Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 14Article 563191

Maoni of Thursday, 14 October 2021

Columnist: mwananchidigital

Kamati ya Bomani na sheria mpya ya madini

Kamati ya Bomani na sheria mpya ya madini Kamati ya Bomani na sheria mpya ya madini

Ili kubaini na kuandaa mapendekezo ya jinsi ya kuondoa upungufu unaosababisha malalamiko kuhusu sekta ya madini, Kamati ya Bomani ilikutana na wadau mbalimbali wakiwamo wenye migodi, wafanyabiashara ya madini, wafanyakazi migodini, wataalamu wa sekta hiyo na wananchi kwa ujumla.

Kamati ilikutana na uongozi wa migodi ambao ulionesha kuridhishwa na mazingira ya uwekezaji katika sekta hiyo hapa nchini. Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka, na kuieleza kamati kuwa suala la uhusiano mzuri na jamii mwenyeji ni sehemu muhimu ya sera zao za kuendesha biashara.

Maoni ya wamiliki wa migodi

Uongozi wa migodi ulipendekeza mabadiliko katika maeneo mbalimbali ikiwemo utaratibu wa utoaji leseni na vibali vya uchimbaji wa madini, ambapo uongozi huo ulionyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa taasisi mbalimbali za Serikali zinazowahudumia.

Pia walilaumu ucheleweshaji wa utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini katika Ofisi za waziri na Kamishna wa Madini ambao ndio wenye mamlaka ya utoaji leseni hizo na Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana kwa kuchelewa kutoa vibali vya ajira kwa wafanyakazi wa kigeni.

Idara ya Uhamiaji nayo ilitajwa katika mapendekezo ya uongozi wa migodi kwa kuchelewa kutoa vibali vya kuishi kwa wageni. Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo iliguswa kwa madai kwamba huchelewesha marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kutokamilisha kwa wakati taratibu za misamaha au nafuu ya kodi kwa kampuni za madini.

Maoni mengine yaliyotolewa na wadau ni yale ya kuinyooshea Serikali kidole kwa kutotimiza majukumu yake kama vile kushindwa kudhibiti wachimbaji wadogo na wavamizi maeneo ya migodi, hivyo kusababisha migongano baina ya migodi na wachimbaji wadogo.

Uhaba wa wataalamu katika sekta ya madini nao uliwekwa kwenye mapendekezo hayo. Ilielezwa kuwa Serikali haijafanikiwa ipasavyo katika kuhakikisha kuwa Taifa linajitosheleza kitaaluma katika sekta ya madini na ndiyo sababu ya wawekezaji hulazimika kutafuta wataalamu kutoka nchi za nje. Pia wenye migodi walilalamikia ukosefu wa uzoefu wa kutosha kwa wataalamu wa hapa nchini kutokana na sekta yenyewe kuwa changa.

Kamati ilionesha uchambuzi wa maoni ya wadau waliokuwa na maoni tofauti juu ya sekta ya madini.

Wawekezaji walitaka mfumo wa usimamizi wa sekta ya madini uboreshwe kwa kuimarisha miundombinu, huduma za usalama na usimamizi wa kodi.

Matakwa ya wananchi

Kwa upande mwingine, wananchi wanaoishi karibu na migodi ambao huwa hawafaidiki na uvunaji wa rasilimali ya madini, walitaka kuona manufaa zaidi katika huduma za jamii na ajira kuliko ilivyokuwa kabla hawajahojiwa na kamati hiyo. Wachimbaji wadogo nao waliona kuwa ujio wa uwekezaji umewafanya kunyang’anywa maeneo na kuwapotezea fursa za kujipatia kipato na ajira.

Wataalamu wa fani mbalimbali wanaotoa huduma kwenye sekta ya madini waliona Serikali haijawawezesha katika kuisimamia kikamilifu sekta ya madini, kutokana na kutopatiwa mafunzo, nyenzo na bajeti ya kutosha, na pia ilionekana kuwa vingi vilivyotolewa kwa wawekezaji ni matokeo ya upungufu uliomo kwenye sera, sheria na mikataba inayosimamia na kuongoza sekta ya madini. Kwa upande wa Serikali, nayo ilionyesha kutoridhishwa na namna sekta hiyo inavyochangia mapato yake na uchumi kwa ujumla.

Wadau wote walikuwa na maoni kuwa utaratibu mzima wa kuiendeleza sekta ya madini unahitaji kuangaliwa upya na kuboreshwa zaidi ili sekta hiyo iweze kukidhi matarajio ya Taifa.

