Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2022 01 11Article 584941

Maoni of Tuesday, 11 January 2022

Columnist: Mwanaspoti

JICHO LA MWEWE: Ni ngumu wachezaji wa majaribio kutoboa Tanzania

Etop David Udoh Etop David Udoh

Miongoni mwa vitu vigumu katika soka la hapa duniani ni pale mchezaji anapoamua kufunga safari kwenda katika nchi inayoitwa Tanzania, kufanya majaribio katika klabu kubwa mbili. Simba na Yanga. Ana nafasi ndogo ya kufuzu majaribio.

Pale Zanzibar kuna mastaa watatu wanafanya majaribio Simba. Mmoja kutoka Sudan, Sharaf Shiboub. Mwingine ni Cheick Ahmed Tenena Moukoro kutoka Ivory Coast, halafu kuna Udoh Etop kutoka Nigeria. Katika siku ya kwanza ambayo utakanyaga katika mechi mashabiki wanakusubiri kwa hamu.

Wanakusubiri kwa hamu kuona ‚“unajua au haujui mpira,” Lakini wanafanya hivyo kwa vigezo vyao. Sio vigezo vya kocha wale benchi lake la ufundi. Hata viongozi wanasubiri hilo kwa vigezo vyao, sio kwa vigezo vya kocha wala benchi la ufundi.

Kigezo cha kwanza ni uwezo wa kuuchezea mpira. Kupiga kanzu maridadi, kupiga chenga, tobo na vingine ambavyo vipo nje ya mpira wa dunia hii. Hatujui tunataka nini kwa mchezaji. Kocha anaweza kujua anachotaka, lakini sisi wengine hatufahamu.

Inawezekana kocha anataka kiungo mwenye akili za kuziba njia, kiungo ambaye anaachia moja na kuanzisha mashambulizi kwa haraka. Kiungo ambaye anajua namna gani ya kuwa eneo sahihi katika wakati sahihi. Wazungu wanaita ‘tactical awareness’. Unaweza kuwa na mchezaji ana kipaji maridhawa, lakini hana tactical awareness.

Kuna mambo mengi. Kocha na watu wake wa benchi la ufundi wanaweza kumuona mchezaji ana vitu hivyo, lakini mashabiki na viongozi wa kawaida wasione kwa sababu mchezaji husika hapigi chenga sana na wala mbwembwe sana. Matokeo yake mchezaji ananyimwa mkataba.

Lakini hapo hapo kuna mchezaji anaweza kuwa wa uhakika. Bahati mbaya inamkuta anapojikuta yupo katika nchi mpya, watu wapya, mazingira mapya, chakula kipya, hali ya hewa mpya, kila kitu kipya. Anahitaji muda wa kuanza kuzoea kabla ya kuonyesha makali yake. Makali yanaweza kuwepo, lakini bado anahitaji muda.

Nawajua wachezaji lukuki wa kigeni waliotamba ambao wangeweza kunyimwa mkataba kama wangekuja nchini kwa majaribio. Mfano rahisi ni huyu Thadeo Lwanga. Alikunja mkataba wake akaanza kuichezea Simba katika michuano ya Mapinduzi mwaka jana.

Alianza kwa kuonekana kuwa mchezaji wa kawaida. Watu wa Simba wakaanza kuulizana kama wamepigwa. Kitu kibaya zaidi ni pale mashabiki wa watani na viongozi wao wanapoanza kuwatania kuhusu mchezaji husika.

Bahati nzuri Lwanga alikuwa na mkataba. Taratibu akaanza kukunjua makucha yake. Kadri alivyoendelea kuzoea ndivyo alivyoonyesha makali yake. Baadaye akawa tegemeo kubwa klabuni. Wachezaji wengine wanahitaji kitu kama hiki.

Tulijua lini umuhimu wa kiungo Mbrazil Fraga. Baadaye sana. Kama angekuja kwa majaribio sidhani kama angefaulu majaribio yetu. Bahati nzuri alishakuwa na mkataba mkononi. Umuhimu wake ulikuja kuonekana baadaye.

