Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 16Article 571711

Maoni of Tuesday, 16 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

JICHO LA MWEWE: Ndoto ya Tshabalala kumkaba Mbappe Qatar ilivyoyeyuka

Beki wa Stars, Mohammed Hussein Beki wa Stars, Mohammed Hussein

Kwamba Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ angemkaba Kylian Mbappe katika michuano ya Kombe la Dunia 2022 pale Qatar ilikuwa ni ndoto iliyokuja ghafla kama ambavyo imeondoka. Taifa Stars hawana tena nafasi ya kusogea kwenda Qatar. Ilikuwa ndoto ya kushangaza sana.

Tulianza kuiota ghafla baada ya Stars kutoka sare ugenini dhidi ya DR Congo pale Lubumbashi. Halafu ikafifia wakati tulipofungwa nyumbani na Benin. Ghafla ndoto ikaibuka tena wakati tulipowachapa Benin ugenini. Ilikuwa ndoto yenye mawimbi mengi.

Kuanzia hapo wanasiasa wakaona wasiachwe nyuma. Wakaidakia ndoto juu juu kama kawaida yao huku wakinong’onezana wakisema; “mzaha mzaha huenda wakaenda kweli hawa tukaachwa nyuma tukakosa sifa”. Kufikia hapo wanasiasa wakaidaka ndoto kikamilifu na kujaribu kuifanyia kazi.

Hatimaye tumeshindwa. Baada ya kupoteza pambano letu dhidi ya DR Congo ndoto imekufa. Wanasiasa kwa sasa watatawanyika mpaka tutakapotengeneza ndoto nyingine kama hii. Kamwe hatutatafakari ndoto yetu ilikwama wapi. Hii ndio hali halisi.

Ambacho wanasiasa na wengine hawaelewi ni ukweli kwamba ndoto hii ya Stars kwenda Qatar haikuwa na misingi imara na tulijua ilikotoka. Ilikuwa ni ndoto ambayo ilitengenezwa katika namna ambavyo Afrika tulikuwa na mfumo rahisi katika hatua ya makundi.

Kundi la Stars lilikuwa rahisi kwa mujibu wa makundi haya. Hakukuwa na mbabe wowote kutoka Afrika Magharibi na Benin sio miongoni mwa timu babe Afrika Magharibi. Zamani tungewekewa mbabe mmoja kutoka Magharibi na mwingine kutoka Kaskazini. Tusingethubutu kuiota ndoto hii.

Mfumo wa sasa ulikuwa rahisi na kwa mzaha mzaha tu Stars angeweza kujikuta katika mechi mbili za mtoano kwenda Kombe la Dunia. Kwa maajabu ya Mungu labda tunapangwa kucheza na Tunisia. Tunashinda mabao mawili nyumbani kisha tunafungwa moja ugenini. Tunapita. Haya tunaenda Kombe la Dunia kufanya nini?

Bila kupepesa macho wengine tulikuwa tunaogopa hili kutoka. Kiasi mioyo ilitamani, kiasi ilisita. Kombe la Dunia ni viwango vya juu kabisa. Kama Afcon pale Misri tulionyesha kubabaisha, vipi kuhusu Kombe la Dunia Qatar. Tshabalala akabane na Lionel Messi? Dickson Job akabane na Cristiano Ronaldo? Inatia simanzi kufikiria.

Hata hivyo, Wacongo wamefanya kazi nzuri ya kutukumbusha kwamba tusikurupuke. Wao wenyewe wana wachezaji wengi Ulaya, lakini hawajawahi kujaribia kwenda Kombe la Dunia tangu mwaka 1974. Vipi kuhusu Tanzania? Sawa mechi ya kwanza tulitoka nao sare Lubumbashi lakini ilichangiwa pia na mzaha mwingi walioufanya kuelekea mechi hiyo wakaichukulia poa.