Pamoja na hayo yote, kuna masuala yaliyojitokeza katika sekta ya madini ambayo yalihitaji kupatiwa ufumbuzi ili kuiboresha sekta hiyo ambayo ni wajibu wa Serikali na mwekezaji.

Mapendekezo ya kamati

Katika hali hii, mapedekezo ya kamati yalieleza kuwa kila sehemu yanapogundulika madini yenye kuhitaji uwekezaji mkubwa, Serikali ijenge miundombinu kama barabara, umeme, maji na huduma za jamii kama vituo vya afya, shule na huduma za usalama.

Ilipendekezwa pia kwa mradi mkubwa kama Kabanga, Serikali ianze mapema maandalizi ya kuweka miundombinu ya umeme, barabara na reli na iwalazimishe wawekezaji kuwakatia bima za ajali wafanyakazi wao.

Kuhusu Sera ya Madini ya mwaka 1997, ilipendekezwa kuwa Serikali iainishe na kuweka uwiano baina ya vivutio vya mfumo wa kodi na vingine kama vile, uwepo wa madini na utulivu wa kisiasa, na sera iainishe bayana nafasi ya Serikali kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta ya madini.

Ilitakiwa sera iweke wazi umuhimu wa kushirikiana na kufungamanisha sekta ya madini na zingine za uchumi kama njia ya kuharakisha maendeleo, na ielekeze vivutio vingi vitolewe kwa utafutaji wa madini na si kwa uchimbaji madini.

Mapendekezo mengine kwenye Sheria ya Madini yalikuwa ni pamoja na maombi ya leseni ndogo yawasilishwe katika ngazi za chini na leseni zitolewe katika ofisi za kanda ili kuharakisha shughuli za uchimbaji na leseni za uchimbaji mkubwa (SML) hali kadhalika.

Mamlaka ya Waziri kufuta leseni nayo yalizingatiwa na kamati hiyo. Mapendekezo yalikuwa kwamba Kifungu Na. 57 cha Sheria kifanyiwe marekebisho ili kumtaka waziri atekeleze uamuzi wake ndani ya siku 60 baada ya kutoa taarifa ya kusudio la kufuta leseni.

Kifungu cha 10 cha Sheria ya Madini kifanyiwe marekebisho kwa kumtaka waziri mwenye dhamana ya kuingia mkataba wa madini kufanya mashauriano kwanza na mamlaka katika maeneo ya mgodi husika kabla ya mkataba.

Hatimaye ikaja Sheria mpya ya Madini namba 14 ya mwaka 2010. Sheria hii ilitungwa baada ya mchakato mrefu uliotanguliwa na kamati na tume mbalimbali zilizoundwa pamoja na msukumo mkubwa kutoka asasi za kiraia na kuhitimishwa na kamati iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Mark Bomani iliyoundwa mwaka 2007. Sheria hii inaweka utaratibu wa kisheria katika kutekeleza sera mpya ya madini ya mwaka 2009.

Kamati ilisema ianzishwe mamlaka ya madini nchini inayojitegemea na iwe na jukumu la kusimamia na kuendeleza sekta, na ipatiwe wataalamu wenye ujuzi na uzoefu katika sekta ya madini na vitendea kazi na bajeti ya kutosha na ipewe sehemu ya makusanyo ya mrabaha kwa ajili ya bajeti yake.

Mara baada ya kuanzishwa kwa mamlaka ya madini, kamati ya ushauri wa madini ivunjwe na majukumu yake yatakayokuwa yameboreshwa yahamie kwenye mamlaka hayo. Kuhusu suala la fidia, kamati ilipendekeza kuwa Sheria ya Madini ifanyiwe marekebisho kwa kujumuisha vipengele vya fidia kwa wanaopisha shughuli za madini.

Kuhusu utatuzi wa migogoro, mapendekezo yalieleza kifungu cha 101(2) cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998 kirekebishwe ili kumtaka Kamishna wa Madini kutatua migogoro iliyowasilishwa kwake au kutoa sababu za kukataa kusikiliza mgogoro huo, na pia liundwe baraza maalumu kwa ajili ya kutatua migogoro ya madini (Mining Tribunal).

Kutokana na mapendekezo haya na mengine yaliyotolewa na Kamati ya Bomani, Sheria hii ya madini namba 14 ya mwaka 2010 ilipitishwa na Bunge Ijumaa ya Aprili 23, 2010 na kusainiwa na Rais Kikwete Alhamisi ya Mei 20, 2010.

Kesho tutaangalia jinsi mabadiliko ya sheria yalivyowanufaisha wachimbaji wadogo ambao, kwa sasa wamekuwa wakishiriki kwenye ukuaji wa sekta hiyo na uchumi wa Taifa kwa ujumla.