Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 24Article 553378

Maoni of Tuesday, 24 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

JICHO LA MWEWE: Yanga ninayoitazama ikijiandaa Marakech

JICHO LA MWEWE: Yanga ninayoitazama ikijiandaa Marakech JICHO LA MWEWE: Yanga ninayoitazama ikijiandaa Marakech

HAKUNA kazi ngumu kama kwenda katika kambi ya bondia anayejiandaa na pambano kali. Ni rahisi kutabiri kwamba atashinda. Analikung’uta ‘punching bag’ kwa hasira na haraka haraka. Unawaza kwamba anakwenda kuua mtu ulingoni hata kama mpinzani wake ni Mike ‘Iron’ Tyson.

Ni kazi ngumu kutabiri kitakachotokea kwa sababu unaona mazoezi ya upande mmoja. Unaona bondia akirusha ngumi bila ya kurushiwa ngumi. Unabaki kuwaza ambacho kinaweza kutokea. Mwisho wa siku unamuachia Mungu na kuamini kwamba ulingo utaamua.

Ndicho ninachokiona Marrakech katika kambi ya Yanga. Yanga wapo hapa mji fulani hivi wa starehe zaidi Morocco. Watalii wengi kutoka kila kando ya dunia wapo hapa wakila raha. Yanga wamekuja hapa wakiwa sio miongoni mwa watalii. Wanafanya mazoezi asubuhi na jioni kujiweka fiti na michuano mbalimbali inayowakabili usoni.

Tatizo nawaangalia wao tu na ubora wao binafsi. Sijui maadui wengine wanaendeleaje. Lakini kwa ninachokiona hapa huenda Yanga wakawa bora kuliko Yanga yoyote waliyowahi kuwa nayo ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kwa mfano, tuanzie katika tatizo lao la msingi misimu michache iliyopita. Washambuliaji. Hapa tuna washambuliaji watatu wa kati. Fiston Mayele, Herritier Makambo na Yusuph Athuman ambaye amechukuliwa kutoka Biashara Shinyanga.

Wote hawa wanang’aa mazoezini. Makambo ananifurahisha kwa aina ya mabao anayofunga. Hachagui mguu. Amefunga mabao mengi hapa mazoezini Marrakech. Amenikumbusha kwanini Yanga walihaha kuziba pengo lake tangu alipoondoka mpaka sasa amelazimika kurudi.

Kuna Mayele. Anaonekana kuwa bora kuliko Makambo katika mbinu. Anajua kugeuka haraka, anajua muda gani apige muda gani asipige. Anajua kufinya kwa haraka. Anafunga mabao ambayo yanatuacha mdomo wazi. Hatujui kama atakuwa hivi hivi katika Ligi.

Yusuph ni kijana mdogo mwenye umbo refu. Anajua kukaa na mpira, anajua kufunga lakini yuko bora zaidi katika mikimbio yake. Upinzani mbele yake ni mkubwa lakini akipata nafasi atakuwa bora zaidi na ataimarika zaidi kama akiamua kujifunza na kuzingatia.

Wote tunamfahamu mshambuliaji mwingine aliyepo hapa, Yacouba Songne. Tunafahamu ubora wake. Na tunafahamu namna alivyomaliza Ligi vema. Tatizo ni kwamba tupo mazoezini. Hatujui kama watapata kiwango kile kile cha upinzani ambacho wanapewa na walinzi wao mazoezini.

Mazoezi ni mazoezi na mechi ni mechi. Hata hivyo kuna dalili kwamba Yanga watakuwa wamepata safu nzuri ya ushambuliaji kutokana na ubora unaoonyeshwa na hawa akina Makambo mazoezini. Sikuwahi kwenda katika mazoezi ya akina Michael Sarpong lakini kwa kile ambacho nilikuwa nakiona katika mechi zao ni tofauti kabisa na hiki ninachokiona katika mazoezi ya Yanga.

