Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 09Article 569341

Maoni of Tuesday, 9 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

JICHO LA MWEWE: Manula, Diarra tuamini namba au tunachokiona

Walinda milango Simba na Yanga Walinda milango Simba na Yanga

Aishi Manula hajafungwa bao lolote mpaka sasa. Yupo salama katika lango la Simba. Upande wa pili kwa wapinzani wao, kipa wa Mali, Djigui Diarra amefungwa bao moja tu na mchezaji anayeitwa Shaaban Msala wa Ruvu Shooting. Tujichangamshe na mijadala.

Nani kipa bora? Siwazungumzii wao ambao mmoja amefungwa bao moja, mwingine hajafungwa kabisa. Nazungumzia mjadala unaoendelea duniani kote. Tuamini katika namba au tuamini kile tunachokiona kikitokea uwanjani bila ya kujali mambo ya namba? Ni mjadala unaosisimua.

Binafsi ningeweza kuwaweka wote kando kisha nikamchagua kipa wa Ruvu Shooting, Mohamed Makaka. Ameokoa michomo mingi kuliko hawa makipa wa Simba na Yanga. Pambano dhidi ya Yanga lilikuwa moja kati ya mifano. Aliruhusu mabao matatu lakini aliokoa hatari nyingi kuliko Diarra.

Ni kama Jonathan Nahimana wa Namungo alivyookoa hatari nyingi dhidi ya Simba kuliko vile Aishi Manula alivyofanya katika lango lake. Na wote hawa wawili, Makaka na Nahimana wamefanya hivyo zaidi katika mechi zilizopita kuliko Aishi na Diarra.

Hapa ndipo unapotokea mzozo katika soka la kisasa ambalo wakati mwingine linaamuliwa zaidi na namba.

Tuhame hapo twende eneo jingine. Hamis Dilunga alichaguliwa mchezaji bora wa Simba mwezi uliopita. Dilunga hajafunga wala kupika bao lolote katika msimu huu. Mashabiki wa Simba wameona anafaa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi. Nafasi yake ni kiungo mshambuliaji.

Kwa nini wameona hivyo? Wameamini walichokiona kuliko kuamini katika namba. Wanamwona Dilunga anautawala mpira. Wanamwona Dilunga anawasaidia katika mashambulizi. Wanamwona Dilunga anafanya kazi nyingi kuliko wachezaji wengine walionao. Huu ni ukweli mchungu kwa wachezaji ambao labda wamefunga kuliko Dilunga au kupiga mabao kuliko Dilunga.

Achana na Dilunga. Pale Yanga kuna viungo wanaimbwa sana. Khalid Aucho na Yannick Bangala. Hakuna ambaye amefunga wala kupika pasi ya bao. Mashabiki wanawaimba sio kwa sababu ya Namba bali kwa sababu ya wanachokiona uwanjani

Bangala na Aucho wameituliza timu. Wanatawala eneo la kiungo katika kila mechi ambayo Yanga inacheza msimu huu huku wao wakiwa uwanjani. Inavyoonekana mbele ya safari Yanga itakuwa na wakati mgumu kama Bangala na Aucho watakosekana uwanjani.

Subiri kidogo. Wakati Aucho na Bangala wakiwa hawana bao wala pasi ya mwisho, mmoja kati ya wachezaji ambao wameathirika na ujio wao, Tonombe Mukoko ana bao moja. Alifunga dhidi ya ya Ruvu Shooting akihitimisha ushindi mnono wa mabao 3-1 wa Yanga.

Waulize leo Wanayanga kama watakubali mchezaji mmoja kati ya Aucho na Bangala akae nje katika mechi ijayo kwa ajili ya kumpisha Mukoko, hakuna ambaye atakubali. Haya ndio maisha ya namba dhidi ya hali halisi. Maisha ambayo yamekuwa yakisumbua hata wazungu.

