Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 11 15Article 488005

Maoni of Friday, 15 November 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

KONA YA MMACHINGA: Kwa kuuza mchele nimejenga nyumba mbili

KONA YA MMACHINGA: Kwa kuuza mchele nimejenga nyumba mbili

Kwa wahitimu wengi, kujiajiri ni mtihani wenye majaribu mengi lakini wachache wanaofanikiwa kuyashinda, hufurahi na roho zao.

Kwa mwananchi wa kawaida wakiwamo wahitimu wa chuo kikuu, kuanzisha biashara au mradi wowote wa kiuchumi ni suala linalokabiliwa na kutokuwa na mtaji wa kutosha.

Tofauti na mtazamo huo wa wengi, Enock Mwabeja ambaye ni mhitimu wa shahada ya siasa ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2016 ameshajenga nyumba mbili baada ya kujiajiri ndani muda mfupi alipoachana na vipindi vya darasani.

“Niliamua kufanya biashara ya mchele kwa sababu niligundua ndiyo inayouzika kuliko nyingine, kila mtu anaitumia na wote wanaweza kuipata,” anasema.

Mwabeja alianza biashara hiyo Desemba 2018 akiwa na mtaji wa Sh7 milioni. Hiyo ilikuwa baada ya kukuza mtaji kwenye biashara ya mifugo aliyoanza nayo muda mfupi baada ya kumaliza chuo. Amewahi kufanya biashara ya madini pia.

Kwa kutumia mtaji huo, anasema alinunua tani 4.5 za mchele na kuanza kuuza kwa bei ya jumla katika duka alilolifungua huko Tandika jijini hapa.

“Nauza mchele kwa bei ya jumla, kuanzia kilo 10 na kuendelea na mpaka sasa nimejenga nyumba mbili, nimenunua viwanja na ninawasomesha wadogo zangu,” anasema mjasiriamali huyo.

Licha ya utitiri wa kodi unaompa changamoto na biashara hiyo kuhitaji mtaji mkubwa kuliko alionao, anasema bado ana ndoto za kuiboresha ili imlipe zaidi.

“Nataka ifike kipindi mchele ninaouza uwe na nembo yangu, niufungashe katika ujazo tofauti na kuusambaza mpaka mikoani,” anasema.