Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 15Article 551587

Maoni of Sunday, 15 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

KAGERE TERMINATOR ASIYEKATA TAMAA!

KAGERE TERMINATOR ASIYEKATA TAMAA! KAGERE TERMINATOR ASIYEKATA TAMAA!

JAPO hakung’ara msimu uliopita katika kikosi cha Simba na kushindwa kuvunja rekodi yake ya mabao ya misimu miwili nyuma, lakini Meddie Kagere ‘MK14’ a.k.a Terminator bado ana vitu vya kujifunza kupitia uzoefu wake katika soka, huku akisema kamwe huwa hakati tamaa.

Kagere aliibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo - 2018/19 alipofunga mabao 23 na 2019/20 mabao 22 wakati msimu uliopita alimaliza akiwa na mabao 13.

Kimuonekano Kagere anaweza kutafsiriwa tofauti kama asiyependa stori na mtu, kiburi ila ukipata nafasi ya kufanya naye mazungumzo utafaidi madini anayotoa yanayokusogeza hatua moja mbele.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Kagere ambaye anafunguka mambo mengi yanayoweza kuwafunza wengine wanaohitaji kutikisa kwenye soka na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kazi sambamba na kutokata tamaa. Endelea naye...!

ROHO NGUMU

“Ukiwa na roho ndogo usicheze soka. Nashauri ufanye kazi nyingine kabisa kwani kuna nyakati ambazo unaweza ukapitia changamoto za kukuondoa kwenye reli,” anasema.

“Vivyo hivyo kwa mashabiki wanatakiwa wawe na roho za ustahimilivu kukubaliana na matokeo matatu, la sivyo kama wakijijengea tu kuwa timu yao inatakiwa kushinda mwisho unakuta watu wanapata presha na kupoteza maisha baada ya matokeo kuwa sivyo.”

MTOTO ALIYEJINYONGA

Mwanaspoti liliripoti habari za mtoto Joshua Edward (9) aliyejinyonga Julai 3, saa 2:00 usiku kisa kikiwa ni Simba kufungwa bao 1-0 na Yanga, kumbe hilo lilimuumiza sana Kagere na hii ndio kauli yake.

“Nilisikitika sana baada ya kuiona (habari ile) kwenye kundi letu la kazi, bado alikuwa mdogo. Nilikuwa miongoni mwa wachezaji waliotajwa na baba yake kwamba alikuwa anatupenda, niwape pole sana na Mungu ampumzishe kwa amani,” anasema Kagere.

“Nirudie kusema kuwa mtu akijiingiza kwenye soka awe amejidhatiti, vinginevyo kuna ugumu sana. Niwaambie mashabiki kwamba mchezaji anapitia nyakati nyingi za furaha na huzuni, hivyo timu inapofungwa nasi tunaumia pia hivyo tunapaswa kupewa moyo.”

MADEMU MTANDAONI

Kipindi Kagere wa moto, warembo wengi walikuwa wanajirekodi video na kutuma mitandaoni wakieleza kama staa huyo hajaoa wapo tayari

kujipeleka bure na licha ya kwamba alikuwa akiyaona yote hayo, lakini aliwapotezea.

“Mambo ya soka hayawezi kuingiliana na familia yangu. Pia ni namna ninavyoyachukulia.Niliona ni mashabiki ambao wamefurahishwa na kazi yangu, ndio maana kipindi ambacho sijang’ara huoni likitokea hilo. Vilevile huwa napendwa sana na watoto, huo ndio mtazamo wangu.”

TIMU ZINAZOCHEZA DABI

Kagere anasema mechi za watani maarufu kama dabi huwa hazimpi presha hata kidogo kwani amezizoea tangu akiwa anaichezea Gor Mahia ya nchini Kenya.

Kabla ya kutua Msimbazi, alisajiliwa akitokea Kenya ambako alicheza Gor Mahia yenye ushindani mkali na FC Leopard na ni kama ilivyo kwa Simba na Yanga kwa hapa Bongo.

“Afadhali mashabiki wa hapa Tanzania. Kenya ni hatari maana kuna ukabila ndani yake na mchezaji kama hawajakuelewa usubiri kufuatwa moja kwa moja na wakati mwingine wanaweza wakakurushia mawe.

“Nimejifunza mazingira hayo na

yalinifanya niwe bora zaidi hata hapa,” anasema.

Mechi nyingine za dabi alizocheza ni kati ya APR ya Rwanda dhidi ya Rayon Sports, Club African ya Tunisia dhidi ya Esperance pamoja na Simba na Yanga.

Ukiachana na hizo timu za dabi, anasimulia maisha ya Albania ambako aliichezea klabu KF Trana, kwamba ilikuwa ngumu kuonekana amevaa nguo inayoendana na jezi ya timu pinzani.

“Ndio maana nasema nimejifunza kupanda na kushuka. Yote hayo yananifanya kuwa bora, najijua mimi ni nani na natakiwa kufanya nini, mfano huko nchini Albania ilikuwa nikivaa nguo ya nyumbani ambayo hata kwa mbali inaendana na rangi ya timu pinzani shughuli yake ilikuwa pevu,” anasema Kagere.

“Mashabiki wanakuita wanachangishana pesa, wanakuvua hiyo nguo na kwenda kukununulia nyingine dukani, kisha wanaichoma (moto) mbele yako.”

ISHU NA YANGA

Kabla ya kutua Simba, Kagere alihusishwa kutaka kusajiliwa Yanga na anakiri kuwa ni kweli, lakini kabla ya dili hilo kukamilika alipata dili nje na hakutaka kuliacha akaondoka zake.

“Msimu wa 2014/15 niliwahi kuzungumza na Yanga, lakini sikumalizana nao na nilipoona nimepata dili KF Tirana ya Albania nikaamua kwenda kupata changamoto mpya huko na baada ya kurudi na kusajiliwa Gor Mahia, Simba wakaniwahi na hawakutaka kunichelewesha kunipa mkataba,” anasema Kagere.

UGUMU MAJARIBIO NJE

Kagere anasema wanapofanya majaribio nje ya nchi ni tofauti na Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda huku akitolea mfano Afrika Kusini kwamba wachezaji wanakuwa wengine na utaratibu wao ni mgumu.

“Mnaweza mkacheza mechi ya kirafiki wiki mbili. Sasa kila mechi wanakuwa na mtu spesho wanayemlenga, mfano kama wanataka beki basi washambuliaji mnatakiwa mumpe changamoto, akipatikana kesho wanaanza na kiungo hivyohivyo na nafasi nyingine,” anasema Kagere.

“Mnaweza kuwa wachezaji 100, kesho wanachagua huyu wanaacha yule, wakati huohuo dirisha la usajili linakuwa linakaribia kufungwa, hivyo ikipatikana dili unaachana na majaribio na kuwahi usajili na ndio maana mnaona wengi wanarejea nchini.”

KUSUGUA BENCHI

Mshambuliaji huyo anasema pamoja na kupata changamoto za hapa na pale ikiwamo kutoanza kikosi cha kwanza, lakini kwake ni somo la kujifunza zaidi badala ya kurudi nyuma.

“Mimi siyo mtu wa kukata tamaa. Najifunza kila wakati kujua nifanye nini. Ndio maana nimecheza kwa mafanikio kwenye timu nilizopitia. Hili liwafunze na wengine unapopata changamoto wasikate tamaa, bali wajifunze namna ya kuwa bora zaidi,” anasema Kagere.