Yanga wana wachezaji wa pembeni wenye kasi. Kina Jesus Maloko na Dickson Ambundo. Wote ni mahiri na wataziba vema pengo la Tuisila Kisinda. Uzuri ni kwamba hawatashambulia peke yao kwa sababu Yanga wamechukua mabeki wa kushambulia. Djuma Shaban kulia na David Bryson kushoto.

Uzuri wa suala la kushambulia hapo Yanga lina mambo mawili. Kwanza wameongeza machaguo yenye ubora. Benchi lao litakuwa na watu wenye afya. Ina maana Makambo anaweza kutokea benchi halafu Mayele akaanza. Yacouba anaweza kuanzia kushoto, halafu baadae nafasi yake ikachukuliwa na Ambundo.

Jambo la pili ni namna pia ambavyo kocha wao, Nasreddine Nabi anavyotaka timu ishambulie. Mazoezi mengi ya Nabi ni ya ushambuliaji. Kutokea pembeni na pia katikati. Juzi nililazimika kumuuliza kwamba kwanini kila aina ya mazoezi ya Yanga ni kushambulia, akanijibu kwa kifupi tu kwamba “Yanga ni timu kubwa”.

Katika eneo la kiungo juzi aliwasili kambini mchezaji anayeitwa Khalid Aucho. Mrefu, ana misuli na anajiamini. Katikati pia Yanga wana ubora na machaguo bora. Wana Aucho, Gift Mauya aliyemaliza msimu akiwa bora, Tonombe Mukoko, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Saido Ntibanzokonza. Hapo wote ni bora.

Kama Aucho anasimama na Mukoko halafu kwa mbele anacheza Fei, Yanga itakuwa inaweza kusumbuana na timu nyingi za ukanda wake. Lakini hapo hapo katika benchi kutakuwa na machaguo yaliyo bora. Anapoingia Gift au Saido unajua kuna mchezaji ameingia.

Katika safu ya ulinzi achilia mbali mabeki wa pembeni wanaosifika kwa kushambulia lakini ameongezeka mbabe anayeitwa, Yannick Bangala Litombo ambaye alikuwa nahodha wa Vita wakati ikiwa na akina Mukoko. Ina maana Yanga wamepata kiongozi katika safu ya ulinzi.

Wana machaguo manne ya uhakika kwa sasa kupitia kwa Bakari Mwamunyeto, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Dickson Job ambaye kwa sasa ni mlinzi namba moja. Nani atacheza na Bangala? Mwalimu atajibu swali hilo kwa kadri atakavyoona. Huenda pia Yanga wakawa wametatua moja kati ya matatizo yao makubwa kikosini. Eneo la golikipa. Kwanini waliwaacha wote Metacha Mnata na Faruk Shikhalo? Nadhani kwa sababu hawakuwa wazuri kwa kiasi cha kuaminika katika lango la Yanga.

Djigui Diarra amekuwa bora sana mazoezi kiasi kwamba amekuwa akiwastaajabisha wachezaji wenzake. Siku moja alisika Ditram Nchimbi alisema “Huyu kipa sasa tutakuwa tunamfungaje?” Diarra ana sifa nyingi za ukipa ikiwemo kubwa la ‘timing’ ambalo linawatesa makipa wengi nchini.

Labda kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu sasa Yanga watakuwa wamepata kipa namba moja wa uhakika tofauti na Metacha na Shikhalo ambao walilazimika kuwa wanapishana langoni kwa sababu hakuna aliyewahi kuishawishi Yanga moja kwa moja kwamba yeye ni bora. Nilimwambia kiongozi wa Yanga ambaye anahusika sana na masuala ya usajili klabuni hapo, Injinia Hersi Said kwamba walau msimu huu huenda akawa ametengeneza kikosi ambacho kitasaidia kuondoa utovu wa nidhamu klabuni.

Yanga ilijikuta ikitengeneza tatizo hilo kwa sababu kulikuwa na ushindani mdogo wa ubora katika kikosi chao.