Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 07 07Article 545869

Maoni of Wednesday, 7 July 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Ustaa wa Mzee Mpili na tamaduni za soka duniani

HISIA ZANGU: Ustaa wa Mzee Mpili na tamaduni za soka duniani HISIA ZANGU: Ustaa wa Mzee Mpili na tamaduni za soka duniani

NILIMTAZAMA mlinzi wa Tottenham Hotspurs, Serge Aurier akiwa amerudi kwao Ivory Coast akicheza soka katika uwanja wa vumbi. Hakuwa peke yake, kulikuwa na mastaa wengine kutoka katika ligi mbalimbali ambao walikuwa wamerudi nyumbani.

Ni utamaduni wa wachezaji wa Afrika Magharibi. Wanalipwa mabilioni Ulaya, lakini wakati wa likizo wengine huwa wanarudi nyumbani kujifurahisha katika soka la vumbi kwa ajili ya kujikumbusha enzi zao za soka la vumbi. Hii ndio asili ya soka la Afrika. Nimegundua kila bara lina utamaduni wake katika maisha. Ni utamaduni huo katika maisha ndio unaozalisha utamaduni katika michezo. Ni utamaduni huo katika michezo ndio ambao unatofautisha bara moja na jingine.

Wazungu wao ni wakimya. Hawajui mambo ya Afrika wala Amerika Kusini. Wao wanaishi katika misingi ya ubinadamu tu, basi. Jinsi wanavyolea watoto wao na kujilea wenyewe ni kufuata sayansi halisi tu ya maisha. Wazungu wanaamini mchezaji afundishwe soka, awe na nidhamu. Aende uwanjani akatazamwe na mashabiki ambao wanaimba na kulewa, basi. Ndio maana hauwezi kukuta shabiki mzungu kabeba ungo na tunguri.

Amerika Kusini wao ni kama sisi. Kwa mfano, Brazil jinsi wanavyopenda kucheza soka mchangani. Lakini pia nilifurahishwa na namna ambavyo huwa wanafunga barabara zao mida ya usiku na kucheza soka. Humohumo katika mechi hizi za usiku unawakuta kina Ronaldinho nao wamo.

Basi tu kwa vile wakienda Ulaya wanalipwa mamilioni ya pesa ambayo hawawezi kuyapata katika soka lao, lakini naamini wachezaji wa Brazil wangetamani kucheza soka nyumbani kuliko Ulaya. Utamaduni wao wanaupenda na kuutukuza. Mara nyingi maisha wanayafanya kuwa mepesi.

Ni wepesi huohuo wa maisha huwa unaangukia hata katika tamaduni za mpira wetu. Angalia jinsi umaarufu wa Mzee Mpili ulivyoibuka ghafla. Ni utamaduni wetu. Kwanini kawa maarufu? Ana kona nyingine lakini kubwa ni vitisho vya ushindi wa mchezo wa soka nje ya uwanja. Inachekesha sana. Alianza kwa kuwashambulia viongozi wa Yanga kwa mikwara kibao, lakini mambo yalipoenda sawa kati yake na viongozi hao akahamishia mikwara yake kwa pambano la watani wa jadi. Wote tukabaki tunacheka.

Wazungu hawana watu kama mzee Mpili kwa sababu ya utamaduni wao. Hata kule Amerika Kusini hawana wazee kama hawa kwa sababu ya utamaduni wao. Afrika tuna wazee kama hawa kila kona kwa sababu ni utamaduni wetu.

Na unashangaa pale Mungu anapoweza kuunganisha matukio. Baada ya mikwara mingi kutoka kwa Mzee Mpili kwamba Yanga ingeshinda mechi kwa sababu ‘ana watu’ akimaanisha waganga wazuri nje ya uwanja kuweza kuifanya Yanga ishinde ni kweli Yanga ikashinda mechi. Ni uunganishi tu wa matukio lakini sisi wengine hatuamini. Unapoona Bernard Morrison anakosa bao kama lile kwa mpira wa Afrika ulivyo unaweza kuamini kweli ilitokana na ‘mambo ya Mzee Mpili’. Hata hivyo wengine tunaamini tofauti.

Jana niliandika hisia zangu za namna ambavyo Simba walipoteza mechi. Kuanzia kwa namna ambavyo walionekana kujiamini sana kabla ya mchezo tofauti na inavyopaswa kuwa.