Donaldo Ngoma alipotua Yanga alionekana mshambuliaji wa kawaida. Kuna mashabiki walikuwa wanamkebehi kwa kumlinganisha na mmoja ya washambuliaji wa zamani wa Yanga waliofeli klabuni, Idd Mbaga. Walidai hawaoni tofauti ya Ngoma na Mbaga.

Baadaye Ngoma aliibuka kuwa tishio la nchi. Nadhani ni baada ya mazoea. Katika kipindi kile ambacho baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwa wanamfananisha na Mbaga, kama Ngoma angekuwa katika majaribio viongozi wangeachana naye.

Kuna wachezaji kadri wanavyozoea ndivyo wanavyoibuka kuwa imara zaidi. Hata Jose Luis Miquissone, ingawa Simba iliona kipaji chake maridhawa akiwa na UD Songo, lakini alipokuja alianzia kwa gia ya chini na baadhi ya mashabiki wakimfananisha na Shiza Kichuya.

Kama angekuwa amekuja kwa majaribio si ajabu wengine wangeshauriana wamkate jina lake. Bahati yake alikuwa na mkataba kwapani akaanza kung’ara taratibu. Huu ndio ugumu wa mpira wetu. Baadaye akaibuka kuwa staa mkubwa.

Lakini Yanga majuzi walileta mchezaji mwingine Mmakonde kutoka Msumbiji. Jimmy Julio Ukonde. Kwa macho yangu yule ni mchezaji hasa, lakini alihitaji muda. Na kama angekutana na mafundi waliokuja Yanga baadaye kina Fiston Mayele, Shaban Djuma, Jesus Moloko na wengineo si ajabu angekuwa bora zaidi.

Hata hivyo, Yanga walimuweka katika majaribio na wachezaji wa kawaida, kisha naye akaonekana wa kawaida kwa vile timu ilikuwa haichezi vizuri. Hata hivyo, umiliki wake wa mipira ulikuwa wa kiwango cha juu. Alikuwa na vitu miguuni. Bahati mbaya alikuja kwa majaribio.

Tunashindwa kuelewa sayansi ya mpira. Kitu cha msingi zaidi kwa sasa ni kwa viongozi kujikita zaidi katika kutanua wigo wa kufanya skauti wawe na uhakika na mchezaji wanayemchukua. Pindi wanapomchukua wasiwe na mambo ya majaribio.

Katika soka la Tanzania mchezaji mzuri anaweza kukatiliwa na majaribio kwa kucheza pambano kwa dakika 15 tu akaonekana hafai. Ni bora angetazamwa moja kwa moja na kisha akapewa mkataba. Hata kama angeharibu katika mechi ya kwanza, lakini unajua kitu cha kutazamia pindi mchezaji atakapokaa sawa.

Barani Ulaya majaribio mengi huwa yanafanywa kwa wachezaji makinda. Hata Michael Essien amewahi kwenda mazoezini Manchester United akiwa kinda. Wanachoangalia ni nafasi ya kukuchukua na kukuweka katika timu ya vijana kuelekea katika kupambania nafasi ya kucheza timu kubwa.

Wanaangalia mengi uwanjani lakini zaidi maamuzi yao yataangalia zaidi kama litakuwa jambo jema kufanya uwekezaji kwa mchezaji husika kwa ajili ya matumizi ya baadaye, au kama ataweza kuuzika kwenda kwingineko umri ukifika.

Wengine wanaofanyiwa majaribio ni wachezaji ambao tayari wameshaonyesha uwezo wao mahala, lakini wakajikuta hawana timu kwa kipindi kirefu kidogo kutokana na majeraha au kumalizika kwa mikataba yao kwingineko.

Sisi tunawafanyia majaribio wachezaji ambao wametoka katika timu na walikuwa wanacheza. Kwanini hatukuchukua maamuzi mapema na kwenda kuwatazama wakicheza ili tujiridhishe na viwango vyao?