Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 31Article 566989

Maoni of Sunday, 31 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

KWAKO JESSE JOHN: Tatizo la Simba ni Gomes au uwiano katika usajili?

Aliekuwa kocha wa Simba, Didier Gomes Aliekuwa kocha wa Simba, Didier Gomes

Klabu ya Simba mapema wiki hii ilitangaza kuachana na baadhi ya maafisa wa benchi la ufundi akiwemo aliyekuwa kocha mkuu, Mfaransa Didier Gomes Da Rosa, kocha wa utimamu wa viungo Mtunisia Adel Zrane na kocha wa makipa Mbrazil Milton Nienov kwa kile kilichoelezwa ni uwajibikaji binafsi kwa mwalimu Gomes na hawa wenzie wamesitishiwa mikataba yao.

Kumekuwa na maoni mengi baada ya sakata hilo na mijadala ikaibuka, huku gumzo kubwa likiwa ni kocha wa utimamu wa viungo na kocha wa makipa kutokana na utendaji kazi wao ulioonekana kuwakonga nyoyo mashabiki wa soka na uhaba wa wataalamu hasa wa viungo na kitendo cha kuachana na Zrane halikuwa suala la kueleweka haraka.

Ingali naheshimu sana mtazamo wa viongozi wa Simba, lakini kwangu ilikuwa ni mapema sana kuridhia maamuzi ya kuachana na benchi la ufundi kwa ukubwa ule na hali hii siwezi kuitofautisha sana na kile kilichowahi kufanywa na klabu hiyo mnamo mwaka 2012 ilipoamua kuachana na kocha Milovan Circovic na klabu hiyo kupoteza ubingwa iliyokuwa inautetea.

Simba ya 2011/2012 ilikuwa ni hatari mno ikiifunga Yanga mabao 5-0 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na hata katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ilifanya vyema kwa kiasi kikubwa ikitolewa kwenye raundi ya mwisho kabla ya kuingia makundi kwa penalti dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan ikiwa na nyota kama Emmanuel Okwi, Haruna Moshi, Kelvin Yondani, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Patrick Mafisango (Mungu amrehemu), Felix Sunzu na kadhalika.

Baada ya msimu klabu hiyo ikawapoteza nyota kama Kelvin Yondani, Patrick Mafisango, Emmanuel Okwi, Ally Mustafa na wengineo na kuwasajili nyota kadhaa kama Lino Musombo, Nkanu Mbiyavanga na kadhalika ambao uwezo wao haukuwa sawia na wale walioondoka. Msimu wa 2012/2013 Simba ilianzia kwenye michuano ya Kagame ilikotolewa katika hatua ya Robo fainali na Azam Fc kwa bao 3-1 huku John Bocco akiwa mwiba mchungu katika mchezo huo.

Ndani ya msimu Simba ilitaabika mwanzoni na wakamuondosha mwalimu Circovic na hata alipoingia Patrick Liewig bado timu haikuwa vyema ingali haikuwa kosa la mwalimu bali hakukuwa na uwiano wa kiusajili kati ya wachezaji walioondoka kikosini na walioingia kwani walioondoka walikuwa ni bora kuliko walioondoka.

Msimu uliopita Simba ilikuwa timu tishio si tu kwa hapa nchini bali kwa ukanda huu wa afrika kwa ujumla wakiwa na nyota wengi wazuri lakini kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Miquisone kumeigharimu zaidi Simba ndani ya kiwanja kwani nyota hao waliochangia mabao zaidi ya 42 ya Simba msimu uliopita walikuwa ndio uti wa mgongo wa timu kiuchezaji.

Mwalimu Gomes amesajiliwa wachezaji ambao hawana daraja kama walioondoka na licha ya Simba kuondoshwa kizembe na Jwaneng Galaxy, lakini ukweli usiopingika ni kuwa klabu hiyo ina wachezaji wa kiwango kisichofikia walioondoka na mwalimu alipaswa kupewa muda zaidi ili kuitengeneza Simba yake yenye sura mpya bila kuwekewa presha kubwa kimatokeo vinginevyo kila mwalimu atakayekaa Simba kwa sasa atajikuta kwenye shinikizo kubwa kimatokeo ilhali wachezaji waliosajiliwa wanahitaji muda zaidi.

Ni vyema Simba watafute haraka mwalimu wa kuja kuinusuru klabu kwenye kombe la Shirikisho barani Afrika kwani timu hii kwa sasa inahitaji utulivu, mshikamano, umoja na dua za pamoja kwa mustakabali mzuri kwa ustawi wa soka letu na majaaliwa ya kheri kwenye nafasi nne za ushiriki wa timu zetu kwenye michuano ya kimataifa.

UCHUMI KWA KLABU UPEWE KIPAUMBELE

Tumeshuhudia sakata la hivi karibuni, kwa wawakilishi wetu michuano ya Shirikisho ya Afrika, Biashara United kushindwa kujisafirisha kwenda Libya kwa ajili ya mchezo wa marudiano. Tunaipongeza serikali kwa kuwapa msaada wa ndege ingawa hadi dakika za mwisho suala la vibali likatatiza safari yao.

Kushindwa kwenda Libya pia kumechangiwa na kutokuwa na mipango ama kujiandaa mapema kwa maana safari ilijulikana, maandalizi ya mapema yangesaidia hata vibali kupatikana mapema, tumejifunza katika hili.

Timu zinashiriki ligi kwa kuwa na lengo la kutwaa ubingwa pia ziweze kushiriki kimataifa kwa kuwakilisha nchi, ila kwa sasa kumeonekana suala la uchumi limekuwa shida. Aidha wadhamini wanaoning’iniza mabango yao kwenye jezi vifuani wanawanyonya kwa kutowawezesha kiuhakika. Ifikie mahala sasa klabu ziingie mikataba ya uhakika ikiwa ni pamoja na kuwawawezesha kusafiri kimataifa,haitakuwa na maana unaweka nembo kifuani na jina kubwa kwenye kusafiri timu inafeli,na mdhamini anafeli,” watu wa kawaida hawatojua kuwa kazi yako ni kulipa mishahara tu”.

Niliongea na kocha wa Namungo akanipa uzoefu kuwa, kusafiri kimataifa hasa mbali na Afrika Mashariki ni gharama sana. Klabu zitakuwa zinashiriki ligi zikikaribia ubingwa zitajilegeze ili wenye uwezo wachukue nafasi zao, hii haitokuwa na maana ya kuwepo kwa ligi.

Aidha alinitanabaishia kuwa, ukikosa connection mfano walipokwenda Angola ilibidi kuepuka rungu la CAF kukodi ndege iliyowawagharimu dola 200,000, deni ambalo wamemaliza juzi. Hii ni hatari sana, wadhamini wakubwa jitokezeni kuzidhamini timu zote ili kuisaidia serikali na TFF kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.