Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 26Article 539911

xxxxxxxxxxx of Wednesday, 26 May 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Ni muda wa kuteta na Barbara Gonzalez na Mo

SIMBA imetolewa. Ilishinda vita pale Temeke, lakini walishatolewa mapema kule Soweto Johannesburg baada ya kuruhusu kichapo cha mabao manne ugenini. Wameishia hatua ya robo fainali. Walitamani kufika nusu fainali na kuifikia rekodi yao ya mwaka 1974.

Na sasa kuna maswali muhimu kwa mmiliki wa timu, Mohammed Dewji pamoja na Mtendaji Mkuu wa klabu, mrembo Barbara Gonzalez. Maswali ambayo yatalenga kupima nguvu ya Simba katika kushikilia palepale ambapo wapo kwa sasa. Kuwa juu ni jambo rahisi, kuendelea kuwa juu ni jambo gumu kidogo. Kuingia katika kundi la Al Ahly, Raja, TP Mazembe, Zamalek, Mamelodi na wakubwa wengine sio kazi rahisi rahisi. Mpaka sasa Simba haijaingia katika kundi hilo kwa sababu mbalimbali.

Hawa wakubwa kila siku wanarudi tena nafasi za juu. Kama sio robo, basi nusu fainali au fainali. Miaka miwili iliyopita Simba walipofika robo fainali ya michuano hii msimu uliofuata wakatolewa na UD Songo katika hatua za chini.

Msimu huu wameishia robo na hatuna uhakika msimu ujao wataishia wapi. Wakati wa kupima ukubwa wa Simba ni huu ambao unawakabili kwa sasa kwa sababu utabiri wa hali ya hewa unaonyesha ishara nyingi.

Ishara ya kwanza ni kwamba Simba imecheza vizuri zaidi msimu huu. Kila wiki wachezaji wao wamekuwa wakiingia katika kikosi cha wiki cha michuano ya Ligi ya Mabingwa. Leo atakuwepo Aishi, kesho Luis Miquissone, keshokutwa Clatous Chama na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, siku nyingine Larry Bwalwa.

Ukubwa wa Simba utaanza kupimika pale itakapofanikiwa kwanza kuwabakisha mastaa wakubwa ambao watatakiwa kwingineko. Kuna wakubwa kutoka Afrika Magharibi au hata majirani zetu Wacongo kina TP Mazembe watataka kugawana wachezaji wa Simba.

Ni kweli mpira ni biashara, lakini wakati mwingine inategemea na malengo ya timu. Malengo ya Simba ni kufanya biashara au kuchukua ubingwa wenyewe. Tutaanza kuona nguvu ya Mo katika kuhimili mawimbi pindi wakubwa wakitaka kugawana wachezaji wao.

Kwa mfano, Raja wamtake Kapombe kwa Dola 500,000. Vipi kama Waydad wamefurahishwa sana na Simon Msuva na sasa wanamgeukia Tshabalala. Vipi kama Zamalek wakimtaka Chama. Vipi kuhusu Miquissone.

Kitakuwa kipimo kwa Mo kwa sababu sidhani kama watapokea ofa za kitoto endapo wakubwa wakiamua kufanya kweli. Timu imejiweka katika jicho zuri dhidi ya wakubwa. Haitakuwa bahati mbaya kama ofa zikianza kukaa katika meza ya Simba. Watakubali kuichanachana timu yao au wataamua kuchukua pesa? Shauri zao.

Wakubwa wa kule Kaskazini ni ngumu sana kung’oa wachezaji wao. Hata TP Mazembe naamini tajiri wao alikuwa anakataa pesa nyingi kutoka kwa Waarabu ambao walikuwa wanawataka kina Mbwana Samatta, Jean Kasusura, Kidiaba, Reinford Kalaba na wengineo.

