Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 20Article 579946

Maoni of Monday, 20 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

JICHO LA MWEWE: Kuna kitu Himid Mao amewakamata Mafarao wa Misri

Nyota wa Tanzania Himd Mao Mkami Nyota wa Tanzania Himd Mao Mkami

Nitakuibia siri moja nzuri katika soka. Kipa wa Arsenal, Aaron Ramsdale ameshusha timu mbili za Ligi Kuu. Sidhani kusema kwamba ‘ameshusha’ ni neno zuri. Basi tunaweza kusema timu mbili za Ligi Kuu zilishuka huku yeye akiwa langoni. Uswahilini kwetu tunasema alishusha. Ni neno la kumkosea heshima kidogo.

Aliposhuka na timu yake ya kwanza Bournemouth alikwenda zake Sheffield United. Hapo pia alishuka. Ghafla akaibukia Arsenal. Wengi walilalamikia uhamisho wake lakini sasa ndiye mmoja kati ya wachezaji bora wa Ligi Kuu ya England. Ni mmoja kati ya wachezaji bora Arsenal pia.

Unajiuliza Sheffield waliona nini kwake kiasi cha kumchukua akiwa ametoka kuishusha Bournemouth daraja? Hapo hapo unajiuliza, Arsenal wameona nini kwake wakati aliishusha Sheffield daraja? Na unaweza kwenda mbali na kujiuliza kwamba waliona nini pia kwa kipa ambaye pia aliishusha Bournemouth?

Hadithi hii inamtokea mchezaji anayeitwa Himid Mao Mkami. Staa wetu wa Tanzania anayecheza Misri. Majuzi nilikuwa namtafakari Himid jinsi ambavyo amelikamata soka la Misri. Ndivyo inavyopaswa kuwa kwa wachezaji wetu. Kama kila mmoja akiweza kulikamata soka la nchi fulani iliyoendelea kisoka basi mambo yatakuwa mazuri kwetu.

Wengi tunamsahau Himid kwa sababu haitwi katika kikosi cha Stars lakini Himid ni mwanaume anayepambana sana Misri. Mara kadhaa nimewahi kuona Waarabu wa Misri wakianika takwimu zake za uwanjani. Zinavutia.

Kuna wakati jina lake lilijitokeza katika kikosi cha wiki cha Ligi Kuu ya Misri. Kumbuka jina linapotokea hapo basi Himid amefanya hivyo mbele ya mastaa wa klabu kama Pyramids, Al Ahly, Zamalek na nyingineZo. Sio kitu kidogo.

Wakati fulani Himid aliwahi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi. Sio kitu cha kawaida sana katika soka la Misri. Wametuacha mbali. Ligi yao ni ya kiushindani zaidi. Ukiona mchezaji ametoka Tanzania na amefanya hivyo basi lazima umuheshimu.

Himid alikutana na mkasa wa Ramsdale. Alipotua Misri kwa mara ya kwanza kukipiga klabu ya Petrojet bahati mbaya ikamkumba timu hiyo ikashuka daraja. Hata hivyo, kuna timu nyingine iliyotoka kupanda, ENPPI ikamchukua Himid.

Bahati mbaya tena ENPPI ikashuka dajara. Ikajitokeza timu ya Ghazel El Mahalla ikamchukua. Unadhani haya yote yanatokea kwa bahati mbaya? Hapana. Lazima kuna jambo. Kuna kitu ambacho Himid anawafanyia Mafarao na ndio maana anapata timu.

Lazima wanaoweka ofa mezani kwake wanajua kwamba Himid hakuwa miongoni mwa wachezaji walioshusha timu. Na ni kweli. Kwa tunaomfahamu Himid tunajua kwamba Himid ni shujaa. Himid ni Simba. Himid anaweza kichwa chake katika mguu wa mpinzani kwa dakika zote 90.

Himid ni miongoni mwa viungo wakabaji ambao kwa sasa wameanza kutoweka. Siku hizi tuna viungo wengi ambao wanaitwa Holding. Wale wanaoudhibiti mpira vema wakiwa katika maeneo yao. Himid ni wale wa ulinzi zaidi (Defensive Midfielders). Jamii ya kina Javier Mascherano.

Inaonekana katika soko lake wapo wachache pale Misri kiasi kwamba jina lake linaibuka kiurahisi katika timu za Ligi Kuu ya Misri. Kama wangekuwa wapo wengine na ushindani ungekuwa mkubwa si ajabu sasa hivi Himid angekuwa amerudi Chamazi. Hasa kwa taifa kama Misri ambalo limeweka idadi ya wachezaji wachache wa kigeni ndani ya kikosi.

Achilia mbali hilo unaweza pia kumsifu Himid kwa kuendelea kuwepo Misri kwa muda mrefu sasa. Wachezaji wetu huwa hawawezi kumudu kuwepo nje ya nchi kwa muda mrefu. Wana ule ugonjwa wa kupenda kuwepo nyumbani (Home sickness).

Ndani ya miezi michache tu mchezaji anaanza visingizio vingi na baadaye utamuona amerudi katika Ligi yetu ambayo anafahamu kwamba yeye ni staa. Unapoona mchezaji kama yeye anamudu kuwepo nje ya nchi kwa muda mrefu kama ilivyo kwa Simon Msuva na Morocco yake basi ujue kwamba anaweza kuwa mfano kwa mastaa wetu wengine.

Kwa ninavyoifahamu Misri, ile sio nchi ambayo itakupa starehe nyingi rahisi kama ilivyo kwa Tanzania. Lakini pia kuna ubaguzi dhidi ya mtu mweusi. Wachezaji wengi hawafurahishwi sana na maisha ya kawaida Misri na kinachowaweka katika nchi hiyo ni kusaka noti tu. Himid anastahili pongezi kwa hili.

Kwanini Himid haitwi katika kikosi cha Taifa Stars? Hili ni swali ambalo limeanza kujitokeza mara kwa mara pindi tunapopata habari njema za Himid. Ukweli ni kwamba inawezekana Himid sio aina ya mchezaji wa Kim Poulsen. Nililifahamu hilo mapema.

Tangu Kim Poulsen atue nchini sijawahi kumsikia akimuita Himid ingawa amekuwa akiita wachezaji wengi wa kigeni katika nyakati tofauti. Himid ni mchezaji wa shoka ambaye sio fundi sana. Yeye ni hodari zaidi katika kupora mipira na kuziba njia za adui.

Kim Poulsen anapenda zaidi wachezaji mafundi ambao wanatulia zaidi na mpira mguuni. Wachezaji wake ndio hawa kina Salum Aboubakar, Jonas Mkude, Novatus Dismas na wachache wengineo. Hata hivyo, nadhani hiyo sio sababu pekee ya Himid kutoitwa kikosini.

Kwa kadri ninavyofahamu ni kwamba wakati mwingine timu inahitaji uwiano ulio mzuri. Unahitaji wachezaji wa aina tofauti tofauti katika kikosi kwa sababu sio kila siku utahitaji kucheza mchezo wa aina moja. Kuna nyakati ambazo utahitaji ujilinde sana na utamuhitaji Himid.

Wakati mwingine itategemea mechi yenyewe. Unaweza kuongoza kwa idadi kadhaa ya mabao na mpinzani akaanza kukuchachafya vilivyo. Utahitaji mchezaji wa aina ya Himid kwa ajili ya kupora mipira na kuwalinda wale walinzi wanne wa nyuma. Ukweli ni kwamba Himid pia anahitajika katika kikosi cha Taifa Stars.