Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 03Article 567778

Maoni of Wednesday, 3 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Simba washushe pumzi, wafuate nyayo za Chama

Clatous Chotta Chama Clatous Chotta Chama

Baada ya Yanga kucheza mpira mkubwa, au mwingi Jumamosi dhidi ya Azam, wachezaji wa Simba juzi wakaingia uwanjani pumzi zikiwa juu. Pumzi za hasira. Pumzi za kutukumbusha Simba ni nani. Walikuwa wanacheza dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Nini kilitokea? Pambano lilimalizika kwa suluhu bila ya kufungana. Kulikuwa na kadi nyekundu nyingi kuliko mabao. Kadi nyekundu mbili huku kukiwa hakuna bao lolote. Kwanini? Ndiyo Coastal Union ni wazuri lakini sio kwa Simba ya Clatious Chama na Luis Miquissone.

Inachukiza kuwakumbuka kila mara wachezaji hawa waliouzwa, lakini ndio ukweli. Walikuja kina Al Ahly hapa na Pisto Mosimane, lakini bado maisha yalikuwa magumu kwao. Ukuta wao ulifunguka vizuri tu na wakafungwa. Wakaja kina AS Vita na wengineo hali ilikuwa hivyohivyo.

Leo Simba wanashindwa kuwafungua Coastal Union. Niliwatazama juzi wakiwa na papara kubwa. Kibu Dennis alikuwa anakimbia ovyo, John Bocco alikuwa hafungui njia, Bernard Morrison alikuwa anataka kufanya anachojisikia.

Karibu kabisa na lango Simba hawakuwa na ushirikiano wowote. Sio kawaida. Walicheza dakika zote bila ya kushusha pumzi. Walicheza kwa jazba. Walicheza bila ya kutazama. Waliufanya mpira uwe mchezo mgumu tofauti na walivyokuwa wanafanya kipindi cha miaka minne iliyopita.

Inawezekana ni kwa sababu ya kiwango cha Yanga Jumamosi. Kwamba walipania kuonyesha ukubwa na utawala wao wa soka. Kwamba kwa sasa kila wanapocheza wanajikuta na madeni makubwa kwa mashabiki tangu watolewe kizembe na Jwaneng ya Botswana. Simba hawatengenezi nafasi nyingi za wazi (clear chances). Wanatengeneza nafasi nyingi ngumu ambazo sio za wazi (half chances). Kwanini? Hawatazamani. Wanapoteza utulivu ambao ulikuwa unaletwa na Chama wakati akiwa katika jezi namba 17 ya Simba. Miqissone pia anakosekana.

Bahati mbaya kwa Simba, Rally ‘Soft touch’ Bwalya sio Chama. Hawezi kuicheza namba 10 kama ambavyo Chama alikuwa anacheza.

Larry anakaa chini sana akiungana na viungo wengine wawili wa Simba wanaocheza chini yake. iwe Sadio Kanoute au Mzamiru Yassin.

Siamini kama Rally atatengeneza nafasi nyingi kwa wenzake kama ilivyo kwa Chama, au kama atafunga mabao mengi kama ilivyokuwa kwa Chama. Sijui kama anajua kuwa Simba inahitaji utulivu wake kuliko wakati mwingine wowote ule.

Katika pambano dhidi ya Polisi Tanzania, akiwa amezungukwa na rundo la mabeki wa mabeki wa Polisi mara mbili alijaribu kutaka kupiga mashuti langoni huku wenzake wakiwa wamefungua. Baadaye mpira ukaporwa Polisi wakaondoka zao.

Juzi tu Chama alikuwa ametupia video katika mtandao wake wa Instagram akituonyesha kile ambacho Simba wanakikosa kwa sasa. Huko anakocheza kwa Wamorocco alipata shambulizi la kushtukiza wakiwa wamebaki na mlinzi mmoja na mwishowe akapiga pasi rahisi kwa mwenzake.

Rally lazima asongee mbele na kujua kwamba Simba inamhitaji kwanza katika ubunifu, halafu pili katika kujaribu kufunga.

Hiki ndicho ambacho Chama alikuwa anawazawadia kwa misimu mitatu ambayo alikaa pale mtaani Msimbazi.

Simba wasicheze kwa presha. Itakuwa aibu kama wachezaji wawili tu wataleta mvurugano katika kikosi. Mchezaji kama Morisson alipaswa kuwa Miquissone mpya lakini na yeye anatawaliwa na ubinafsi na anataka kuvaa viatu vya haraka. Hatazami wenzake na anajaribu zaidi kujitafutia nafasi mwenyewe kuliko kutafutia nafasi wengine.

Enock Inonga. Bonge la beki, lakini aliishia kufanya ujinga uleule ambao rafiki yake Tonombe Mukoko aliufanya pale Kigoma. Alimpiga mtu mbele ya mwamuzi msaidizi kwa kisingizio cha kuwahi kuupiga mpira wa kuotea.

Hii ina maana kwamba Inonga anakwenda kuidhohofisha Simba kwa mechi tatu zijazo. Simba ilihitaji kasi, stamina na nguvu yake mchezoni. Ndiye beki wa Simba ambaye yupo katika fomu zaidi. Sijui kwanini alifanya alichofanya.

Kifupi Simba bado wana ubora mwingi kuliko maadui zao. Katika hizi mechi nne walizocheza dhidi ya Biashara, Dodoma City, Polisi na Coastal Union bado wanaonyesha utawala mzuri wa mechi, lakini ubunifu umerudi nyuma kwa kiasi kikubwa.

Kinachoshangaza kingine ni kwamba achilia mbali Inonga, wachezaji wengine wapya hawajawapa nguvu inayostahili. Wapi Peter Banda? Yanga ametoka Tuisila Kisinda ambaye alikuwa anawasaidia ameingia Jesus Moloko ambaye anawasaidia na mabao mawili mpaka sasa.