Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 11 08Article 487102

Maoni of Friday, 8 November 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

JICHO LA MWEWE: Kauli moja tu ya Magufuli itabadili Ligi Kuu

JICHO LA MWEWE: Kauli moja tu ya Magufuli itabadili Ligi Kuu

TUPO katika mwanzo mwingine wa ligi nyingine, katika msimu mwingine, wenye viwanja vibovu katika sehemu ya kuchezea kama ilivyokuwa katika misimu mingine ya nyuma. Unashangaa kama tupo makini kiasi gani.

Wimbo umekuwa ule ule kuhusu viwanja vya kuchezea soka la Tanzania. Ukienda uwanja wa Mkwakwani mchezaji hawezi kukokota mpira kwa uhuru walau hatua saba. Nenda Uwanja wa Jamhuri, Morogoro hadithi ni ile ile. Uwanja mgumu kama lami.

Ukienda Singida utashangaa sana. Halafu funga safari mpaka Arusha. Jiji la pili kwa ukubwa Tanzania. Jiji lenye pesa. Jiji lenye ng’ombe wengi. Jiji lenye madini. Jiji lenye kila kitu. Nenda katika uwanja wao mkubwa zaidi unaitwa Sheikh Amri Abeid. Niliona Simba wakicheza pale hivi karibuni walikuwa kama vile wanacheza katika zizi la ng’ombe.

Kabla ya hapo niliona Yanga wakicheza pale na AFC Leopards ya Kenya wakati wakijiandaa kucheza dhidi ya Township Rollers ya Botswana. Ilikuwa kama vile wanacheza katika matuta ya viazi. Hauwezi kuamini kama uwanja huo upo Arusha.

Kitu cha kushangaza hauwezi kupata jibu sahihi ni nani anahusika kuvifanya viwanja hivi kuwa na sehemu ya kuchezea bora kama ya Uwanja wa Taifa. Ukitaka kujua nani anahusika basi Rais wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli atoe kauli moja tu ya amri.

Magufuli aseme tu ‘Nataka viwanja vyote vya Ligi kuu vya Tanzania viwe na sehemu ya kuchezea kama Uwanja wa Taifa. Wahusika msipofanya hivyo basi Mkuu wa Mkoa niletee majina yao.’ Baada ya hapo ungeshangaa sana.

Kwanza tutawajua wahusika. Tutajua kama wanaopaswa kufanya hivyo ni CCM, Serikali, TFF, Bodi ya Ligi au wadhamini. Ghafla tutaanza kuona malori ya michanga yakifumua viwanja. Tutaanza kuona nyasi zikipandwa upya na kushindiliwa. Baada ya hapo kila kitu kitakaa sawa.

Kwa sasa utasikia sababu nyingi za kushindwa kutunza eneo la kuchezea la viwanja. Utasikia kuhusu ukosefu wa pesa. Magufuli akitoa amri utashangaa pesa zimetoka wapi. Utasikia ukosefu wa vifaa. Magufuli akisema utashangaa vifaa vilitoka wapi.

Nchi hii imejaa watu wanaopuuzia mambo. Ili mradi hakuna timu zilizowahi kugomea mechi kwa sababu ya ubovu wa eneo la kuchezea la uwanja basi maisha yanaendelea. Watu watalalamika kidogo kisha maisha yataendelea.

Hii ni nchi ya amri. Watu wengine wanaopuuzia mambo, kama hawa hapa wanaopaswa kututengenezea sehemu safi na salama kwa wachezaji wa Ligi Kuu kuchezea kiboko yao ni Magufuli tu. Akisema utashangaa jinsi uwajibikaji unavyojitokeza ghafla.

Kwa sasa kinachoendelea katika viwanja vyetu ni aibu. Majuzi nilikuwa Mombasa nikacheza katika uwanja wa nyumbani wa timu ya Bandari ya Mombasa unashangaa namna Wakenya wametuzidi katika suala hili la kawaida kabisa. Sehemu ya kuchezea ni safi na salama.

Leo ukitazama Azam TV kuna viwanja ni aibu kwa nchi. Unajiuliza, hata kutengeneza uwanja katika sehemu ya kuchezea tunahitaji msaada wa watu wa Marekani? Watu wa Vodacom na Azam Tv wanakubali vipi kuingiza pesa zao katika ligi yenye viwanja kama hivi?

Kupitia viwanja hivi tunashindwa kutengeneza falsafa ya mpira wetu. Makocha wengi wa kisasa waliojaa katika timu za Ligi kuu wangependa wachezaji wao waweke mpira chini. Watauweka mpira chini kwa viwanja vipi hasa? Wachezaji wanaishia kubutua. Kubutua ni njia salama ya kuufikisha mpira mbele.

Imefikiwa wakati sasa uwanja wa CCM Kirumba nao ni mbovu. Zamani ulikuwa unasifika kwa kuwa na sehemu nzuri ya kuchezea. Leo wapinzani wa Yanga wamepelekwa Mwanza kwa sababu Yanga walitaka kujivunia ubovu wa sehemu ya kuchezea.

Ukichunguza ni viwanja vichache tu ndivyo ambavyo vinaweza kuamua bingwa halali wa nchi. Kwa mfano, kama Simba na Yanga zingekuwa zinacheza katika viwanja vya mikoani kwa ligi nzima, si ajabu zingekuwa zinasimama maeneo ya katikati ya msimamo wa Ligi Kuu.

Walau wanapata nafuu kwa sababu mechi zao nyingi, ikiwemo zile za nyumbani na ugenini kwa baadhi ya timu kama Ruvu JKT na Azam huwa zinachezwa katika uwanja ambao unaweza kuamua timu bora ishinde mechi.

Kama viwanja vyote vya Ligi Kuu vikiwa katika kiwango cha uwanja wa Taifa nadhani Ligi Kuu ingekuwa yenye kusisimua zaidi. Nadhani soka lingekuwa la kuvutia zaidi. Rafiki zangu kina Kevin Yondani ambao wamezoea kubutua mbele wangeanza kuweka mpira nchini.

Kuwa na viwanja vibovu katika eneo la kuchezea ni uvivu wa Kitanzania tu. Rwanda wametupita. Kenya wametupita. Zambia wametupita.

Ni uvivu wetu na kushindwa kuheshimu ukweli kwamba mchezo wa soka ni maisha ya watu. Ni ajira za watu. Ni kiwanda kinachoweza kuzalisha mamilioni ya pesa ndani na nje ya uwanja.