Wakati mwingine pia wazungu huwa wanasumbuka na suala la mataji achilia mbali namba. Namna ambavyo kuna wachezaji wengi mahiri wanakosa kupewa tuzo kwa sababu ya ukosefu wa mataji lakini ukweli unaonyesha kwamba wao ni bora.

Kuna wachezaji ambao wamewahi kukosa tuzo hizi wakiwa wametoka kushinda mataji mengi halafu wale ambao hawakushinda mataji wakatwaa tuzo. Nadhani wapigakura waliangalia hali halisi kuliko namba zilizopo mezani. Huwa inachanganya sana.

Mfano ni mwaka 2010. Wesley Sneijder alitoka kushinda ubingwa wa Ulaya, akafika fainali za kombe la dunia lakini hakuingia katika tatu bora ya wachezaji wanaowania tuzo ya kuwania mwanasoka bora wa dunia. Alishinda Lionel Messi ambaye msimu huo alitoka kapa.

Swali hapo lilijileta kama kitu cha msingi kilikuwa ni mataji au uwezo wa mchezaji. Achana hata na Sneijder, rafiki wa Messi, Andres Iniesta ambaye alikuwa katika ubora wake huku akitwaa kombe la dunia mwaka huo alikosa tuzo hiyo. Iniesta pia alikuwa amefunga bao pambano la fainali dhidi ya Uholanzi akiwa amevaa jezi ya Hispania.

Tukirudi tena nchini nadhani mashabiki waanze kujiingiza katika mjadala huu. Mchezaji bora ni yupi? Yule unayemwona kwa macho yake au yule ambaye utaletewa takwimu zake mezani. Siamini kama kipa aliyefungwa bao moja au ambaye hajafungwa anaweza kuwa bora kuliko wengineo ambao wapo katika timu zinazoshambuliwa zaidi.

Sio kwamba Aishi na Diarra ni makipa wabovu lakini swali la kutoruhusu mabao mengi ni mjadala mkubwa kutokana na namna ambavyo vikosi vyao vinatumia muda mwingi kukaa na mpira na kushambulia zaidi kuliko wao wanavyofanyiwa. Ni mjadala wa kidunia zaidi.

Tunapopanga vikosi vyetu vya wiki au mwezi katika mitandao ya kijamii ambako mpira umehamia huko siku hizi ni muhimu kama tukiendelea kukumbushana umuhimu wa namba na uhalisia. Mashabiki wetu wengi pamoja na wachambuzi wameanza kuingia katika suala la namba pengine kuliko uhalisia.

Wakati fulani kipa wa zamani wa Barcelona, Victor Valdes aliwahi kutaka mshahara mkubwa klabuni hapo lakini Rais wa Barcelona wa wakati huo, Johan Laporta ambaye kwa sasa amerudi tena katika nafasi hiyo alimtolea nje Valdes akiamini kipa huyo hakuwa na kazi kubwa ya kufa langoni kwa sababu timu yao ilikuwa na utawala wa mpira kwa muda mrefu.

Binafsi kuna wakati nitapenda kubakia katika uhalisia zaidi kuliko namba. Wakati mwingine namba zinadanganya kidogo. Ni kama vile ambavyo unaweza kuangalia timu ambayo imepiga idadi kubwa ya pasi lakini ambazo hazikuwa na madhara.Kwa mfano, Yanga kwa sasa wapo katika ubora wao huku wakipiga pasi nyingi. Wanaweza kupiga pasi nyingi kuliko Simba ya akina Clatous Chama lakini naanza kuona Yanga wanapiga pasi nyingi nyuma na katikati kuliko eneo la mbele ambalo Simba walikuwa wanapiga pasi nyingi na kutengeneza nafasi nyingi zaidi.

Mjadala upo wazi lakini ni mjadala ambao unaisumbua dunia. Hatujui sana kipi ambacho kinaamua ubora wa mchezaji au mechi au ubora wa timu fulani. Ni namba au hali halisi? Nafungua mjadala.