Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 16Article 542899

Maoni of Wednesday, 16 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

HISIA ZANGU: Yanga wametafakari hasara za Sarpong na Yikpe usajili huu??

HISIA ZANGU: Yanga wametafakari hasara za Sarpong na Yikpe usajili huu?? HISIA ZANGU: Yanga wametafakari hasara za Sarpong na Yikpe usajili huu??

NAFAHAMU kwamba Yanga wataachana na Michael Sarpong. Nafahamu pia wataachana na mshambuliaji mwingine, Fiston Abdoulrazaq ambaye walimchukua kwa mkataba wa miezi sita tu. Huyu wa pili ni kama vile Yanga machale yaliwacheza.

Kwa Sarpong Yanga waliamini kwamba walikuwa wamefuta makosa ya mshambuliaji aliyeitwa Yikpe Gnamien ambaye aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Nairobi huku mashabiki wakiwa na imani kubwa kwake.

Alikuwa na umbo kubwa na alionekana kama angeweza kuwa straika wa maana klabuni. Baadaye iligundulika kwamba Yanga walikuwa wameingia mkenge. Walikatisha mkataba wake kwa kumlipa pesa nyingi. Kabla ya hapo walikuwa wanamlipa mshahara mzuri.

Baadaye alikuja Sarpong ambaye najua anakaribia kuondoka na Yanga watalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fidia kwa kukatisha mkataba wake. Kabla hata hawajakatisha mkataba wake ikumbukwe kwamba Sarpong tayari alichota kiasi kikubwa cha pesa kusaini mkataba wa Yanga lakini pia analipwa mshahara mkubwa.

Kuna kitu cha msingi ambacho Yanga wanapaswa kukiangalia. Wachezaji wote hawa walitua Yanga bure kutokea walikotoka. Mikataba yao ilikuwa imeisha. Katika kipindi chote cha mikataba yao hawakununuliwa na timu nyingine. Nadhani walikuwa na walakini.

Related UCHAMBUZI: Hili la Ajibu Yanga inaweza kurudia yaleyale ya SarpongYanga wanahitaji kufanya jambo moja la maana. Washambuliaji wa maana ni adimu barani Afrika. Ni nadra kumkuta mshambuliaji wa maana ambaye hana timu. Yanga inabidi waangalie uwezekano wa kumng’ata jongoo kwa meno.

Kuna nyakati ambazo watalazimika kulimaliza tatizo la ushambuliaji klabuni kwao kwa kutoa pesa kununua mshambuliaji wa maana ambaye ana mkataba kwingineko kama wana uhakika kuwa atakuja kumaliza tatizo la mabao klabuni.

Tatizo klabu zetu zinapenda wachezaji wa bure ambao baadaye wanajikuta wameingia hasara ya pesa ambayo wangeweza kumnunua mchezaji wa maana kutoka kwingineko. Ni hasara ambayo nitakufafanulia kwanini Simba wameiepuka kwa kuwaongeza mikataba Mohamed Hussein na Shomari Kapombe.

Kwa mfano, kuna uwezekano mkubwa ambapo Yanga wamepoteza zaidi ya dola laki moja kwa kuishi na Yikpe na Sarpong katika klabu yao kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Kumbe wangeweza kwenda sokoni na kumnunua mshambuliaji wa maana mwenye thamani ya dola laki moja na kufuata tatizo la umaliziaji klabuni hapo.

Yanga haijapata mshambuliaji yeyote wa maana tangu kuondoka kwa Herritier Makambo klabuni hapo. Wamejaribu kila walipoweza na mshambuliaji aliyejitahidi kufunga mabao mengi klabuni alikuwa David Molinga ‘Falcao’.

Na yeye alionekana bora kwa sababu Yanga haikuwa na washambuliaji wa uhakika. Na hata sasa unaweza kutazama nyuma na kuamini kwamba Molinga alikuwa bora kwa sababu alifunga mabao mengi kuliko kina Sarpong.

Vinginevyo Molinga hakuwa bora na alikuwa na uzito mkubwa. Washambuliaji wa timu kubwa huwa wanapimwa na washambuliaji wengine wa timu kubwa. Molinga hana uwezo kuliko John Bocco, Meddie Kagere au Chris Mugalu.

Molinga pia hauwezi kumfananisha na Prince Dube. Ni mzuri kutokana na washambuliaji waliokuwepo Yanga wakati ule kina Yikpe. Hata hivyo, kiukweli Yanga ina viwango vyake ambavyo katika miaka ya karibuni viliwekwa na kina Makambo, Donald Ngoma, Amis Tambwe na wengineo.

Yanga kama wanaweza kumnunua mshambuliaji wa maana hata kwa Dola laki moja kwingineko wanaweza kufanya hivyo kuliko kuendelea kubahatisha. Tatizo timu zetu kubwa zimezoea wachezaji wa bure. Wapo ambao wamefanikiwa lakini wapo wengi ambao wamefeli.

Watazame watu wa Simba. wamelazimika kuwabakisha Kapombe na Tshabalala lakini kama wawili hao wangeondoka ina maana wangelazimika kutazama nje kununua walinzi wa pembeni wa maana. Na vipi kama walinzi hao wangechemsha? Ina maana wangeweza kujikuta wakilipa pesa kubwa zaidi ya ile ambayo wangetumia kuwabakisha kina Kapombe.

Angeweza kuja mlinzi wa kwanza akafeli, msimu ujao angekuja mlinzi mwingine akafeli, msimu mwingine angeweza kuja mlinzi mwingine akafeli. Baadaye mnajikuta katika gharama kubwa kuliko ile ambayo mngetumia kuwabakisha wachezaji wenu.

Mfano ulio wazi ni kwamba hata Yanga mpaka sasa wametumia pesa nyingi kuziba pengo la Makambo kuliko pesa waliyopokea kutoka kwa Horoya kwa ajili ya kumuuza staa huyo Mcongo. Katika soka unahitaji hesabu hizi.

Arsenal wamemlipa mshahara mkubwa Pierre Emerick Aubameyang kwa sababu walijua kwamba kama Auba angeondoka kikosini wangetumia pesa kubwa kupata mshambuliaji mwingine wa aina yake na wangeweza kupitia mchakato wa miaka mingi ambao ungegharimu pesa nyingi kupata mshambuliaji wa aina yake.

Yanga wamng’ate jongoo kwa meno tu. Waende sokoni wanunue mshambuliaji ambaye walau atawapa uhakika wa kufunga mabao 20 kwa msimu. Mshambuliaji ambaye anatoka katika Ligi imara, anacheza katika timu imara.

Zaidi ya hapo katika maeneo mengine wanunue wachezaji imara ambao watamuwezesha mchezaji imara kuonyesha uhodari wake. Hiki ndicho ambacho Simba wamefanya ingawa hawajanunua sana wachezaji. Walipata bahati ya kupata wachezaji wa bure wenye uwezo.

Vinginevyo pengo kati ya Simba na Yanga litaendelea kutanuka na kila siku watu wa Yanga hawataishiwa vilio kwamba wanaonewa na TFF. Nafahamu kwamba Yanga wasingependa kuishi katika dunia mbili tofauti na wenzao wa Simba. haijawahi kutokea mashabiki wa timu moja kati ya hizi wakakubali kuwa timu ya kawaida huku wenzao wakipanda juu.

Hii inatokea zaidi wakati huu ambao wote kwa pamoja wanaweza kushiriki katika michuano ya kimataifa. Itakuwa aibu kama timu moja itakuwa kali zaidi kuliko nyingine wakati wakubwa wa Misri na Morocco wanaweza kwenda mbali kwa pamoja.