekuja Yanga. Ingawa Simba wameendelea kutawala lakini walau Yanga wameitoa njiani Azam ambayo ingeweza kushika nafasi ya pili kwa kipindi hiki.

Ni vema kumkaribisha Yusuph Manji kwa akili zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Safari hii akaribishwe katika misingi ya kikatiba ambayo itamfanya anufaike na Yanga huku Yanga pia ikinufaika naye. Waliokuwa wanamshangilia wengi akili zao zimelala katika ufadhili.

Wengine walikuwa wanashangilia au wameshangilia ujio wa Manji kwa sababu walikuwa wananufaika naye moja kwa moja katika mifuko yao na wameshindwa kuingia katika mfumo wa GSM. Huu ni ukweli ambao wachache tunaufahamu.

Maisha ya ufadhili yana madhara na tunaona namna gani ambavyo timu hizi zinakuwa hoi pindi wafadhili wakiondoka. Labda mabadiliko ya Katiba yanaweza kuondoa suala la ufadhili klabuni. Ni suala la miaka mingi kabla hata ya kina Abbas Gulamali na Azim Dewji hawajajitumbukiza. Tusishangilie sana wafadhili.

Hata huyu GSM tusimshangilie sana kama akiendelea kuwa mfadhili. Inabidi anunue hisa za klabu pindi milango ikifunguliwa ili iwe rasmi yeye kuwepo alipo. Kwa sasa akiamua kuutumikia mkataba wake wa mauzo ya jezi tu basi Yanga inarudi ilipokuwa.