Haikushangaza kuona karibu kila msimu Mazembe wanarudi katika ubora uleule kwa sababu waliendelea kubakisha wachezaji wao bora. Sio kwamba mastaa wao walikuwa hawatakiwi, hapana, noti za Moise Katumbi zilikuwa zinawazuia.

Mpira ni biashara. Wachezaji waondoke au wasiondoke lakini je Mo yupo tayari kutia tena pesa nzuri kwa wachezaji wapya kwa ajili ya kukichangamsha kikosi? Simba inahitaji wachezaji wa uhakika kwa ajili ya kuendelea kuwepo.

Hata kama kina Chama watabaki na hawatatakiwa na wakubwa wengineo lakini timu zote kubwa Ulaya na kwingineko huwa wanaleta nyota wengine kwa ajili ya kuchangamsha kikosi. Kuchangamsha kikosi inamaanisha kuhakikisha wachezaji waliopo hawabweteki.

Walifanya vizuri msimu uliopita kwa kuwatia kikosini Bernard Morrison na Bwalya kwa ajili ya kuchangamsha na kuongeza ushindani katika eneo la kiungo. Pale mbele kulikuwa na John Bocco na Meddie Kagera lakini bado wakamleta Chris Mugalu. Hivi ndivyo inavyotakiwa.

Hata hivyo ni wakati wa kuweka pesa kwa wachezaji wa maana ambao wanahitajika kikosini. Sio wakati wa kubahatisha tena. Bahati nzuri kwa Simba ni kwamba mambo yalikwenda vizuri kwa Morrison na Bwalya lakini wakati mwingine Simba isitegemee sana kupata ubora kutoka kwa wachezaji wa bure bure. Lazima itie pesa.

Nategemea kuona kwa sasa Simba inapambana kuwapata mastaa wa kuanzia Dola 100,000 na kuendelea kutoka katika timu hizi hizi ambazo wamekuwa wakipambana nazo katika michuano hii. Habari ya kuchukua wachezaji wa bei nafuu iachwe. Inatokea mara chache kulamba zali la kuchukua wachezaji wa bei chee halafu wakawa mastaa.

Kitu kingine ni kwamba Simba bado haina uhakika wa kumalizia pale ilipoishia. Wakati mwingine ni bora kumalizia ndoto. Ingekuwa bora Simba kufika nusu kisha fainali, ikiwezekana kuchukua ubingwa wenyewe moja kwa moja.

Wakati mwingine unaweza kuwa na msimu mzuri kama ambao Simba walikuwa nao, lakini ghafla kila kitu kinabadilika kama mkishindwa kumalizia ndoto. Wakati mwingine unakuta wachezaji wamechoka na hawapo katika hali ya ushindan tena.

Mfano mzuri ni hawa Liverpool. Baada ya kutwaa ubingwa kwa kutumia nguvu nyingi msimu uliofuata wamerudi wakiwa nyanya pale England. Juzi walikuwa wakishangilia kuingia Top Four. Ulitazamia Liverpool washangilie kuingia Top Four?

Hiki kitu Waingereza wanaita Second Season Syndrome. Uchovu wa msimu wa pili. Hata ndugu zangu Leicester City iliwatokea. Bayern Munich mabingwa wetu wa Ulaya wa mwaka jana msimu huu walishindwa kufika walau nusu fainali.

Simba wajihadhari na hali hii kwa kuandaa mastaa wakubwa ambao wataingia kikosini kuendelea pale ambapo kina Chama wanaweza kuishia. Mazembe wakiwa moto kweli kweli walikuja nchini wakambeba Samatta kuongeza nguvu.

Kwa namna hii Simba wataendelea kubaki katika klabu kubwa za Afrika wasilegee. Inahitaji nguvu kubwa ya pesa na maarifa kuingia katika kundi la wakubwa. Hawa kina Al Ahly wamekuwa wakifanya kila kukicha. Haikushangaza walichukua ubingwa halafu wakatia mamilioni ya pesa kuchukua beki kutoka Morocco na kocha kutoka Afrika Kusini.

Join our Newsletter