Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 20Article 552541

Maoni of Friday, 20 August 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Inasikitisha; faru wanateketea kutokana na imani potofu

Inasikitisha; faru wanateketea kutokana na imani potofu Inasikitisha; faru wanateketea kutokana na imani potofu

Juni 30, mwaka 2019, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, alikaririwa na vyombo vya habari akiwataka Watanzania kuachana na dhana potofu kuwa pembe za faru zinasaidia kuongeza nguvu za kiume.

Kigwangalla ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu, alisema huo ni uzushi na kwamba pembe hizo hazina msaada wowote katika kuondoa tatizo hilo kwa mtu ambaye analo.

"Kisayansi haisaidii kitu, haiongezi chochote kwa sababu ni melanini kama iliyoko kwenye nywele za binadamu. Basi kama wanadhani pembe hizo zinasaidia, wakinyoa nywele wazisage na kutumia kama itawasaidia lolote," alisema Kigwangalla.

Chapisho moja linalopatikana katika https://rhinosos.com/myths-about-rhino-horn-dont-buy-it/ likiwa na kichwa cha habari ‘Ukweli Kuhusu Pembe za Faru ambalo haya yanaligusia pia, linaonesha kwamba mbali na nywele, vitu vinavyotengeneza pembe za faru ndivyo vimo kwenye kucha zetu pia.

"Fikiria unachukua kucha (na nywele zako), unazisaga kisha unakunywa ili zikutibu matatizo yako (ikiwemo tatizo la nguvu za kiume). Kama hili linaonekana jambo la kushangaza kwako basi ndivyo ilivyo kwa wanaotumia unga wa pembe za faru wakiamini kuna dawa."

Hivi karibuni kauli ya kuwaonya Watanzania dhidi ya dhana hii potofu imetolewa tena: "Kama unadhani unga unaopatikana baada ya kusugua au kusaga pembe ya faru unaongeza nguvu za kiume hakika utakuwa umekosea sana."

Safari hii anayetoa angalizo hilo ni mratibu wa uhifadhi wa wanyamapori hao nchini Tanzania, Philbert Ngoti.

Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) uliowahusisha wahariri na waandishi waandamizi wa habari, Ngoti anasema: “Kuna uvumi tu ulitokea mji mmoja huko India kuwa unga wa pembe za faru unaongeza nguvu za kiume lakini utafiti ambao umefanyika, umebaini kuwa si kweli.”

Mratibu huyo anasema idadi ya faru imeongezeka nchini baada ya kutoweka kwa asilimia 90 kutokana na kuuawa na majangili na hivyo anaonya hali hiyo isitokee tena.

Ni katika muktadha huohuo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro, anaitaka jamii kuachana na imani hiyo potofu. Dk Ndumbaro anaitaka jamii kuungana na Serikali katika kumlinda faru ambaye ni kivutio kikubwa cha utalii hapa nchini.

Anasema kuwapo kwa imani hiyo potofu kumepelekea faru kuwindwa sana na kuna baadhi ya nchi zimekuwa zikinunua pembe hizo za faru kwa bei ya ajabu.

Anasema kimsingi dhana hiyo potofu pia imesambaa sehemu nyingi za dunia.

Anasema kutokana ni hilo, imeilazimu Serikali ya Tanzania kujizatiti katika kuwalinda faru kwa kuwawekea vifaa maalumu kwa ajili ya ulinzi ili wasiweze kuuawa.

Akizindua zoezi la uwekaji wa alama pamoja na vifaa maalumu kwa faru katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyama hao ambao ni zao kubwa la utalii nchini, Dk Ndumbaro anasema kuhifadhi faru kunataka nguvu ya ziada pamoja na akili ya ziada.

Anasema hiyo ni kwa sababu binadamu ni kiumbe mharibifu na tayari ameingiza mawazo yake kuwa nyara hizo za Taifa zina nguvu ya ziada.

Kufuatia hali hiyo ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ushirikiane na Idara ya Wanyamapori kuhakikisha wanakamilisha kuweka alama na vifaa maalumu kwa ajili ya utambuzi na ulinzi kwa faru wapatao 45 badala ya kuwawekea vifaa hivyo faru 20 pekee waliokuwa wamepanga kuanza nao.

Waziri anasema lengo ni kuhakikisha faru wote katika eneo hilo wanakuwa salama zaidi.

Dk Ndumbaro anafafanua kwamba, faru wote wanatakiwa kuwekewa vifaa kwa sababu wale 25 kati ya 45 ambao watakuwa wamesalia wanaweza kukutana na balaa lolote, kitu ambacho serikali haiko tayari kuona kikitokea.

Anasema kama uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro una changamoto yoyote wamfikishie ili kuhakikisha faru wote wanapata alama za utambuzi na ulinzi kwa sababu mitambo iliyopo ina uwezo wa kufuatilia nyendo za faru zaidi ya 100,000 kwa ajili ya usalama wao.

Katika hatua nyingine, Dk Ndumbaro ameuagiza Uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha faru wenye watoto wadogo wanahifadhiwa katika maeneo maalumu hadi pale faru wadogo watakapokuwa wakubwa na kurudishwa katika mazingira yao ya asili ili wasiliwe na fisi.

Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba fisi wamekuwa tishio kubwa kwa watoto wa faru na katika eneo la Ngorongoro kuna idadi kubwa ya fisi.

