Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 29Article 581944

Maoni of Wednesday, 29 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Muda ulifika Sure Boy kupanda daladala la kuelekea Jangwani

Usajili mpya Yanga, Salum Abubakar Usajili mpya Yanga, Salum Abubakar "Sure boy"

Lilikuwa suala la muda tu kabla ya Sure Boy mtoto hajatambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga. Moyoni alikuwa ‘ameichezea Yanga’ kwa muda mrefu, katika mwili alikuwa anaichezea Azam. Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ametangazwa kuwa mchezaji wa Yanga Ijumaa jioni akiwa kama zawadi ya Krismasi kwa mashabiki wa Yanga.

Baba yake, Abubakar Salum alikuwa staa mkubwa Yanga. Geuza jina. Mtoto ni Salum Aboubakar, baba ni Abubakar Salum. Baba walimuita jina la utani la ‘Sure boy’ na mtoto naye akarithi jina la utani la ‘Sure Boy’. Kuanzia hapo kila kitu kuhusu maisha ya mtoto kilihusishwa na Yanga.

Yanga wanajua kuwabatiza wachezaji wao kuwa Yanga. Baba mtu alibakia kuwa mnazi mkubwa wa Yanga hata baada ya kumaliza maisha yake ya soka. Haijulikani ni kwa namna gani mwanaye naye alijikuta kuwa mnazi mkubwa wa Yanga. Rafiki wa karibu wa Sure Boy walikuwa wanasema kwamba Sure ni mnazi wa Yanga.

Suala lilikuwa ni namna gani Sure Boy atakuja kuichezea Yanga. Azam walikuwa wamemlea tangu akiwa kinda. Nyakati hizo asingeweza kucheza Yanga. Lakini kumbuka kwamba hata Sure Boy alipoibuka kuwa mkubwa alijikuta akiibukia katika klabu ambayo ilikuwa na uwezo mkubwa wa kipesa.

Linapokuja suala la pesa, Yanga au watani zao Simba hawana ubavu wa ulazima wa kuilazimisha Azam iwape mchezaji. Azam ni matajiri kuliko Simba na Yanga. Simba na Yanga zina mashabiki wengi kuliko Azam. Hapo ndipo ambapo Sure Boy alijikuta amekwama kwa muda mrefu.

Kumbuka kwamba mwishoni mwa msimu uliopita alikuwa ameandika barua ya kuomba kuondoka Azam aende Yanga, lakini ilishindikana kwa sababu Azam walitanua misuli yao ya pesa na akajikuta akilainika kusaini mkataba mpya pale Chamazi. Kama Sure Boy angekuwa anacheza timu nyingi za kawaida angekuwa ameshasaini Yanga.

Hatimaye sasa amesaini kweli. Kwanini? Kuna mambo mawili au matatu. Kwanza kabisa ni ukweli kwamba Azam nao walikuwa wamemchoka Sure Boy. Walikuwa wamemchoka kwa mambo mawili. Kwanza alikuwa miongoni mwa wachezaji wa zamani ambao walioonekana virusi kwa ustawi wa klabu.

Kuna kundi la wachezaji waandamizi wa Azam ambao kwa muda mrefu walishaonekana kama virusi klabuni. Walionekana kama vile wana ufalme mkubwa klabuni na walikuwa wanaharibu wachezaji wageni. Kina John Bocco, Sure Boy, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Mudathir Yahaya, Agrey Morris, Aishi Manula na wengineo.

Kwa Sure Boy ilienda mbali zaidi. Yeye alionekana kuwa mtu wa Yanga zaidi. Uhusiano wa baba yake na Yanga ulirithishwa kwake. Ni kweli kwamba yeye mwenyewe ni shabiki wa Yanga. Amekulia katika Uyanga. Lakini zaidi ni kwamba mara zote watu wa Yanga walikuwa wakijinasibu kwamba Sure Boy ni mtoto wao.

Kichekesho kilikuja pia alipocheza dhidi ya Yanga. Katika mechi hizi alihitajika kuwa malaika. Hakupaswa kukosea. Kila ambapo angekosea ingeonekana kama vile alikuwa anacheza kinazi. Siku moja Sure Boy aliwahi kuhojiwa na mwandishi akaulizwa “Mbona haujawahi kuifunga Yanga?” Yeye alitoa jibu lenye akili ambalo pia liliendana na swali. Alijibu, “kwani lini nimewahi kuwafunga Simba?”

