Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 11Article 537193

xxxxxxxxxxx of Tuesday, 11 May 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

JICHO LA MWEWE: Yanga ilivyowatia adabu wanasiasa wanaoingilia soka

KAMA mzaha juzi. Mechi haikuchezwa. Yanga walipasha misuli yao moto. Wakajipanga uwanjani. Simba hawakuwepo. Yanga wakarudi katika vyumba vya kubadilishia nguo wakachukua mabegi yao. Wakaenda katika basi wakaondoka zao.

Mechi haikuwepo. Kisa? Saa nane, ikiwa ni saa tatu kabla ya mechi kuanza ilikuja taarifa kwamba pambano limesogezwa mbele mpaka saa moja. Ilikuwa taarifa fupi iliyosambaa haraka mitandaoni. Watu wa Yanga na wale wa Simba hawakupenda. Hasa wale ambao walikuwa uwanjani.

Yanga hawakuwa tayari tena kucheza mechi. Unaweza kusema kwamba wamewaogopa Simba kwa sababu watani wao wana kikosi kikali na nje ya habari kwamba mechi za watani wa jadi huwa hazitabiriki bado Simba walikuwa wamepewa asilimia kubwa ya kushinda mechi.

Chochote unachoweza kusema kuhusu Yanga kuogopa mechi ukweli ni kwamba kanuni ilikuwa upande wao. Haijashangaza kuona TFF wamekuwa wapole kwa Yanga kiasi cha kudai kwamba ‘pambano limehairishwa’. Naona wazi kwamba hawajakasirika kwa sababu wangeweza kutangaza faini kali kwa Yanga pamoja kuipoka pointi tatu.

TFF wanajua kwamba Yanga wamekwenda katika kanuni ambayo inasema klabu zitataarifiwa mabadiliko ya muda saa 24 kabla ya mechi. Kuna wanaosema kwamba kwanini Yanga iliwahi kucheza na Azam na Biashara Shinyanga huku mabadiliko ya muda yakija muda mchache kabla ya pambano kuanza.

Wanaosema hivyo wanasahau kwamba Yanga walitumia busara tu kucheza mechi hizo. Na hata Azam na Biashara pia walitumia busara. Juzi Yanga hawakutaka kutumia busara waliamua kutumia kanuni. Wakati mwingi wa maisha yetu busara na hekima huwa zinavunja kanuni.

Tunarudi katika maswali ya msingi. Nani aliahirisha mechi? Nadhani kutakuwa na wahuni wawili watatu waliotumia chombo cha serikali kinachoitwa Wizara kwa ajili ya kuahirisha mechi hii. tunaruhusiwa kuwaita wahuni kwa sababu hawakutoa sababu yoyote ile.

Na kwa sababu hawakutoa sababu yoyote mbele ya maelfu ya watu waliolipa viingilio au wale mamilioni waliokuwa nyumbani kutazama mechi hii basi tunaweza kusema huenda wahuni walikuwa ni washkaji waliokuwa wanasubiri wapenzi wao watoke saluni ndipo waje uwanjani.

Unawezaje kuahirisha mechi kama ile bila ya sababu yoyote? Na hapa ndipo tunapojikumbusha ni kwanini Fifa haitaki serikali iingilie michezo. Tunaposema Wizara tunamaanisha serikali. Na hapa serikali ilikuwa imeziingilia dakika 90 za pambano la juzi na wakubwa wenyewe wa mchezo huu waliopo Uswisi wakisikia watakasirika sana. Ni wazi kwamba TFF ilipokea kile kitu kinachoitwa ‘Maagizo kutoka juu’. Kitu hiki kilitawala sana katika utawala wa awamu ya tano. Kuna watu bado wana mning’inio (hangover) wa ubabe huu. Naweza kuona kabisa TFF walikuwa wamechukia maagizo haya lakini hawakuwa na namna.

Ungeweza kuona wazi kwamba taarifa ya TFF ilijikosha mapema na ndio maana wakaweza wazi kwamba mechi ilikuwa imeahirishwa kutokana na maagizo ya Wizara. Kuna maswali mawili ya kujiuliza. Je, TFF waliwashauri Wizara kwamba kanuni zao zilikuwa nje ya muda kusogeza pambano hilo mbele?

Inawezekana waliwashauri lakini wakubwa wa Wizara wakadharau. Lakini hapo hapo tujiulize swali jingine. Je, TFF walifanya jitihada zozote za kufanya kikao cha haraka na watu wa Simba na Yanga kwa ajili ya kufikisha ujumbe kutoka Wizarani au walitoa agizo tu ambalo walitaka litekelezwe bila ya kujua hisia za timu hizi, hasa Yanga?

Wakati haya yote yakitokea uhusiano wa Yanga na TFF ni mbovu. Yanga wana hisia kwamba TFF ni mali ya Simba. Yanga wanaamini kwamba Simba wanaipelekesha TFF wanavyotaka na si ajabu mabadiliko haya ya muda yalikuja kwa shinikizo kutoka Simba.

Uhusiano huu mbovu baina ya wawili hawa ndio ambao umeharibu mechi zaidi. kwanini Simba hawakuonekana kuchukizwa na mabadiliko ya muda? Ni kitu ambacho watu wa Yanga wakaamua tu kuunganisha mistari na kujikuta wakiamini kwamba Simba na TFF lao moja.

Mwisho wa siku ni kwamba hatukuwa na mechi ya soka. Mtu anayejilaumu zaidi ni yule aliyetoa wazo la mechi hii kusogezwa mbele. laiti kama angejua ambacho kingetokea nadhani asingefanya alichofanya.

Na hapa ndipo unapojiuliza, ni kweli Yanga hawakutaka kucheza mechi? Mbona walikuja uwanjani na walikuwa tayari kucheza saa kumi na moja. Mbona kabla ya hapo hawakuwa na kisingizio kingine kama vile hofu ya waamuzi na hujuma? Aliyebadilisha muda atakuwa anajilaumu sana.

Na sasa umefika wakati wa kutenganisha mpira na siasa. Yanga wametufundisha kwamba mpira na siasa ni vitu tofauti. Lazima sasa wanasiasa wajifunze jambo hapa. Kama hawatajifunza hapa basi hawatajifunza tena. Wenzetu kule nje taasisi za serikali ambazo zinaweza kuingilia mabadiliko ya ratiba za mechi ni watu wa ulinzi na usalama pamoja na watu wa Mamlaka ya hali ya hewa. Ni kama ambavyo majuzi watu wa usalama pale Manchester walivunja mechi ya Manchester United dhidi ya Liverpool Old Trafford kwa sababu za kiusalama.

Mara kibao tumeona mechi za Ulaya zikiharishiwa kwa sababu usalama au uchelewaji wa baadhi ya mashabiki linapokuja suala la kuingia uwanjani. Kwa mfano, juzi Yanga wangeambiwa mechi imesogezwa mbele kwa sababu mashabiki wengi wamekwama barabarani sidhani kama wangeondoka.

Lakini hivyo hivyo kwa hali ya hewa. Ulaya kuna mechi nyingi zinasogezwa mbele kwa sababu ya utabiri wa hali fulani mbaya ya hewa au umwagikaji mkubwa wa barafu. Ni kitu cha kawaida tofauti na ile barua ya TFF ambayo tumeiona juzi. Hakukuwa na sababu. Wanasiasa waachane na soka. Na Yanga imewapa fundisho kubwa. Nani atarudisha pesa za tiketi za mashabiki? Vipi wale mashabiki waliotoka mikoani?

Join our Newsletter