Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 28Article 581668

Maoni of Tuesday, 28 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

JICHO LA MWEWE: Adios Amigo Sergio Lionel Kun Aguero

Sergio Kun Aguero Sergio Kun Aguero

Unatazama namba. Unatabasamu. Kipi bora kuliko pesa? Amestaafu soka Kun Aguero. Kifua kilimbana katika pambano la Barcelona dhidi ya Alaves Oktoba 30 mwaka huu. Madaktari baadaye walimuamuru aachane na soka. Ilikuwa ni tahadhari nzuri ambayo wangeweza kumpa.

Wiki iliyopita akamwaga machozi katika mkutano na waandishi wa habari pale Nou Camp. Hata Pep Guardiola alisafiri kwenda kuhudhuria mkutano huo. Alikwenda kwa sababu alikuwa mchezaji wake City au kwa sababu Pep bado ni shabiki wa Barcelona? Nadhani jibu la kwanza ni sahihi.

Wiki hiyo hiyo Aguero alirudi nyumbani kwake Buenos Aires pale Argentina akachoma nyama na familia. Inawezekana roho inamuuma kwa kuachana na soka, lakini ukweli ni kwamba labda imuume katika masuala ya kipesa zaidi. Huku katika soka, hasa katika mabao hakuna ambacho tunamdai.

Alipata sifa anazostahili? Hapana, lakini Kun Aguero anabakia kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora kuwahi kuupamba uso wa ulimwengu. Tatizo lake ni moja tu, hakucheza Real Madrid, Manchester United, Arsenal, Liverpool, AC Milan, Chelsea au Barcelona. Subiri, ni kweli alicheza Barcelona lakini alivaa jezi mara nne tu. Kwa tunaomfahamu tunaweza kusema hakucheza.

Katika ardhi ya Malkia, Aguero anaweza kuwa mchezaji bora zaidi wa kigeni kama utahesabu namba. Tatizo hatumuimbi sana kwa sababu hakucheza timu zetu.

Aguero ni mfungaji bora wa muda wote Manchester City. Waingereza watapiga kelele kuhusu mastaa mbalimbali wa zamani waliopita City, lakini Aguero anasimama kama bora zaidi. Aliifungia City mabao 260. Anayemfutia? Mkongwe wao, Eric Brook ambaye alifunga mabao 177.

Aguero ndiye aliyeifungia City mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu. Ameifungia mabao 184. Anayefuatia? Raheem Sterling, ambaye ameachwa mabao 82 nikimaanisha Sterling ana mabao 102. Sidhani kama Sterling ana maisha marefu City kuziba pengo hilo.

Katika historia ya Ligi Kuu ya England yote, Aguero anashika nafasi ya nne. Kaachwa mbali na Alan Shearer mwenye mabao 260, Wayne Rooney, 208 na Andy Cole, 187. Hata hivyo, Aguero anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika timu moja tu. yote hayo kayafunga akiwa na City tu.

Hao walio juu yake wote ni Waingereza. Wamekulia pale pale. Kama Aguero angekuwa amekulia England hapana shaka angekuwa ameshawaacha mbali hao wengine. Ni rahisi tu kufikiria. Shearer amefunga mabao hayo akiwa na Southampton, Blackburn Rovers na Newcastle United.

Rooney amefunga mabao hayo akiwa na Everton, Manchester United na kisha Everton tu. Cole ndio usiseme. Amefunga mabao hayo akiwa na timu zaidi ya tano. Usidhani kuwa Aguero angezaliwa England angeanza kutamba Manchester City.

Si ajabu angeanzia Crystal Palace, kisha Leicester City halafu akatua City. Na si ajabu pia baada ya kuondoka City angeenda klabu nyingine ya England. Lakini yeye hakuwa na mwanzo huo England na pia alipoachana na City akaamua kwenda Hispania.

Haishangazi kuona kwamba katika wote hao walio juu yake na chini yake, Aguero ndiye mchezaji mwenye wastani mzuri kwa dakika za kufunga mabao hayo. Alifunga bao kila baada ya dakika 108. Kwa mfano, Shearer ana wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 146.

