Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2020 07 02Article 503755

Maoni of Thursday, 2 July 2020

Columnist: TanzaniaWeb

Hofu kupata majibu ya ziada inavyokwamisha upimaji TB

Walengwa shaka yao HIV, corona

NI kampeni ya nyumba kwa nyumba kutoa elimu na kuhamasisha jamii kupima ugonjwa wa kifua kikuu, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, sasa zimefikia watu 6808.

Waendeshaji kampeni ni vilabu vya maradhi ya kifua kikuu, chini ya Shirika la Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Temeke (Mukikute), lililopo Temeke, ikifanya kazi kwa ubia wa karibu na Halmashauri ya Wilaya Temeke.

Makamu Mwenyekiti wa Mukikute, Seif Mchila, anasema nyendo zao karibuni zimekuwa ikionishwa na Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya, yaliyoanza tarehe 15 hadi kilele 26, mwezi uliopita.

Mchila anasema, utekelezaji wao wanashirikiana kwa karibu na Idara za Kifua Kikuu na Ukoma, Afya ya Akili na Dawa za Kulevya ya Manispaa ya Temeke, kuwaibua wangojwa wa kifua kikuu wa wilayani Temeke.

"Huwa wanapata huduma ya dawa katika zahanati zote za manispaa na wataalamu wa afya wa manispaa, hutoa mafunzo kwa wanachama wetu ya jinsi ya kuhudumia wagonjwa wa kifua kikuu," anasema.

Ili kunusuru jamii na janga la kifua kikuu, wabia hao wamekuwa wakiwaelekeza watoa huduma wa Mukikute, kuwapelekea dawa wagonjwa walio mbali na zahanati.

"Unajua siyo sisi tu tunaoibua wagonjwa, bali wapo wanaokwenda hospitali wenyewe na kama watakuwa wanaishi mbali na zahanati, watoa huduma wa Mukikute hupewa jukumu kuwapelekea dawa nyumbani," anasema.

CHANGAMOTO

Mchila ana ushuhuda wa changamoto, baadhi ya wanaojitokeza katika tukio hilo ni waoga na wanahusisha na uwezekano wa kugundua maradhi mengine.

Anasema, inachangiwa na uchache wa waliojitokeza kupima afya ya kifua kikuu, ingawa idadi ya waliofikwa na kupata elimu ni kubwa.

Ni elimu iliyotolewa na wahamasishaji kutoka klabu za TB ambazo ziko chini ya shirika la Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Temeke (Mukikute), yenye maskani eneo la Temeke.

"Kata hizo ni Azimio, Kiburugwa na Keko, lakini idadi ya waliojitokeza kupima kujua kama wana maambukizi ya kifua kikuu 166 tu, kati ya watu 6808 waliofikiwa na klabu zetu za TB," anasema Mchila.

Anasema, watu 130 katika Kata ya Keko walipimwa na 10 ndio waligundulika kuumwa; kata ya Azimio kuna watu 15 waliopimwa, saba kati yao wakigundulika kuwa na kifua kikuu.

"Kwa upande wa Kata ya Kiburugwa walijitokeza watu 21 waliopima afya zao na wawili kati waligundulika kuwa na TB, wote hao kutoka katika kata hizo wameshaanza kutumia dawa," anasema.

KWA NINI HAWAPIME?

Mdau huyo wa afya ya umma, anasema sababu kubwa ya kutopima afya, ni hofu kwamba ama wangezuiwa kwenye kambi za wagonjwa wa corona au kupimwa virusi vya Ukimwi.

"Klabu zetu zimefanya kazi kubwa kwenye kampeni hizo, lakini hofu hiyo," anasema, akieleza kuwa inaonyesha bado kuna haja ya elimu zaidi kwenye jamii, kutambua vyanzo vya ugonjwa huo na kuuepuka, kuliko kuogopa kupima afya.

"Haikuhusiana na mambo ya corona au Ukimwi, ingawa dalili za maambukizi ya kifua kikuu zinafanana na Ukimwi," anasema.

Mchila anasema, licha ya wahamasishaji wa klabu kujitahidi kufafanua, baadhi ya watu waliofikiwa walisita kuafiki, wakisisitiza wanahofia ama kuwekwa karantini au kupimwa Ukimwi.

Anasema, walengwa wa kampeni walikuwa watu wa rika zote, wakiwamo wanaopatikana katika vilabu vya pombe za kienyeji, watumiaji dawa za kulevya na walioko kwenye 'mageto'.

Pia, anasema kuna shida zilizo juu ya uwezo wao na jamii kwa ujumla, kama vile kukosa fedha za kuchangia vipimo, mtu anapohisi ugonjwa, lakini akapima makohozi na hakukutwa na athari yoyote.

"Yaani ni kwamba, iwapo TB haitaonekana katika makohozi, mgonjwa analazimika kupiga X-ray ambayo anatatakiwa angalau kuchangia gharama kidogo ya Sh. 15,000, lakini mtu hana," anasema.

Anashauri uwezekano wa kutolewa huduma zote kwa wagonjwa wa TB bure, hasa watu wa hali ya chini, ambao Mukikute imewatembelea baadhi yao na kuwapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.

KIFUA KIKUU?

Dk. Emmanuel James, kutoka Kitengo cha Kifua Kikuu, katika Zahanati ya Tambukareli, iliyoko Kata ya Azimio, anasema ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria visivyoonekana kwa macho ya kawaida, bali darubini.

"Kuna aina mbili za kifua kikuu kinachoshambulia mapafu na nje ya mapafu kama mifupa. Lakini ikumbukwe kwamba, kifua kikuu cha mapafu ndiyo chanzo cha maambukizi," anasema Dk. James.

Anasema namna mtu anavyoambukizwa ni kwa njia ya hewa kutoka kwa mwenye ugonjwa ambaye hajaanza matibabu.

"Vimelea hivyo husambaa kwenye hewa na iwapo kuna mtu mwingine ambaye hana ugonjwa huo, akivuta hewa hiyo anaweza kuambukizwa kirahisi, hivyo ni vyema watu kupima afya zao," anasema.

Dk. James anasema, katika zahanati hiyo, kati ya Januari hadi Machi mwaka jana, watu 71 walijitokeza kupima afya dhidi ya kifua kikuu, lakini kwa mwaka huu katika kipindi kama hicho kuna mahudhurio ya watu 66.

"Nimejaribu kutoa mfano huo mdogo, lakini ukweli ni kwamba elimu zaidi inahitajika kwa jamii, ili kutambua umuhimu wa kupima afya, pia kuzingatia ratiba ya matumizi ya dawa za kifua kikuu," anasema.

Dk. James anasema katika zahanati ya Tambukareli, wagonjwa wanaoibuliwa na klabu ya TB ya eneo hilo, wanaogunduliwa hufika kupata dawa.

Anasema, si kila anayeumwa kifua kikuu ana VVU, hali kadhalika si kila anayeishi na VVU ana kifua kikuu, ila kwa kanuni kila anayehisiwa anao anashauriwa kupima na akikutwa nayo, ataanzishiwa dawa za kupunguza makali ya VVU na zinazozuia magonjwa nyemelezi.

"Kwa ujumla ni kwamba, kifua kikuu kinatibika pale mgonjwa anapozingatia maelekezo na taratibu za matibabu na hasa ratiba ya kunywa dawa, ambayo baadhi ya wagonjwa wamekuwa hawaizingatii," anasema.

Anafafanua dawa hizo hutolewa kwa utaratibu maaluma wa umezaji kila siku, kwa usimamisi wa mtaalamu afya au mwanajamii aliyepata mafunzo.

Join our Newsletter