Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 17Article 572080

Maoni of Wednesday, 17 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Tumheshimu Bocco, mchezaji nyota hazimiki ghafla

John Bocco John Bocco

Miongoni mwa Watanzania wanaopitia wakati mgumu katika kazi zao kwa sasa yupo, John Bocco. Nilikwenda katika pambano kati ya Simba na Namungo na mashabiki walionekana wazi kutoridhishwa na kiwango chake. “Mtoe Bocco”. Ilikuwa kawaida kusikia hivyo.

Bocco alikuwa kila akiharibu anazomewa. Mbaya zaidi kocha wake mkuu, Thierry Hitimana akamtoa. Ilinishangaza kidogo. Namungo walikuwa wamepungua na muda wote Simba walikuwa wanashambulia. Kwanini umtoe mshambuliaji halafu umuingize mshambuliaji? Kwanini kusiwe na washambuliaji wawili uwanjani?

Hapo kocha alikuwa anaendeleza maumivu ya moyo ya Bocco. Haishangazi kuona pia kwamba Simba waliongeza kasi ya kusaka kocha mpya kwa haraka. Sidhani kama walikuwa wanajua wanachokifanya hasa baada ya kuondoka kwa Didier Gomes.

Baada ya hapo Bocco ameichezea Taifa Stars mechi mbili. Dhidi Congo nyumbani na dhidi ya Madagascar ugenini. Hajacheza vizuri. Hayupo fomu. Hata hivyo, hizi ni nyakati za kusimama nyuma ya mchezaji. Badala yake kinachotokea dhidi ya Bocco ni maneno mengi ya kumkashifu na kumkejeli zaidi.

Kuna wanaosema “Bocco umri umekwenda apumzishwe”. Unajiuliza, mchezaji anakuwaje mzee ghafla ghafla? Juzi tu alikuwa anatangazwa kuwa mchezaji bora wa ligi yetu. Imekuwaje amekuwa mzee ghafla? Mchezaji ambaye amecheza kwa muda mrefu haruhusiwi kupitia fomu mbovu? Akipitia fomu mbovu anaambiwa amezeeka.

Mchezaji ambaye alikuwa bora kufikia Mei mwaka huu anawezaje kuzeeka ghafla ifikapo Novemba? Hakujawahi kuwa na hesabu za umri za namna hii. Ni kama vile Tyson Fury alipigwe katika pambano lake lijalo halafu useme amepigwa kwa sababu ya uzee. Sawa umri wake unaweza kuwa umesogea lakini hawezi kuzeeka ghafla.

Kuna wanaosema “Bocco amechoka apumzike kwanza”. Amechoka wakati ndio kwanza msimu mpya umeanza. Msimu umeanza Septemba mwaka huu na ghafla tunaambiana kwamba kuna wachezaji wamechoka. Hapana. Haiji kwa haraka hivyo. Labda kama ingekuwa tumefika Aprili.

Kinachotokea ni upotevu wa fomu wa kawaida tu. Mchezaji ambaye anakuwa mzee ni yule ambaye kiwango chake kinapungua taratibu. Hakiwezi kupungua ghafla ndani ya msimu mpya. Kama kwa mshambuliaji basi kama alikuwa anafunga mabao 20 kwa msimu anajikuta akifunga mabao tisa au kumi kwa msimu. Msimu mwingine tena anajikuta katika mazingira hayo hayo. Kadri siku zinavyokwenda mabao yanapungua.

Kwa misimu zaidi ya kumi sasa Bocco hakosi mabao 15 au zaidi. Ndiye mshambuliaji hatari zaidi anayecheza ndani kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita. Ndiye mshambuliaji ambaye anatuwakilisha zaidi katika kupambana na washambuliaji wa kigeni wanaotamba nchini.

Chini ya Bocco kuna washambuliaji wazuri wa kizawa lakini wameshindwa kufikia ubora wake. Wapo wengi na wamejaribiwa na timu kubwa lakini mambo yamekataa. Wapo kina Charles Ilamfya, Yusuph Mhilu, Waziri Junior, Adam Salamba na wengineo wengi. Bocco amebakia kuwa kinara wao.

Kinachochekesha zaidi ni kwamba hata sasa ukiwaambia mashabiki wa Simba wanaomzomea Bocco kwamba amezeeka au amechoka basi aende Yanga, hakuna atakayekubali. Na hata wale wa Yanga ukiwaambia waletewe Bocco wote watashangilia. Huu ndio unafiki wa mashabiki wa Kitanzania.

Bocco anastahili heshima hata kama fomu yake ipo mbovu. Nadhani ni mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu. Amefunga mabao zaidi ya 100. Hata kama hayupo vizuri kwa sasa lakini tunahitaji kusimama nyuma na sio ‘kumuua’ zaidi.

Wenzetu huwa wanasimama nyuma ya mastaa wao ambao wanastahili heshima. Leo sio Bocco tu, hata Mbwana Samatta anatukanwa. Kisa? Kwa sababu Simon Msuva yupo katika fomu nzuri zaidi kwa sasa. Wanasahau mengi ambayo Samatta ameyafanya kuleta heshima ya nchi. Hata Msuva mwenyewe alitamani zaidi kucheza nje kwa sababu ya kutaka kufikia mafanikio ya Samatta.

Kitu kingine unachojiuliza kuhusu Bocco ni kama kuna washambuliaji wengine wa ndani ambao wanaweza kuziba nafasi yake ndani na nje ya Simba. Nani hasa? Kama Samatta hayupo kama ilivyokuwa juzi pale Madagascar unaweza kumuamini mshambuliaji gani mwingine wa kizawa wa kukufanyia kazi yako?

Wenzetu huwa wanamuondoa mtu sio tu kwa sababu ya fomu yake mbaya bali pia kwa kuibuka kwa wachezaji wengine mahiri katika nafasi zao. Kama Bocco akifunga mabao 17 ya Ligi basi awepo mshambuliaji mwingine wa kizawa ambaye atafunga mabao walau 16. Bahati mbaya hatukuti washambuliaji hao.

Tumpe heshima yake Bocco. Hata wacheze wakubwa na mahiri duniani huwa wanapoteza fomu. Kina Lionel Messi pia wanapitia vipindi vibovu. Kuna washambuliaji mahiri kama kina Ronaldo De Lima ambao wamewahi kucheza mechi saba bila ya kufunga. Ni kitu cha kawaida katika mpira wa miguu.

Waingereza mpaka leo wanaulizana kinachomtokea Harry Kane. Msimu huu amerudi akiwa na fomu mbaya. Hakuna anayesema Kane amechoka wala hakuna anayesema Kane amezeeka. Na wanaweka akiba ya maneno wakiamini kwamba Kane atarudi katika fomu.

Ni kama ambacho kitatokea kwa Bocco. Muda si mrefu naamini atarudi katika fomu yake na tutaanza kusikia lugha tofauti. Hakuna ambaye atakumbuka uzee wake na wala ambaye hakuna atakayesema ni mzee. Mara ngapi tunasahau uzee wa Kagere akiwa anatupia mabao katika nyavu?