Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 31Article 567046

Maoni of Sunday, 31 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Xavi Hernandez ni Guardiola mpya au Lampard mwingine?

HISIA ZANGU: Xavi Hernandez ni Guardiola mpya au Lampard mwingine? HISIA ZANGU: Xavi Hernandez ni Guardiola mpya au Lampard mwingine?

“....HATAKUJA kutokea tena mchezaji kama Xavi. Nilikuwa na bahati kucheza naye na kujifunza jambo jipya kila siku. Alifanya jambo gumu kuonekana jepesi, alirahisisha kila kitu...” aliwahi kusema hivyo Santi Cazorla. Staa wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Hispania.

Katika nyakati tofauti Ander Herrera, staa wa zamani wa Manchester United na Hispania naye aliwahi kusema “..Xavi ni mchezaji wa kipekee sana. Hakutakuwa na mchezaji kama yeye tena. Staili ya Barcelona na Hispania zilitengenezwa kupitia yeye..”

Halafu siku nyingine Cesc Fabregas alijikuta akilalamika akisema “Moja kati ya makosa makubwa ambayo tunaendelea kuyafanya ni kumtafuta Xavi mwingine. Siku zote watu wamekuwa wakiulizia kuhusu Xavi ajaye, jamani hakutakuja kuwa na Xavi mwingine...”

Siku nyingine akasikika Iker Casillas akisema: “...Kila siku watu wamekuwa wakiniuliza ni mchezaji gani wa Barcelona ambaye ningemchukua kwa ajili ya kuhakikisha tutatwaa ubingwa kila siku. Jibu langu ni lile lile. Xavi. Utawala wake wa mpira unamfanya awe mchezaji bora sana.”

Lionel Messi yeye alikwenda mbali zaidi lakini alikuwa amerahisisha zaidi. Alisema “Yeye (Xavi) ndiye mchezaji bora zaidi katika historia ya Hispania.” Naam. Hispania hii hii waliyocheza kina Raul Gonzalez, Andres Iniesta, Emilio Butrugueno na wengineo? Ndio, hii hii.

Kuna watu zaidi ya hamsini wamemzungumzia hivi Xavi. Kina Johan Cruyff, kina Arsene Wenger, kina Sir Alex Ferguson, kina Ronaldo de Lima, kina Cristiano Ronaldo. Kuna Xavi mmoja tu. Xavi Hernandez. Alitubadilisha mawazo kuhusu mchezo wa soka.

Binafsi nilimuita ‘ukuta’. Kwanini? Pasi zake. Aliurahisisha mpira kama ambavyo zamani ungekosa mtu wa kucheza naye huku ukiwa na mpira mkononi. Ungekwenda katika ukuta na kuupiga mpira ukutani kisha ungekurudia ulipo. Ndicho alichokuwa anafanya Xavi wakati anacheza. Unampa anakupa, unampa tena, anakupa tena, unampa tena anakupa tena.

Ndani yake alikuwa na maono makubwa. Haishangazi kusikia kile ambacho Herrera amesema juu yake. Xavi aliubadili ulimwengu kutoka kwa viungo wenye mbwembwe kwenda katika viungo ambao wanaurahisisha zaidi mpira. Kupitia Xavi wengine tulianza kuhesabu umakini wa viungo kupiga pasi kuliko kupiga chenga na tobo.

Simulizi ya Xavi kama mchezaji iliishia patamu. Wakati akiondoka Ulaya kwenda kuvuna pesa za Waarabu hadithi ya Xavi na sisi ilikuwa ni kama vile mwandishi mahiri wa kitabu cha mapenzi alikuwa akiandika mstari wa mwisho wa simulizi yake.

Muda si mrefu Xavi atarudi Barcelona kufungua ukurasa mwingine. Inanitia hofu. Ukurasa wa ukocha. Kujaribu kuwafanya wachezaji wengine wafanye kila alichokuwa anafanya wakati ule akiwa na jezi ya Barcelona. Ni kazi tofauti na inatia hofu kubwa, hasa kwa Barcelona ya sasa iliyojaa umaskini na ukosefu wa vipaji maridhawa.

