Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 03Article 561070

Maoni of Sunday, 3 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

KWAKO JESSE JOHN: Nilichokiona kwa watani "wenye nchi tabu ipo palepale"

KWAKO JESSE JOHN: Nilichokiona kwa watani KWAKO JESSE JOHN: Nilichokiona kwa watani "wenye nchi tabu ipo palepale"

LICHA ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara niwarejeshe kidogo katika pambano la Kariakoo Derby lililopigwa wikiendi iliyopita ambapo mapema kwenye toleo la Septemba 25 niligusia kwa kichwa cha habari kilichosema “Nani kukutwa na taabu?”

Imedhihiri Wenye Nchi wamepata wakati mgumu. Maandalizi ndani na nje ya uwanja kati ya timu hizi yanahuisha ushindi kwa timu husika tangu enzi za Nyamagana.

Inapofika mechi ya watani Yanga huwa na maandalizi kabambe na wanazichukulia uzito mechi hizo za dabi kuliko Kombe la Afrika, na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Moyo wa ushindani, jihadi, kupigania furaha ndivyo vilivyoiwezesha Yanga kuifunga Simba na hii ni jadi ya vijana wa Jangwani miaka yote tangu enzi za 1974 pale Nyamagana, Mwanza. Simba pamoja na kucheza vizuri, kisaikolojia huwa hawapo vizuri dhidi ya Yanga. Kuna vitu vinavyowaogopesha wachezaji na kuwatoa mchezoni ambavyo Yanga wamekuwa wakifanya siku zote. Achana na Mzee Mpili, kuruka ukuta enzi hizo, kutotumia mlango maalumu na kadhalika kwani hata Simba wamekuwa wakiamini Yanga ni wababe wa vita katika hilo kuliko wao.

Katika mechi hiyo ya ngao ya jamii, wachezaji wa kigeni Khalid Aucho, Fiston Mayele, Yannick Bangala, Diarra Djigui na Djuma Shaban waliisaidia sana timu kwa uzoefu wao wa soka la kimataifa, kwani hata ile ‘football maturity’ walikuwa kuliko wachezaji wa kigeni wa Msimbazi kama Sadio Kanoute, Peter Banda, Pape Ousmane Sakho na wengine waliocheza mchezo huo kwa mara ya kwanza. Wageni wa Simba walionekana wachanga dhidi ya “midude hiyo ya Yanga” ambao waliimiliki thamani ya dabi katika ‘medulla oblongata’ zao kuliko Simba.

Pengine unaweza kusema ahadi ya mamilioni yaliwapagawisha kutoka kwa mdhamini, Kocha Didier Gomez alipaswa kuanza na wazoefu kama John Bocco, Meddie Kagere na sikuona sababu ya kumtoa Hassan Dilunga aliyemfanya Djuma asipande mara kwa mara mbele ya lango lake.

Aidha Chriss Mugalu ndiye aliyepaswa kuibeba timu baada ya kukosa nafasi kadhaa na amekuwa na wakati kama huo katika eneo la adui, kwani alikosa utulivu na kupaisha ovyo mipira akiikosesha timu yake mabao, jambo ambalo amekuwa akilifanya mara kwa mara.

Nafasi zile angepata Fiston Mayele ingekuwa balaa kubwa. Naona akili za Simba huenda zikamrejesha Okwi dirisha dogo, kwani ni wazi bado anatamani kurudi na kama bado ana meno atapiga pesa sana maana anajua tija ya dabi.

Aidha, suala la umri kati ya Pascal Wawa na Joash Onyango ukiwalinganisha dhidi ya Bakari Mwamnyeto na Dickson Job ni mjadala katika muktadha wa utimamu wa mwili, wepesi wa uamuzi na akili katika kuikabili nafasi ya mabeki wa kati na kwenda sambamba na presha ya eneo hilo dhidi ya washambuliaji wenye uchu, kasi, maarifa na nguvu kuzitikisa nyavu kama alizonazo Mayele na wengineo.

Nilieleza upungufu wa ukuta wa Simba walipofungwa na TP Mazembe ya DR Congo katika siku ya tamasha la Simba Day. Nilieleza wanaposhambuliwa wanakuwa na wasiwasi, umakini unapungua, wanakosa mtu wa kuwapanga na kuwakumbusha wajibu wa mabeki hasa kipa Aishi Manula kwani kipa huyo si msemaji na uwezo au maarifa ya kuona hatari inayowakabili golini ni mdogo sana ukilinganisha na kina Idd Pazi ‘Father’, Mohammed Mwameja au Juma Kaseja.

Manula alipaswa kumkumbusha Shomary Kapombe kabla Farid Mussa hajaupata mpira na alipaswa kumuwaza Mayele na kujua mikimbio yake. Angekuwa ‘sharp’ angeweza kuwapanga mabeki wa kati kufanya ‘immediate pressure au kula naye sambamba.

Vilevile mashabiki katika dabi ya Kariakoo hii hawakujaa uwanjani kama kawaida yao na mitaani kabla ya mechi hakukuwa na shamrashamra kutokana na timu hizo kutofanya vyema katika mechi zao dhidi ya Zanaco na TP Mazembe na hasa Yanga kushindwa dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia uwepo wa tamaa ya viingilio vikubwa iliyofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya Simba dDay na Wiki ya Mwananchi kufana kulisababisha nyomi kujaa nje ya uwanja karibu na Chuo cha Duce, Kwa Chichi na vibanda umiza vingi vilijaza mashabiki na hili lifanyiwe kazi na mamlaka kuanzia sasa.

Mwisho nimalizie na msemaji mpya wa Yanga, Haji Manara amepata heshima kubwa. Ameiepuka fedheha na wale wengine wamefedheheka. Watake wasitake Simba kumfunga Yanga naiona kama bahati ya “ndege kumnyea binadamu!” LIGI IMEANZA NGOJA TUONE !!!