Dk Ndumbaro anafafanua sababu za kuliwa kwa faru wadogo na fisi kunatokana na tabia ya faru weusi wanapokuwa wanatafuta malisho huwaacha nyuma watoto wao, hivyo kuwa rahisi kwa fisi kutumia nafasi hiyo kuwavamia na kuwala.

Anasema kutokana na umuhimu wa fisi kiikolojia na kiutalii haiwezekani kuwaondoa badala yake jambo linalotakiwa kufanywa ni kuhakikisha faru watoto wanalindwa kwa kuwaondoa katika mazingira hatarishi.

Dk Ndumbaro pia ameagiza uongozi wa hifadhi hiyo kutenga eneo maalumu kwa ajili ya faru wazee. Kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu zilizopo, faru wanapozeeka hupoteza uwezo wa kuona na ndio maana anaagiza kutengwa kwa eneo maalumu kwa ajili ya faru wazee, hatua ambayo pia inanogesha utalii katika mbuga hiyo.

Kamishna Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Freddy Manongi, anasema Ngorongoro ni eneo pekee duniani ambalo watalii wanaweza kuwaona faru weusi katika mazingira yao ya asili.

Kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo katika kumlinda faru, Dk Manongi anasema ni kutokana na uwepo wa matumizi mseto katika eneo moja, hali inayochangia ugumu kwa kiasi fulani kuwalinda faru hao.

Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Maurus Msuha, anasema zoezi la kuweka alama kwa faru ni utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana faru yanalindwa kwa mbinu za kisasa.

Anasema faru huwekewa alama za utambuzi ili kuwafuatilia mienendo yao kwa urahisi zaidi.

Suala la faru kuzuliwa mambo ambayo hayaingii akilini na ambayo yameshindwa kuthibitishwa kisayansi yapo takribani manne kwa mujibu wa chapisho lililotajwa hapo mwanzo.

Makala hiyo inasema kwamba, vijana wanaozaliwa sasa wanapaswa kuelimishwa kwamba imani hizi potofu ambazo ni za siku nyingi hazina ukweli wowote wala hazitokani na tafiti za kisayansi.

Kisha mwandishi wa chapisho hilo anasema: "It is only through education that we find a path to success in the war on rhino horn trafficking," ambayo tafsiri yake inaweza kuwa "Ni kupitia utoaji wa elimu inaweza kuwa njia sahihi katika kushinda vita dhidi ya ujangili na usafirishaji wa pembe za faru."

Uzuaji wa kwanza kuhusu faru ni imani potofu ni ule unaonesha kwamba pembe za wanyama hao zina dawa inayotibu magonjwa kadhaa. Katika nchi za Bara la Asia, kuanzia Malaysia, Korea ya Kusini, India hadi China, pembe za faru zinaaminika kimakosa kwamba zina uwezo wa kutibu idadi kadhaa ya magonjwa kama homa, rumatizm na gauti.

Ilikuwa inaaminika kwamba, unga wa pembe hizo unaweza pia kutibu sumu kwa mtu aliyeumwa na nyoka, kumwondolea mtu ndoto mbaya na kuona maruweruwe, homa ya matumbo, kutapika, kumsaidia mtu aliyekula chakula chenye sumu na kudhibiti mashetani.”

Lakini hakuna ushahidi wowote unaofahamika wa mtu aliyenufaika na unga wa faru kumtatulia matatizo hayo.

Hii maana yake ni kwamba, ukitaka kufa haraka, wewe sumbuliwa na matatizo hayo kama kuumwa na nyoka au kula chakula chenye sumu kisha ukategemea unga wa pembe za faru ukusaidie badala ya kwenda hospitali!

Imani nyingine potofu ni hiyo iliyoanza kuzungumzwa katika makala haya ya kuongeza nguvu za kiume. Chapisho hilo pia linasema tafiti mbalimbali za kisayansi zimeonesha kwamba hakuna ukweli wowote katika hilo.

Kisha chapisho likahimiza wenye matatizo hayo kuwaona madaktari au kutumia bidhaa ambazo tayari ziko sokoni na wanaweza kuziagiza kwa njia ya mtandao. Wakitaka waandike “Viagra” au “Cialis” kwenye injini ya utafiti ya Google, watapata msaada.

Hata hivyo, inaaminika kwamba tatizo la nguvu za kiume kwa zaidi ya asilimia 50 linatokana na saikolojia. Vitu vingine vinavyochangia tatizo hilo, ni lishe duni, baadhi ya magonjwa na hata baadhi ya aina za dawa.

Vilevile kuna imani huko Vietnam kwamba eti kama umelewa pombe au dawa za kulevya, unga wa pembe za faru utakuondolea uchovu wa ulevi (hangover), kitu ambacho pia hakijathibitishwa na utafiti wowote wa kisayansi.

Chapisho hilo linasema: "Hata kama ingekuwa kweli, ni sahihi kweli kuua faru ili akuondolee uchovu wa ulevi?"

Sababu ya nne inayotajwa ni watu kutumia pembe za faru kama mapambo yenye thamani kwenye baadhi ya vitu wanavyovaa ili kuona ufahari. Mtu kwa mfano, anataka avae miwani ambayo fremu zake ni pembe za faru ili watu wamjue ana pesa.

Chapisho linasema huu ufahari wa kuhatarisha wanyama ambao wako hatarini kutoweka duniani ni wa hovyo sana. Chapisho hilo linashauri mataifa yapitishe sheria kali inayokataza matumizi ya pembe za faru kwa aina yoyote ile.