Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 13Article 537610

xxxxxxxxxxx of Thursday, 13 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Historia ya mafunzo ya  udereva na ajali Tanzania

WAKATI akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/ 2022 hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema hadi kufikia mwezi Machi, 2021 matukio makubwa ya ajali 1,228 yaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini kilinganishwa na matukio 1,920 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Waziri anasema pamoja na kutolewa elimu kuhusu usalama barabani kwa wanafunzi 760,953 wa shule za msingi 14, madereva 275,768 wa bodaboda na abiria 5,361,859, hatua kali zilichukuliwa dhidi ya madereva waliokiuka Sheria za Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kufungiwa leseni kwa madereva 71.

Jumatatu iliyopita, Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani lilitangaza kufunga leseni za madereva 11 wa mabasi ya abiria yanayokwenda mikoani kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ukiwamo mwendokasi na uendeshaji wa hovyo, ukiwamo wa kuwapita madereva wengine katika maeneo hatarishi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Wilbrod Mtafungwa, pamoja na judi za polisi kuweka mikakati na kuongeza kasi ya kutoa elimu endelevu ya usalama barabarani kwa madereva, umma hata katika shule za msingi, bado wapo madereva wengi wasiozingatia kanuni, sheria na maadili ya taaluma ya udereva.

Kimsingi, kila siku ajali za barabarani hukatili uhai wa maelfu ya watu, kuwaacha wengine na ulemavu wa maisha na kuathiri mustakabali wa familia nyingi duniani.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Siku ya Kuwakumbuka Waathirika wa Ajali za Barabarani Novemba 18, 2018 inasema maisha ya watu milioni tano yanaweza kuokolewa katika muongo wa ‘Hatua kwa Ajili ya Usalama Barabarani Ulioanza 2011-2020.’

WHO lilisisitiza kuwa, lengo ni kupunguza kwa asilimia 50 majeruhi na vifo vitokanavyo na ajali za barabarani ifikapo 2020 katika juhudi za kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) hususani lengo la 3.6 linalohusu afya.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO watu 3,400 hupoteza maisha kila siku duniani kote kutokana na ajali za barabarani na athari zake kwa familia na jamii kwa jumla ni kubwa.

Wanaokufa, ndio hao waliokuwa walezi, watoa huduma na wazalishaji katika familia, kada, sekta na ngazi mbalimbali.

Vifo hivyo vya ghafla huacha kovu la milele kwa familia ikiwa ni pamoja na kwa majeruhi katika kila kona ya dunia na huongeza idadi ya mamilioni wanaosalia kuwa tegemezi kwa njia moja au nyingine huku majeruhi wakigharimu familia na taifa pesa nyingi kwa ajili ya matibabu na huduma nyingine.

Mmoja wa washiriki wa tathmini ya mafunzo na mchango wa wanahabari katika vita dhidi ya ajali za barabarani yaliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), anasema: “Kwa kuwa, karibu kila ajali ya barabarani inapotokea, kiwango cha udereva kinahusika na ajizi ya madereva wenyewe hubainishwa kama kisababisho au chanzo cha ajali.”

“Kwa msingi huo,” anasema: “Hatuna budi kuelekeza mtazamo na nguvu zetu katika eneo hili la udereva na madereva wenyewe.”

Kwa mujibu wa takwimu kutoka vyanzo mbalimbali, takribani asilimia 76 ya ajali zote za barabarani hutokana na mchango wa binadamu.

Imebainika kuwa, takribani asilimia 63 katika hizo asilimia 76 ni mchango wa madereva wenyewe.

HISTORIA YA MADEREVA TANZANIA

Ikumbukwe kuwa, tangu mwishoni mwa miaka ya 1930 na kuendelea hadi miaka ya 1950, zimekuwapo harakati za kijeshi na za kiuchumi nchini zilizosababisha ongezeko kubwa la mwendo (mobility) nchini Tanzania.

Mjumbe wa Baraza la Kitaifa la Usalama Barabarani, Henry Bantu, anasema; “Bila mwendo hakuna ajali.”

Vyanzo vinazitaja harakati hizo kuwa ni pamoja na zile za kijeshi wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na kuendelea, hususani magari ya majeshi, likiwemo Kings African Riffles (KAR).

“Harakati nyingine ni shughuli za miradi ya Overseas Corporation (OFC) ya Kongwa na Nachingwea pamoja na shughuli za mikongeni (silabu) zilizoajiri watu wengi kushiriki katika kilimo cha mkonge na uzalishaji wa katani hasa katika mikoa ya Pwani ya Tanganyika,” kinasema chanzo kimoja.

Kinaongeza: “Katika maeneo hayo, madereva ni kati ya wafanyakazi walioajiriwa harakaharaka ili waanze kazi bila kupoteza muda. Aidha, mfumo wa mafunzo ulikuwa wa kurashia-rashia, bila kuwapo mtaala wa mafunzo hayo.”

“Halikadhalika, wengi walifundishana wenyewe kwa uelewa wa bora liende tu. Ni madereva haohao ambao hatimaye walianza kuendesha uraiani…”

Mintarafu suala la madereva hao wa mtindo wa ‘Bora Liende’, mtaalamu mmoja wa mambo ya usalama barabarani anayekataa jina lake lisiandikwe gazetini anasema: “Walifanya hivyo na kuoneshana umahiri au kuoneshana ubingwa wao wa kwenda kwa mwendokasi kuliko wenzao, na kwa mbwembwe za kila aina, kushindana, kutambiana na kupiga ‘misere’ barabarani.”

