Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 22Article 558922

Maoni of Wednesday, 22 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Yanga walivyoloa tena kwa roho mbaya Nigeria

HISIA ZANGU: Yanga walivyoloa tena kwa roho mbaya Nigeria HISIA ZANGU: Yanga walivyoloa tena kwa roho mbaya Nigeria

ILIANZIA katika akili ya kijinga ya wageni Port Harcourt kudai kwamba wachezaji sita wa Yanga walikuwa na Uviko-19. Baadaye vita ikahamia uwanjani. Yanga walipigana vita kali katika jiji hili la tano kwa ukubwa nchini Nigeria na hawakutolewa kwa urahisi sana.

Rivers walifanya maarifa wachezaji sita wa Yanga waonekane kuwa na Uviko-19 wakati haikuwa kweli. Heritier Makambo, Tonombe Mukoko, Fei Toto na kipa Djigui Diarra ni miongoni mwao. Ilikuwa aibu kidogo kwao. Mabosi wa Yanga wakiongozwa na bosi mtendaji, Senzo Mazingisa waliazimia Yanga wasingecheza pambano hilo kama wasipoonyeshwa hati maalumu za kuonyesha mastaa hao walikuwa na maambuki ya ugonjwa huo.

Ukweli ni kwamba Wanigeria walikuwa hawana hati hizo na msafara mzima wa Yanga haukuwa na maambukizi. Kichekesho kilijitokeza wakati wa mabishano makali kando ya uwanja wakati Diarra alipodai alikuwa ametumiwa barua pepe mida ya asubuhi ikimwambia hana maambuziki.

Kufikia hapo Wanigeria walijua kwamba wameshtukiwa. Kamishina wa pambano alimaliza hadithi hii baada ya kufuata msimamo wa Yanga na kudai kwamba kama hakukuwa na hati za maambukizi ya Uviko-19, basi Yanga walikuwa wanaruhusiwa kuwachezesha mastaa hao.

Pambano lilipoanza mastaa wa Yanga walikuwa na ari kubwa. Tatizo lilikuwa kwa mwamuzi wa pambano. Alionekana kuwauma Yanga. Alikataa penalti mbili za wazi za Yanga katika dakika 20 za mwanzo za mchezo. Iliwashangaza hata Wanigeria ambao walikuwepo uwanjani.

Penalti ya kwanza Jesus Moloko alikuwa anaenda kutazamana na kipa wa Rivers katika boksi la adui. Mlinzi mmoja wa Rivers akamsukuma kwa nyuma. Mwamuzi akapeta. Yanga wakapigwa na butwaa.

Penalti ya pili ilikuwa ya wazi pia. Fei Toto alipokea pasi nzuri ya juu kutoka kwa Makambo. Akatazamana na kipa na kumkwepa. Kipa akauvaa mwili wake. Mwamuzi akapeta. Ilikuwa penalti ya pili ya wazi kama ingechezeshwa katika uwanja wa haki.

Baada ya matukio hayo mwamuzi akazidi kuwaudhi Yanga. Wakati Shomari Kibwana akipokea kadi ya njano kwa kucheza rafu ya kwanza, mchezaji mmoja wa Rivers alimkwatua makusudi Moloko mara mbili na hakupewa kadi yoyote.

Ukiachana na mwamuzi, pambano lilikuwa zuri. Yanga walicheza vyema pengine kuliko pambano lililochezwa Temeke wiki moja kabla ya mechi hii. Walikuwa na muunganiko mzuri wa kitimu kuanzia kwa kipa Diarra mpaka kwa Makambo.

Mtu ambaye aliwapa nguvu nzuri Yanga alikuwa Yannick Bangala ambaye mechi ya kwanza hakucheza. Alikuwa na utulivu wa hali ya juu. Yeye na Mukoko waliulinda vyema ukuta wa Yanga na kisha kumpa kibali kizuri Fei Toto afanye kazi kule mbele.

Katika winga, Moloko alifanya vyema upande wa kulia, lakini Yacouba hakuwa na madhara kabisa upande wa kushoto. Katikati Makambo alikuwa akiwaonyesha kitu ambacho Yanga walikuwa wakikikosa kwa kutokuwa na mtu kama yeye kwa kipindi cha takriban miaka mitatu iliyopita.

Makambo alikuwa na nguvu, stamina na kasi. Aliweza kuwasumbua vyema mabeki wa Rivers kwa kukaa na mipira na kuchezesha timu upande wa mbele. Haishangazi kuona kwamba alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliopewa Uviko-19 feki na Wanigeria.

Tatizo la Yanga lilikuja kipindi cha pili. Pumzi ilikata. Mbaya zaidi mchezaji nyota wa kipindi cha kwanza, Fei Toto ndiye aliongoza kundi la wachezaji waliochoka. Yanga haikusukuma tena mashambulizi kama kipindi cha kwanza.

Bahati nzuri kwao ni kwamba hata Rivers nao walionekana kuchoka. Achilia mbali kuchoka, lakini Rivers wenyewe sio timu ya ajabu.

Kama wangekutana na Simba ya kina Clatous Chama na Luis Miquissone sasa hivi wangekuwa nje ya michuano. Tatizo kubwa la Yanga ni kwamba hawakuwa na maandalizi mazuri ya kuanza msimu.

Ndani ya uwanja Yanga walihitaji nguvu mpya kutokana na timu kuchoka. Watu walioambatana na msafara wa Yanga wakaanza kumpigia kelele Kocha Mohammed Nabi afanye mabadiliko. Akamtoa Yacouba upande wa kushoto na kumuingiza Yusuph Athuman. Akamtoa Moloko na kumuingiza Deus Kaseke.

Hata hivyo, hatimaye Rivers walipata bao. Lilitokana na makosa ya Adeyum katika upande wa kushoto baada ya kukaba kizembe na kumruhusu winga wa Rivers aingie ndani na mpira na kuwakuta walinzi wa kati wakiwa hawajajiandaa. Akamchambua vyema kipa Diarra na kufunga.

Yalikuja mabadiliko mengineyo ya Saido Ntibanzokonza na Zawadi Mauya, lakini ilikuwa wazi kwamba mechi ilikuwa imekata roho katika jiji la Port Harcourt. Mpira ulimalizika dakika kadhaa baadaye na Yanga walikuwa wametolewa nje ya michuano.

Kichekesho kingine kilitukutuka katika uwanja wa Ndege wa Port Harcourt wakati timu ikiondoka. Kwa mujibu wa masharti ni kwamba abiria wote lazima wawe na vyeti vya Uviko-19 kabla ya kuondoka. Majina yalipoletwa, wale mastaa wanne wa Yanga ambao awali walitajwa kuwa na Uviko-19 wote hawakuwa na maambukizi.

Baada ya kurudi nyumbani kimyakimya ni wazi kwamba kocha Nabi ana kazi ya kuiunganisha Yanga kucheza kitimu zaidi na pia kuwa na pumzi zaidi. Hakuwa na pre season nzuri. Bahati nzuri kwake ni kwamba kuanzia sasa anaweza kuwatumia Khalid Aucho, Fiston Mayele na Djuma Shaban.