Mbele ya safari Sure Boy aliwahi kuwafunga Yanga, lakini isingemtoa katika ukweli huu kwamba yeye alionekana amekaa Kiyangayanga. Hatimaye ametua Yanga kweli. Ni baada ya kukosa uhamisho aliouhitaji katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Uhamisho huu unatimiza ndoto zake. Kuna mambo mengi nyuma ya uhamisho huu. Kwanza Sure Boy anafuata nyayo za washkaji zake kina Bocco kucheza katika timu kubwa zaidi nchini. Sasa hivi Sure atafufuka upya kama ambavyo kina Bocco walifufuka upya baada ya kuhamia timu hizi. Ukihamia timu hizi unapendwa kwelikweli.

Ni kweli unacheza katika shinikizo kubwa kwa sababu ni timu zenye idadi kubwa ya mashabiki - tena walio wanazi, lakini unajisikia kuwa mchezaji mkubwa na unazungumzwa zaidi kuliko wakati upo Azam. Unachunguzwa zaidi na zaidi na unaonekana umezaliwa upya.

Ni kama ambavyo nyakati fulani nilikuwa nikiamini kwamba Erasto Nyoni alikuwa ni mchezaji mwenye akili kubwa zaidi uwanjani hapa Tanzania. Mashabiki hawakujua hilo mpaka alipohamia Simba. Kumbe siku zote walikuwa hawamfuatilii kwa umakini. Mpira wetu ndivyo ulivyo. Hatuwajui vizuri wachezaji wa timu nyingine mpaka watue timu kubwa.

Hiki ndicho ambacho Sure Boy ataanza kukifaidi kwa sasa. Wakati mwingine ataanza kufaidi kupewa pesa zisizo na sababu pia akitembea mtaani kama akiwafurahisha mashabiki wa timu yake. Hii ndio tofauti kati ya Simba na Yanga dhidi ya Azam.

Hata hivyo kuna kelele nyingi za kutukanwa kama mambo hayaendi sawa. Kuna kelele alikuwa hapigiwi wakati yupo Azam lakini atapigiwa sana akiwa Yanga pindi akionekana mzembe. Amuulize rafiki yake, Aishi. Baada ya kufungwa lile bao na Mapinduzi Balama dunia ikamuangukia. Mashabiki wa Simba wakalalamika kwamba Aishi alikuwa ana udhaifu mkubwa wa kufungwa mabao ya mbali. Hawakuliona hilo akiwa Azam?.

Ndani ya uwanja Sure ataiimarisha Yanga. Tatizo letu kubwa mashabiki ni kupenda kupanga kikosi cha kwanza tu. Watu wanajiuliza kama Sure Boy atakuwa anaanza au hapana. Hilo sio la msingi. Kitu cha msingi ni kwamba Sure atawapa watu wa Yanga machaguo mazuri eneo la kiungo ambalo mpaka sasa lina utajiri.

Kuna wakati Simba walifanya hivyo. Ilionekana kama vile kiungo chao kilikuwa bora. Kulikuwa na Clatous Chotta Chama, Jonas Mkude, Thadeo Lwanga na wengineo. Wao ndio kwanza wakaenda Zambia kumchukua Rally Bwalya kuongeza makali. Kuna mechi ambayo tayari Simba wametawala na wanaongoza lakini anatoka Chama anaingia Bwalya. Hakuna unafuu.

Kuna wakati Yanga huenda ikamkosa Khalid Aucho, Sure akaanza. Kuna wakati huenda ikamkosa Yannick Bangala lakini Sure akaanza. Kuna wakati atakosekana Fei Toto lakini Sure ataanza. Kuna siku ambayo Sure ataanza na Bangala ataingia kipindi cha pili. Hivi ndivyo Simba walitengeneza kikosi chao kikali.

Kitu ambacho Sure atapeleka Yanga ni utajiri zaidi katika eneo hilo. Atapeleka ubora ambao hautatofautiana kati ya wachezaji wanaoanza na wale walio nje. Tanzania tunapenda ‘first eleven’ imara bila ya kujali sana ubora wa wachezaji waliokaa katika benchi. Katika eneo la kiungo Yanga watakuwa wamelitibu tatizo hili.

Vipi kuhusu Azam? Nadhani kwao wamechukua uamuzi sahihi. Kwanini ung’ang’anie kukaa na mchezaji ambaye hana mapenzi wala moyo? Ndani ya miezi 12 mchezaji akiandika barua mbili za kuomba kuuzwa basi ujue ana jambo lake moyoni. Ni vyema kumruhusu aendelee na maisha yake.

Azam wamekuwa waungwana zaidi kwa sababu wamemruhusu aondoke bure. Ni kitu ambacho klabu za Ulaya zinafanya kama shukrani kwa mchezaji aliyekaa klabuni miaka mingi. Inampa nafasi ya kujadili vyema pesa nzuri ya mshahara anakokwenda. Wapongezwe Azam kwa kutomkomoa mchezaji hata fursa hii ilipojitokeza.