Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 27Article 566044

Maoni of Wednesday, 27 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Simba ‘walivyojitoa’ wenyewe Ligi ya Mabingwa Afrika

Pambano la Simba dhidi ya Jwaneng Galaxy Pambano la Simba dhidi ya Jwaneng Galaxy

Aliandika Crescentius Magori, mtu mzito katika Simba akitumia ukurasa wa Twitter. Aliandika baada ya mechi ya juzi kati ya Simba na Jwaneng Galaxy ya Botswana. ‘Hii ni siku mbaya katika historia ya Simba. Usaliti ni kitu kibaya sana, hakivumiliki.’

Inawezekana Magori anafahamu ambayo hatuyafahamu. Simba imeondolewa kizembe katika michuano ya Ligi ya mabingwa barani Afrika. Waliwahi kutolewa kizembe na Wamakonde wa Msumbiji walioitwa UD Songo na safari hii wametolewa kizembe na Watswana.

Nini kimetokea? Kama ni usaliti wa baadhi ya wachezaji sisi wengine hatufahamu. Kama ni usaliti wa baadhi ya viongozi, wengine hatufahamu. Tunachofahamu ni kwamba Simba waliliridhika baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 pale Gaborone wiki moja iliyopita.

Magori anazungumzia usaliti upi? Tuanze na maandalizi yenyewe ya kisaikolojia kuelekea katika pambano hili. Kila kitu kilikuwa kimya. Simba wenyewe hawakuonekana kuwa na morali na mechi hii. Hakukuwa na gumzo lolote kuelekea katika mechi hii. Ilikuwa kama vile kila moyo wa Mwanasimba unasema “Tutapita tu”.

Hakukuwa na tahadhari yoyote ya kwamba mechi inaweza kuwa ngumu. Hata mpira ulipoanza hakukuwa na kelele zozote kwa sababu Simba walijua wangepita tu. Walipoteza nafasi nyingi za wazi. Ungeweza kumsifu kipa wa Jwenang lakini ukweli upo hivi, wachezaji wanapohisi nafasi zinaweza kuwaangukia zaidi huwa hawawi makini kuchukua nafasi zao.

Simba wamewahi kucheza mechi kali hapa dhidi ya Nkana Red Devils, AS Vita, Al Ahly, JS Soura na wengineo. Walipata nafasi chache katika mechi hizi na wakawa makini mara mbili zaidi kwa sababu wachezaji hawakujua kama zitarudi tena.

Juzi walikuwa na mechi yenye nafasi nyingi mkononi na wakawahisi zitaendelea kufurika tu. Bernard Morrison alikuwa anaupanda mpira mashabiki wanashangilia. Mambo haya waliyafanya Yanga katika mechi fulani dhidi ya Mtani Jembe dhidi ya Simba. Walikuwa wanaongoza mabao matatu hadi mapumziko na kina Mrisho Ngassa wakawa wanainama na kuubusu mpira huku pambano likiendelea. Mwishowe pambano lilimalizika 3-3.

Kuna uzembe wa kisaikolojia katika mambo mawili. Kwanza ni upotevu wa nafasi. Pili ni namna ya kuzuia. Baada ya Simba kupata bao la kuongoza kupitia kwa Larry ‘Soft touch’ Bwalya wachezaji walizidi kulegeza nati. Sijui hata walikwenda kuzungumza nini wakati wa mapumziko. Waliporudi hawakuwa na ukabaji mzuri. Nadhani waliambiwa kwamba baada ya kuongoza kwa mabao matatu - mawili Gaborone na moja Temeke, basi mechi ilikuwa imemalizika.

Hata bao la kwanza halikuwashtua sana. Hakukuwa na ukabaji mzuri katika maeneo ya pembeni hadi katikati. Na baadaye likaja bao la pili. Sijui na hiki ni moja kati ya kitu ambacho Magori ameita usaliti. Inakuwaje Simba wameruhusu mpira wa kurusha utue katika eneo la sita hatua moja kutoka Aishi Manula na kusiwe na mtu hata mmoja aliyeucheza mpira?