Anaongeza: ‘Kwao, huo ndio ulikuwa udereva.’

Uholela huo katika matayarisho ya madereva barabarani uliendelea na kubarikiwa na sheria ya nchi (Driving School Act, 1965), ambayo kipengele kimojawapo kiliruhusu kuwa: “... Dereva yeyote mwenye leseni na ujuzi, anaweza kumfundisha mtu mwingine...” na hatimaye atahiniwe na kupata leseni ya kuendeshea gari.

Utaratibu huo uliendelea hadi kipengere hicho muhimu kilipobadilishwa mwaka 1996. Hapo ndipo msisitizo wa mafunzo katika shule za madereva ulipowekwa.

MATOKEO YA KUFUNDISHANA WENYEWE KWA WENYEWE

Katika mazingira kama hayo, mtu anaweza kujiuliza; “Je, katika mfumo huo wa awali wa kufundishana wenyewe kwa wenyewe, ulijengeka utamaduni wa aina gani barabarani?”

Jibu ni rahisi kuwa, “Kizazi cha madereva wale wa mfumo na utamaduni wa zamani, bado kipo na madereva wa namna hiyo bado tunao nchini na katika barabara zetu…”

Kimsingi, kiwango cha madereva hao walipoendesha barabarani hakikuwa cha aina moja na uelewa wao haukufanana kuhusu matumizi salama ya barabara; Walitofautiana sana, na utamaduni wa tofauti hiyo ni dhahiri sana upo hadi sasa.

MATOKEO YA UDEREVA WA ‘BORA LIENDE’

Kimsingi uthibitisho wa hali hiyo unabainika kutokana na aina ya udereva wa kushindana barabarani ambao madereva wengi wanao ingawa unasababisha madhara kwa maisha ya watu na mali zao.

Kwa mujibu wa uchunguzi, hali hiyo imezaa kasumba ya madereva wengi kunyang’anyana njia, ukosefu wa subira na kuvumiliana, papara barabarani, umbumbu uliopo katika kuzitambua hatari (zilizopo na zinazotegemewa), kuendesha kwa mwendokasi pindukia, usiojali uwezekano wa ajali, na umbumbu wa sheria na Kanuni za usalama barabarani.

Uchunguzi wa kitabia katika jamii unaonesha kuwa, wakati bado kwa wanaume kuna ugonjwa wa baadhi kushabiki mwenda kasi na udereva wa kihuni njiani, mtaalamu wa saokolojia katika Kanisa Katoliki aliyewahi kuwa Gombera wa Seminari Kuu ya Peramiho iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Padri Dk Titus Amigu anazungumzia tabia za wanawake akisema, baadhi wanaweza kuvutiwa na kumpenda dereva mwanaume kwa kuwa anaendesha gari kwa kasi na ana fujo barabarani.

Yote hayo yanayokiuka kanuni na sheria za usalama barabarani, ni baadhi mambo yaliyo kinyume na falsafa, mwenendo na utekelezaji wa udereva wa kujihami.

UJUZI WA DEREVA WA KUJIHAMI

Kwa mujibu wa wataalamu, dereva wa kujihami si kwamba anajua kwenda, bali namna ya kwenda; huamini daima kuwa barabarani ni mahali pa kuheshimiana, kushirikiana na kusaidiana.

Mkuu wa usalama barabarani katika Mkoa wa Morogoro, SSP Michael Deleli anasema: “Dereva wa kujihami anajua namna ya kufidia makosa ya madereva wengine wanaokengeuka barabarani ili asaidie kuepusha ajali na kusababisha usalama barabarani uendelee.”

Deleli anaongeza: “Dereva huyo wa kujihami anazijua, amezikariri na anaziheshimu sheria na kanuni za usalama barabarani.”

Naye Henry Bantu anasema: “Dereva huyo tayari wamejijengea utamaduni wa usalama barabarani na anayo hofu ya Mungu…”

Kila dereva anawajibika kujilinda, kujihami barabarani na anao wajibu wa kuwalinda, kuwaheshimu watumiaji wengine wa barabara na kuzuia ajali isitokee.

Kwa mujibu wa Bantu: “Dereva wa namna hiyo habahatishi na wala hababaishi katika tabia yake ya barabarani. Anajilinda yeye mwenyewe, anawalinda madereva wenzake, analitunza gari lake, shehena aliyobeba au abiria anaowasafirisha.”

Uchunguzi wa mwandishi wa makala haya katika mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam unaonesha kuwa, madereva wa aina hiyo, bado ni adimu nchini, na hasa kwenye magari na mabasi ya watu binafsi.

Bantu anasema: “Wengi wao bado ni ‘dereva - bora gari liende tu’. Wengi wa hao, wanajua tu kwenda na si namna ya kwenda; wanajua tu kusimama na si namna ya kusimama.”

UMUHIMU WA MAFUNZO KWA MADEREVA

Kwa msingi huo, ni dhahiri kuwa msingi wa udereva na madereva tulionao sasa imekuwa kichocheo cha ajali za barabarani nchini na hali hiyo inapaswa kurekebishwa hatraka ili kuokoa maisha ya Watanzania na mali zao.

Suala la mafunzo kwa madereva haliepukiki na maudhui ya mafunzo kwa madereva yawe ya usalama na kuaminika zaidi barabarani. Mafunzo kwa madereva yatiliwe mkazo na madereva wote tangu mafunzo ya awali, kujiendeleza na mafunzo ya rejea ya mara kwa mara, kwa kipindi kitakachopangwa na kukubalika.

Join our Newsletter