Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 18Article 543274

Maoni of Friday, 18 June 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Kifo cha Kaunda pigo Afrika

Kifo cha Kaunda pigo Afrika Kifo cha Kaunda pigo Afrika

RAIS wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 97.

Kifo cha kiongozi huyo aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ni pigo kubwa kwa bara la Afrika.

Hivi karibuni ilitolewa taarifa kuwa alikuwa anaumwa homa ya mapafu na kulazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Maina Soko nchini humo na jana alitangazwa kuwa amefariki dunia.

Kaunda baba wa taifa la Zambia aliyepigania uhuru na kulikomboa taifa hilo kutoka kwa Waingereza mwaka 1964, alishika uongozi wan chi hiyo kwa miaka 27 hadi mwaka 1991.

Atakumbukwa zaidi kwa harakati zake za kupigania Uhuru wa Afrika Kusini nan chi nyingine za Kusini mwa Afrika akiwa mshirika mkubwa wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere. Kutokana na ukaribu wake na Mwalimu Nyerere, Kaunda aliamua kumuita mtoto wake wa kiume jina la Kambarage.

Aliruhusu Zambia kuingia kwenye siasa za vyama vingi, lakini alishindwa kutetea kiti chake uchaguzi mkuu wa 1991 na nafasi hiyo kuchukuliwa na Fredrick Chiluba.

Kaunda alikuwa mwalimu kitaaluma na wakati akipigania uhuru wa nchi hiyo iliyokuwa ikiitwa Rhodedia Kaskazini na alikuwa ni kati ya marais wa Afrika waliokuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa Afrika.

Kaunda alikuwa amebaki pekee aliyekuwa hai kati ya marais waliokuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.

Marais wengine waliokuwa mstari wa mbele ukombozi Kusini mwa Afrika pamoja na Kaunda ni Nyerere, Robert Mugabe wa Zimbabwe, Samora Machel wa Msumbiji, Kamuzu Banda wa Malawi na Rais Milton Obote wa Uganda.