Mfungaji Wender alikuwa peke yake kati ya mabeki wawili wa kati wa Simba, Serge Wawa na Enock Inonga. Anaanza kulaumiwa zaidi Wawa. Kwanini aache kuurudia mpira ambao angeweza kuufikia. Kwanini aache kuurukia wakati hajui kuna nani?

Aishi naye alikuwa ametulia langoni. Kwanini ashindwe kutabiri uzembe wa Wawa na kuutokea mpira huo walau autie ngumi. Mpira wa kurushwa au kona unapotua katika eneo la sita ni uzembe wa wachezaji wa pande zote mbili. Wanaoshambulia na wale wanaoshambuliwa. Lazima kuwepo na kujibu mapigo (reaction) kabla ya mpira haujagusa chini.

Uzembe kama huu waliufanya walinzi wa Watswana katika pambano la kwanza pale Gaborone. Mabao yote mawili yalitokana na uzembe wa kushindwa kuosha mipira ya kona mpaka mpira unatua chini. Simba wakamalizia.

Bao la tatu pia kulikuwa na uzembe mwingi katika maandalizi ya bao lenyewe hadi mpira ulipomfikia mfungaji. Lakini kwanza twende kwa Aishi mwenyewe. Alipotoka kuifuata krosi kwanini aliishia njiani? Inasemwa kwamba kipa anapotoka lazima walau auguse mpira aupoteze mwelekeo kama ulikuwa unakwenda katika kichwa cha adui. Aishi alikwenda akaishia njiani.

Hapohapo mfungaji wa bao hili alikuwa hajakabwa na mtu ambaye alipaswa kumfuatia kutoka nyuma. Angeweza kuwa winga mmoja wa Simba au kiungo kwa sababu Mohamed Hussein Tshabalala alikuwa ameingia ndani kama fomesheni inavyosema pindi mpira ukitokea katika upande wa Shomari Kapombe.

Nadhani ukabaji huu wa mabao mawili ya mwisho ndio uliomtumbukia nyongo Magori kiasi cha kuandika kwamba kuna usaliti. Hakuamini kwamba yalikuwa matokeo ya kawaida tu. Kwangu mimi siamini sana katika hilo kwa sababu mbalimbali. Kwanza ni kwamba hata Simba yenyewe ilifunga mabao ya aina hiyo Gaborone. Huwa inatokea katika soka. Lakini hapohapo tujikumbushe kwamba Simba imefungwa sana mabao ya namna hii katika miaka hii. Mabao ya krosi au mipira iliyotengwa.

Katika safu ya ulinzi ya juzi aliyebadilika alikuwa Enonga tu lakini Shomari, Wawa, Aishi na Tshabalala wote walikuwepo wakati Simba ikifungwa mabao ya namna hii na kina Vita wakati ule wakifungwa tano tano ugenini.

Hata katika Ligi Kuu Simba imefungwa mabao haya na kina Charles Manyama. Inawezekana kuna usaliti upo ambao hatuufahamu lakini ambao tunawafahamu Simba ukweli ni kwamba wamekuwa na tatizo hilo kwa muda mrefu zaidi.

Na baada ya matokeo haya kuna mambo ya kutazama. Kwanza tujifunze kuuheshimu mpira na miiko yake. Simba walilegeza nati kuelekea katika pambano la marudiano. Walidhani kwamba shughuli ilikuwa imemalizika Gaborone.

Kuanzia viongozi, mashabiki, benchi la ufundi na mashabiki hawakuonekana kulijali sana pambano hili. Hata mashabiki walijitokeza wachache wakiamini kwamba timu yao ilikuwa imemaliza kazi Gabiorone na hakukuwa na haja ya kusimama sana nyuma ya wachezaji.

Hapohapo sio mbaya tukikumbushana kwamba Simba wametia aibu na bado wana kazi kubwa kufika kule ambako wakubwa wengine wa Afrika wamefika. TP Mazembe wanaonekana kuwa timu dhaifu katika miaka hii mitatu na kila mara wamekuwa wakitolewa mapema. Lakini wanapokuwa katika ubora wao wamekuwa wakifika nusu fainali au fainali mara nyingi mfululizo.

Simba hawaeleweki. Hawastahili kuingizwa kwa wakubwa kwa sababu wanakosa mwendelezo wa ubora. Walipaswa kuigeuza hatua ya makundi kuwa kijiwe.