Yanga wao wakaja uwanjani wakiwa wamepania sana kushinda mechi kama ilivyo kawaida yao katika miaka ya karibuni. Hii inakuwa sababu ya kwanza kubwa lakini kama una imani ndogo unaweza kudhani Mzee Mpili amesababisha yote haya.

Lakini hapohapo kumbuka kwamba wachezaji wa Yanga waliingia na hasira kali baada ya kuitwa wachezaji wa kuokotwa na msemaji wa Simba, Haji Manara.

Hapo hapo unarudi nyuma na kukumbuka mabao mawili ambayo yalikoswa na mastaa wawili wa Simba, Bernard Morrison na Meddie Kagere. Unacheka sana. Ukiunganisha matukio unaweza kudhani ni kweli watu wa Mzee Mpili walikuwa kazini.Lakini mara ngapi tumeona mabao ya wazi yakikoswa na wachezaji mahiri duniani wakiongozwa na Lionel Messi? Ni kitu cha kawaida katika soka. Tatizo ni pale utakapoamua uyafuate ya Mungu au ya Mzee Mpili.

Tatizo katika kipindi cha pili cha pambano lenyewe baada ya Yanga kupata bao la kuongoza kipindi cha kwanza, wachezaji wa Simba walipagawa na kuondoka katika mchezo wao wa uvumilivu ambao umewapatia matunda siku zote.Simba walijikuta katika papara na kushindwa kupasiana mpaka ndani ya boksi kama ilivyokuwa kawaida yao. Papara ilikuwa kubwa na walikuwa wanajaribu kupiga mashuti yasiyo na malengo kuelekea katika lango la Yanga bila ya kuonana kama ilivyokuwa kawaida yao.Muvu ya Kisimba zaidi ilikuja katika kosakosa ya Morrison ambapo pasi zilitengenezwa Kisimba zaidi hadi kumfikia Morrison.

Vinginevyo ilionekana kuwa rahisi kudhani Mzee Mpili alikuwa kazini kutokana na papara za washambuliaji wenyewe wa Simba ambao walikuwa wanakimbizana na muda uwanjani. Ni kitu cha kawaida katika soka.

Utamu wa soka la Afrika ni huu hapa ambapo wanatengenezwa watu wanaoimarisha saikolojia ya mashabiki kuelekea katika mechi kama hizi na nyinginezo. Hapa ndipo umaarufu wa Mzee Mpili unapowadia. Ndio utamaduni wetu na inapotokea Mwenyezi Mungu akaunganisha matukio basi Mzee Mpili anakula ‘kiki’ mitaani bila ya sababu za msingi.

Wenzetu huwa hawana mambo haya kwa sababu sio utamaduni wao lakini ukizunguka katika soka la Afrika, Ghana, Cameroon, Nigeria, Afrika Kusini na kwingineko haya ni mambo ya kawaida tu ambayo yanatia nakshi katika soka letu.

Ukiamua kuamini unaweza kuamini na itakuimarisha kisaikolojia, ukiamua kutoamini basi unaweza kuamini na inakuimarisha kisaikolojia. Kwa mfano, staa wa zamani wa Ghana, Nii Ordety Lamptey wa Ghana aliwahi kusema hadharani kwamba alishindwa kufikia mafanikio ya juu ya soka kwa sababu alirogwa nyumbani kwao Ghana.

Lamptey ambaye alianza kuwika akiwa kinda katika michuano ya kombe la dunia la vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 1992 pale Scotland baadaye alipata timu za maana Ulaya lakini alijikuta akishindwa kuwika kwa sababu mbalimbali ikiwemo majeraha.

Baadaye alihojiwa na vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi yake huku akidai kwamba kuna mizimu ilikuwa imetumwa kuhakikisha kwamba hapati mafanikio ndani ya uwanja akiwa Ulaya. Ilishangaza sana lakini ndicho alichoamini. Kina Mzee Mpili ndio utamaduni wa soka la Afrika.

Hawawezi kutoweka kwa urahisi kwa sababu wananogesha tu. ukweli ni kwamba hawana lolote la ajabu katika sayansi ya soka. Wananogesha tu lakini inabidi turudi katika misingi ya soka. Yanga wanastahili kuwa na timu nzuri ya vijana, kununua mastaa wazuri ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na benchi imara la ufundi huku wakiwalipa vyema wachezaji na benchi hilo. Mengin-eyo ni mbwem-bwe tu za soka la Afrika. ukiamua kuamini shauri yako.