Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 07Article 568903

Maoni of Sunday, 7 November 2021

Columnist: Mwanaspoti

KWAKO JESSE JOHN: Kulikoni? Guu la shingo guu la roho; ama zetu ama zao!

michezo ya Ligi Kuu Bara michezo ya Ligi Kuu Bara

Tangu kuanza Ligi Kuu Bara tumeshuhudia soka la kujituma kwa timu zote zikipambania pointi tatu ama mgeni akijitutumua ugenini na mwenyeji akichagama kulinda hadhi uwanja wa nyumbani.

Pia tumeona timu zikicheza ugenini na kushinda kama ambavyo Kagera Sugar ilivyomfunga KMC katika Uwanja wa Uhuru, Ruvu Shooting alivyomfurusha Biashara United Uwanja wa Karume mjini Musoma, Biashara pia ikimchakaza Tanzania Prisons pale Sumbawanga kwa mabao 3-0 na kadhalika.

Vilevile tumeshuhudia sare na suluhu katika viwanja kadhaa kama ile ya Kagera Sugar na Mbeya City uwanjani Kaitaba Oktoba 16, Geita Gold na Mtibwa 1-1 katika Uwanja wa Nyankumbu uliopo Geita. Si hivyo tu, lakini pia tumeshuhudia suluhu ya Biashara United na Simba pale Musoma, Wana Mangushi - Coastal Union wakitoka suluhu na Simba katika Uwanja wa Mkapa ambapo pia majuzi Coastal Union walibanwa mbavu na Wajelajela - Tanzania Prisons hatimaye kutoka suluhu pale Mkwakwani mjini Tanga wao wakiwa wenyeji.

Jambo la kushangaza katika mechi hizi za msimu huu kumekuwepo na sintofahamu ya baadhi ya timu kuahidiwa mambo flani ili kuishinda Simba tu, na hatujawahi kusikia pesa zikitangazwa hadharani dhidi ya timu nyingine.

Mfano Dodoma Jiji ilipocheza na Tanzania Prisons pale katika Uwanja wa Jamhuri uliopo jijini Dodoma hatukusikia ahadi, ama Biashara United iliyoshindwa kusafiri kimataifa kuifuata Al Ahly Tripo huko Benghazi nchini Libya hatukusikia ikipewa ahadi dhidi ya Mbeya Kwanza pale katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya au ilivyocheza na Mbeya City katika Uwanja wa Karume mjini Musoma. Kulikoni?!!

Baada ya maneno mengi kuzungumzwa juu ya hizi ahadi hasa wadau wa Simba wakilalama kukamiwa na baadhi ya timu ‘wazee wa ahadi wameshindwa vita hiyo sasa hawatangazi na kinachoonekana ni kumfukuza mwizi kimyakimya!’

Hili halina maana kwamba mustakabali wa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu kuweka nguvu kupitiliza dhidi ya timu moja tu, huko ni kudhoofisha juhudi za kukuza viwango vya soka na ukifanya hivyo huna uhakika na uwezo.

Hatukatai kutoa motisha. Motisha ziende mbali zaidi hadi kuziwezesha timu zisizo na uwezo kiuchumi zisafiri kutuwakilisha kimataifa. Pia, tuone ushindani wa kweli hata dhidi ya timu nyingine na wachezaji walie na kugalagala kama wanavyolia na kugalagala wanavyofungwa na Simba sio kupeana mikono na kugongeana tano huku u’shakula tatu za mkwezi. Hii haina tija na ni kujiwekea mazingira, haina tofauti na uchawi.

Lililonisababishia kuandika makala hii ni jinsi Coastal Union walivyoshangilia kama wameingia fainali Kombe la Shirikisho waliposuluhu na Simba ilhali waliposuluhu na Tanzania Prisons kwao Mkwakwani ilikuwa poa! Namungo nao, kana kwamba wamepishana na gari la mshahara walipofungwa na Simba 1-0 waliomboleza kulia na kusaga meno kama vile hawajawahi kufungwa na Simba, ilhali wameshawahi kufungwa ndani nje mara kadhaa na walikuwa hawalii?

Tunataka tuone soka la nguvu na uhakika dhidi ya timu zote katika ligi. Hilo litasaidia kukuza soka letu kwa ushindani wa kweli.

Ni vyema tuondokane na kukamia shoo ya mara moja kwa karanga, muhogo na nazi. Akili ikizowea hiyo kitu kiwango kitashuka jumla jumla! Tusiwe kama dume la nyuki katika kundi la malkia. Hawa hupaa juu sana wakimfikia na kumaliza shughuli dhidi ya malkia hufa moja kwa moja.

Nimalizie kwa kuitakia kila la heti timu yetu ya tafa ‘Taifa Stars’ itakapokipiga dhidi ya DR Congo Alhamis.

Watanzania pamoja na hamasa ya B.1.6 kuwafunga DR Congo na Madagascar bado kuna hatua nyingine ngumu hapo. Tujenge mshikamano na umoja tuachane na Usimba au Uyanga.