Walipokuja Temeke walitukumbusha kwamba wao ni kiwango tofauti na sisi. Lakini kama wao ni viwango tofauti na sisi, vipi tujaribu kufikiria kucheza mechi ya mtoano na Algeria au Nigeria kisha tukacheze na kina Lionel Messi na Argentina yake? Tujitafakari na tusikurupuke na ndoto hizi. Kuna mambo ya kufikiria.

Ebu tuifikirie Ligi yetu. Huwa tunapiga soga kwamba tuna Ligi nzuri ni kwa sababu ya Simba, Yanga na Azam. Wengine wapo hoi. Na hawa wakubwa wenyewe wanategemea zaidi wachezaji wanaocheza nje kwa sababu wa ndani wamefunikwa.

Simba ingefika mbali michuano ya kimataifa bila Luis Miquissone na Clatous Chama? Hapana. Hivyo kumbe tunategemea wachezaji wa ndani ambao hata hivyo sio roho sana katika klabu zetu kubwa kuliko wachezaji wa nje. Itazame Yanga ya leo. Kina Gift Mauya wameanza kukaa benchi na matokeo yake tunawaimba kina Yannick Bangala na Khalid Aucho.

Bado ni kichekesho kusema tutatumia wachezaji wetu wa ndani kucheza Kombe la Dunia. Labda kina Misri na Afrika Kusini wanaweza kufanya hivyo. Sio sisi. Ligi yetu siamini kama ipo tayari kuzalisha wachezaji wanaoweza kuipigania Afrika katika Kombe la Dunia. Tunazungumzia kuhusu kuiwakilisha Afrika na sio Tanzania pekee.

Nini tufanye? Tuzalishe kina Mbwana Samatta wengi wanaofanya vema Ulaya. Tuendelee kuzalisha kina Simon Msuva wanaotamba katika klabu kubwa ndani ya Afrika. Siamini katika Ligi yetu kwa sasa na kama tunataka kuiamini ligi yetu tutasubiri sana.

TFF ya sasa inapambana sana kuhakikisha timu zetu za vijana zinafanya vizuri. Vijana wana vipaji vizuri. Baada ya hapo nani anavipokea hivi vipaji? Ni kipaji cha Kelvin John tu ndicho ambacho kinaonekana kwenda katika njia sasa. Fikiria kama tungekuwa na vijana kama yeye 20 tu barani Ulaya.

Tatizo klabu zetu kubwa nazo zinajiona kuwa kwa sasa zinastahili kuwa na wachezaji wazuri zaidi kuliko kuwafanyia biashara. Hao hao wachache huwa hawauzwi. Mashabiki hawataki na viongozi hawataki. Mpira sio biashara. Hata hao wageni kina Chama waliouzwa bado viongozi wanalaumiwa.

Hapo hapo wanasiasa wasisahau tuna matatizo mengi, huku chini kuliko ahadi za ghafla wanapoona ndoto ina mwelekeo. Viwanja vyetu ni vibovu hasa katika maeneo ya kuchezea. Nani anajali? Nani anahusika? Wanaohusika ni wanasiasa ambao ikifika hatua hii wanakuwa na jicho la makengeza.

Kuna mambo mengi ya kufanya kabla ya kufikiria Kombe la Dunia. Hata kama tungeenda Kombe la Dunia tungetia aibu iliyopitiliza. Kuna mambo mengi ya kuzingatia. Mambo mengi ya msingi na tusidhani Kombe la Dunia tunaweza kwenda kwa hamasa na michango ya ghafla ghafla.

Tunapaswa kutawala michuano ya mataifa ya Afrika kabla ya kila kitu. Tupate uzoefu wa kwenda huko mara nyingi na kusogea mbele mara nyingi. Unawezaje kuota Kombe la Dunia wakati Afcon umeshiriki mara mbili, tena tu mbinde? Tujaribu kuwa wa kweli tu! Lazima tujipange kwelikweli.