Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 02Article 567433

Maoni of Tuesday, 2 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

JICHO LA MWEWE: Aucho anatufundisha kucheza mpira rahisi, tumuige

Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho akijaribu kuwatoka wachezaji wa Azam Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho akijaribu kuwatoka wachezaji wa Azam

Niliendelea kumtazama mchezaji anayeitwa Khalid Aucho katika pambano la Yanga dhidi ya Azam juzi Uwanja wa Mkapa. Kiungo maridadi wa Uganda kwa sasa anawapagawisha watu wa Yanga. Hana maajabu makubwa isipokuwa anaufanya mpira kuwa rahisi.

Aucho anautaka mpira kisha akiupata hautaki tena. Anauachia unakwenda kwa mtu mwingine. Ni fomula rahisi ya viungo wa kisasa. Mwasisi wake katika zama hizi? Ni Xavi Hernandez wa Barcelona ile iliyosumbua dunia miaka kadhaa iliyopita.

Labda kwa sababu zama zimebadilika, ndiyo maana mashabiki wa Yanga wanapagawa kuhusu Aucho. Zamani mchezaji wa aina ya Aucho asingependwa sana na mashabiki. Zamani mashabiki walikuwa hawazingatii hesabu za pasi wala usahihi wake (accuracy). Zamani mashabiki wapenda sana chenga na tobo.

Vile vile zamani tulipenda zaidi wachezaji wanaokokota sana mpira wakati mwingine bila ya sababu za msingi. Hawa kina Aucho ndio wameleta mpira mpya na kwa sababu mashabiki wameanza kuelimika kujua mpira ni nini ndio maana mchezaji kama yeye anaimbwa sana. Mashabiki wamejua umuhimu wa kuurahisisha mpira.

Kuna viungo wetu ambao nawafahamu. Anachukua mpira huku akiangalia magharibi, anamuona mwenzie akiusubiri mpira, hampasii, anageuka upande wa mashariki halafu anageuka tena upande wa Magharibi na kumpasia yule yule ambaye aliamua kutompasia awali.

Wakati fulani Thaban Scara Kamusoko alikuja kutufundisha hiki hiki Aucho anachofanya kwa sasa. Kucheza mpira rahisi. Inaonekana somo bado halijawaingia viungo wetu wengi na bado wanacheza mpira mgumu. Sasa amekuja Aucho anayetufundisha kucheza mpira rahisi.

Katika eneo la mbele sina shida sana. Eneo hilo linahitaji ubunifu na ubunifu ni kipaji. Hapo ndipo tunapowaachia akina Clatous Chama watupe somo. Hilo ni eneo la uwezo binafsi. Chama anajua wakati gani wa kuachia mpira, wakati gani wa kujaribu kupenya, wakati gani wa kupiga shuti.

Hata hivyo, kama mpira ukimkuta Chama yupo nyuma ni lazima atacheza mpira rahisi. Akienda mbele anaweza kuchukua maamuzi mengi binafsi kwa kadri anavyojisikia. Hilo ndilo eneo unaloweza kuhatarisha mambo mengi tofauti na huku nyuma anakocheza Aucho.

Kina Ronaldinho na Zinedine Zidane walipata bahati nzuri ya kucheza mbele na kufanya wanavyojisikia. Katika eneo analocheza mchezaji kama Aucho ni nadra kufanya unachojisikia. Inabidi ucheze mpira rahisi na sio kufanya mambo mengi yasiyo na maana.

Zamani walikuwepo viungo wengi kama Aucho lakini tulikuwa hatuwakubali kwa sababu tulipenda wachezaji wenye udambwidambwi. Licha ya kusifiwa sana lakini sijaona Aucho akimvalisha mtu kanzu au kumpiga tobo. Amejikita katika kucheza mpira rahisi ambao unaipa timu yake umiliki na uanzishwaji mkubwa wa mashambulizi kuanzia nyuma.

Tuwafundishe vijana wetu kucheza mpira rahisi. Huu ndio mpira wa kisasa zaidi. Haishangazi kuona dunia nzima inaiga kile ambacho Pep Guardiola anafanya. Kupiga pasi nyingi kunamfungua adui kuliko mchezaji mmoja kukimbia na mpira kwa muda mrefu hata kama uwezo huo anao. Aucho ni mchezaji wa Pep kuliko viungo wetu wengi nchini.

Maswali ya msingi baada ya kuona kiwango cha Aucho ni mengi. Jambo la kwanza ni namna ambavyo ameibadili Yanga kama timu katika suala la umiliki wa mpira. Yanga wamerudi katika zama za ‘kampa kampa tena’. Enzi za Kamusoko. Inafurahisha kuwatazama.

Lakini nahisi safari ya Mukoko Tonombe imewadia. Atacheza wapi? Pale katikati Aucho na Yannick Bangala wanaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa umiliki wa mpira kuliko Mukoko. Huyu Mukoko ni mzuri wakati timu haina mpira lakini timu ikiwa na mpira hana umiliki mzuri wa mpira.

Kitakachomrudisha Mukoko uwanjani ni kama mlinzi mmoja wa kati ataumia au atakuwa na kadi zitakazomuweka nje ya uwanja. Kama Bakari Mwamunyeto au Dickson Job mmoja akiumia basi Bangala anaweza kurudi nyuma na Mukoko akacheza na Aucho. Vinginevyo sioni nafasi ya Mukoko kikosini.

Mwingine ambaye ana wakati mgumu ni Gift Mauya. Huyu ni miongoni mwa mastaa ambao waliisaidia Yanga katika kipindi cha mpito kuelekea kuwa na timu nzuri. Inabidi ajifunze mambo mengi kwa akina Aucho. Kinachomuweka nje sio kwamba hana ubora, hapana, amepitwa ubora tu.

Hii changamoto kuna wakati ilimkuta Jonas Mkude pale Simba. Akapambana na kuwa kiungo pekee mzawa anayepata nafasi katika kikosi cha Simba. Gift ana changamoto hii na sio kukata tamaa. Akipata nafasi afanye kile ambacho wenzake wanafanya. Litakuwa jambo jema kwa timu ya taifa.

Kitu ambacho ni kizuri kwa Taifa kwa sasa ni namna ambavyo Fei Toto amejikuta bora zaidi baada ya kuwasili kwa akina Aucho. Kocha Mohamed Nabi amemsogeza mbele na kumbe baada ya kupoteza muda kwa miaka mingi akicheza chini Fei amejikuta akiwa bora akicheza eneo la mbele. Anafunga na anapiga pasi muhimu za mwisho.

Kitu kingine nilichogundua baada ya kumtazama Aucho ni Yanga huenda wasingepoteza mechi dhidi ya Rivers kama Aucho, Djuma Shabani na Fiston Meyelle wangekuwepo uwanjani. Lilikuwa kosa kubwa Yanga kuwakosa hawa watu.

Pia mechi yenyewe kama ingecheza katika tarehe hizi huenda Yanga wangefuzu. Kwa sasa Yanga wamekaa sawa baada ya kucheza mechi kadhaa za Ligi.

Zile mechi dhidi ya Rivers zilikuja mapema zaidi kwao huku wakiwa na maandalizi mabovu ya mwanzo wa msimu (pre season) baada ya wachezaji wao kusumbuliwa na Uviko wakiwa kambini nchini Morocco.