Wachezaji kama yeye hawapo tena. Hawazaliwi mara nyingi. Xavi anaweza kuifanya Barcelona kurudi kuwa Barcelona tuliyoifahamu na kuipenda? Anaweza kurudisha staili ya tiktak ndani ya jezi za Catalunya? Ni swali gumu lakini ni mtihani unaomkabili.

Wengi watataka kuona kama Barcelona itacheza kama ilivyokuwa enzi zake. Hatudhani kama Xavi atafundisha mpira wa Sam Allardyce au Steve Bruce. Tunadhani atafundisha mpira aliofundishwa na Pep Guardiola. Hata katika kundi la wachezaji wasio na vipaji bado tunaamini kwamba Barcelona itakuwa bora kuliko Leicester City tofauti na ilivyo sasa ambapo Leicester City ni bora kuliko Barcelona.

Lakini hapo hapo tukumbushane tu namna ambavyo Xavi anaingia katika mkumbo wa mastaa wa zamani ambao wamerudi katika timu zao kama makocha baada ya ushujaa mkubwa wa zamani. Wakati mwingine mambo huenda sawa wakati mwingine huwa ovyo.

Frank Lampard na Chelsea? Mambo yalienda ovyo. Andrea Pirlo na Juventus? Mambo yalienda ovyo. Vipi kuhusu Ole Gunnar Solskjaer na United yake sasa hivi? Sidhani kama atafika Krismasi akiwa anapaki gari lake Carrington. Ananunua muda tu kwa sasa. Alan Shearer na Newcastle United yake? Mambo yalienda ovyo.

Hata hivyo, wapo ambao ,ambo yalienda poa. Hapo hapo Barcelona Cruyff na Pep Guardiola walifanikiwa. Pale Real Madrid Zinedine Zidane alifanikiwa. Huwa inatokea ingawa hesabu za waliofeli zinakuwa kubwa zaidi. Labda kwa sababu kazi yenyewe ni ngumu.

Kando ya jambo hilo hilo kuna jambo jingine. Wachezaji wengi mahiri sio lazima wawe makocha mahiri. Hata kama haurudi katika timu hiyo hiyo lakini unaweza kwenda kwingineko na bado ukafeli. Hawa ndio kina Diego Maradona, Roy Keane, Thierry Henry na wengineo. Imetokea mara nyingi.

Kitu kibaya zaidi kwa Xavi ni Barcelona. Nadhani amerudishwa pia kwa sababu ana DNA ya klabu. Lakini hata Ronald Koeman ambaye amefukuzwa naye alikuwa na DNA ya klabu. Unarudi Barcelona ukiwa na DNA, sawa, lakini ni kwa wachezaji wapi hasa? Ni kwa uchumi gani hasa?

Barcelona na Real Madrid zipo hoi kiuchumi. Barcelona imelazimika kuchukua kundi kubwa la wachezaji wa bure kutoka kwingineko. Hapo hapo kuna wachezaji wengi ambao sio wa staili ya Barcelona lakini wapo klabuni. Hawa ndio kina Memphis Depay.

Xavi atalazimika kufanya kazi na hawa hawa mpaka tuone matunda yake. Vinginevyo tunaendelea tu kujiuliza ni namna gani mabosi wa Barcelona watamsapoti ili atengeneze timu kali. Au atarudi La Masia na kukuza watu kama alivyokuzwa yeye?

Kwa sasa yetu macho tu. Wengine tunatamani kuona anakuwa Guardiola mpya pale Nou Camp. Hata hivyo katika kila kundi lenye kina Guardiola kando yake kunakuwa na kundi la kina Lampard. Mashujaa waliorudi klabuni wakafeli.

Haijalishi kwa kile alichokifanya Qatar akiwa kama kocha wa Al Sadd. Pale Nou Camp anarudi katika La Liga. Moja kati ya Ligi kubwa barani Ulaya. Fungate yake na kazi ya ukocha imefika tamati.