Aguero ndiye mchezaji aliyetupia hat trick nyingi zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England. Ametupia hat trick 12. Kabla ya hapo Shearer alikuwa ameburuza kwa rekodi hiyo kwa miaka mingi. Alitupia hat trick 11.

Aguero pia anashikilia rekodi ya kupiga mabao mengi katika mechi moja. Hii anaishikilia pamoja na wenzake kina Dimitar Berbatov, Shearer, Jermain Defoe na Andy Cole. Ilitokea jioni ya siku moja Newcastle United walijipendekeza kwake akiwa katika moto na akafunga mabao matano katika ushindi wa mabao 6-1 wa City dhidi ya matajiri hawa wapya. Haitokei mara nyingi katika soka la kiwango cha juu.

Aguero amewahi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi mara saba. Hakuna mchezaji yeyote katika historia ya Ligi Kuu ya England aliyewahi kufanya hivyo. Aguero pia aliweza kufunga mabao zaidi ya 20 ya Ligi Kuu ya England kwa misimu mitano mfululizo. Ni Thierry Henry pekee ambaye amewahi kufanya hivyo.

Aguero amewahi kucheza dhidi ya timu 33 tofauti katika Ligi Kuu ya England. Kati ya timu hizo amezifunga timu 32. Ni timu moja tu ambayo alishindwa kuifunga. Bolton Wanderers. Bahati yao ni kwamba alikumbana nao mara moja tu wakashuka daraja.

Kwao Argentina, Aguero anatisha ingawa kidogo amefunikwa na rafiki yake wa karibu, Lionel Messi. Pamoja na ukame mwingi wa mataji ambao Argentina wamepitia kipindi hiki, huku wakitwaa Copa America tu Julai mwaka huu, Aguero ana rekodi nzuri za kuvutia za kupachika mabao kuliko baadhi ya wakongwe.

Aguero ni mfungaji wa tatu bora wa muda wote Argentina. Wa kwanza ni Lionel Messi mwenye mabao 80 na kila siku anazidi kuyoyoma tu. Wa pili ni Gabriel Batistuta mwenye mabao 54. Wa tatu ni Kun Aguero mwenye mabao 42.

Kama Aguero asingestaafu na angeendelea kucheza walau kwa miaka mitatu ijayo nadhani angempita Batistuta. Ni wazi kwamba asingemfikia Messi, lakini angempita Batistuta. Lakini subiri kwanza, kumbuka kwamba kwa mabao hayo 42, tayari Aguero amefunga mabao mengi kuliko shujaa wa taifa hilo, Diego Maradona ambaye amefunga mabao 34 tu.

Kama Kun angekuwa Muingereza sifa hizi zingekuwa zinaanikwa sana kama ambavyo kwa sasa huwa tunasikia namna ambavyo sifa za Harry Kane zinaanikwa. Hata hivyo, Kun ni Muargentina na ataendelea kuwa Muargentina.

Kitu kingine ambacho pengine kilimharibia Kun mwenyewe ni kuondoka Atletico Madrid na kufuata pesa za mafuta Etihad. Baada ya kuonyesha makali yake na Atletico nadhani Kun angeweza kwenda Barcelona wakati ule au Real Madrid.

Hata hivyo, Kun ni miongoni mwa mastaa wakubwa ambao waliamua kufuata pesa za mafuta pale Etihad na kutengeneza himaya yao. Wengine ni kama vile Kelvin De Bruyne, David Silva, Vincent Kompany. Wangeweza kuwa wakubwa zaidi kama wangeenda Madrid au Barcelona na kutamba katika ufalme wa Ulaya pamoja na kutazamwa kwa wingi katika mechi za El Clasico.

Hata hivyo, yeye aliamua tofauti na kwenda kujificha katika jiji lenye mvua nyingi Manchester. Labda ndio maana kuna wakati hapewi sifa anazostahili. Kwa namba hizi alizokuwa nazo City kama angekuwa nazo Madrid halafu pia akatwaa ubingwa wa Ulaya, si ajabu angekuwa anaingia katika tatu bora za mwanasoka bora wa dunia. Hata hivyo, haikuwahi kutokea.