Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 05Article 568342

Maoni of Friday, 5 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Kijiwe cha Salim Said Salim: Rashid Yakini Staa aliyeondoka akiacha historia tamu na chungu

Kijiwe cha Salim Said Salim: Rashid Yakini Staa aliyeondoka akiacha historia tamu na chungu Kijiwe cha Salim Said Salim: Rashid Yakini Staa aliyeondoka akiacha historia tamu na chungu

MARA nyingi tunasikia masikitiko ya wanamichezo walioipatia heshima nchi hii na kuifanya ijulikane wametupwa na kuwa na hali ngumu katika siku za mwisho za maisha yao kwenye dunia hii iliyojaa mitihani.

Tatizo hili pia lipo katika nchi nyingi za Afrika na unapopata maelezo ya wanamichezo waliokuwa mashuhuri walivyoishi siku za mwisho unaweza kutokwa na machozi.

Miongoni mwa wanamichezo walioteseka na kugeuzwa kuwa kama vinyago vya mpapure kama hawakufanya mambo ya maana ni mshambuliaji maarufu wa timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, Hayati Rashid Yekini.

Waandishi wa habari na mashabiki wa michezo wengi wa Afrika na nje hawakushangazwa Yakini aliposhinda tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika 1993. Yakini anakumbukwa zaidi kwa bao alilofunga nchini Ufaransa katika fainali za Kombe la Dunia 1998 lililoipeleka Nigeria kuingia mzunguko wa pili wa mashindano hayo ilipoibuka na mabao 3-0 dhidi ya Bulgaria.

Aliisaidia Nigeria kushinda mashindano ya nchi za Afrika Magharibi na kuiwezesha kubeba Kombe la Mataifa la Afrika 1994. Alikuwemo katika kikosi cha Nigeria kilichoshiriki mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Seoul, Korea Kusini 1998. Aliifungia Nigeria mabao 37 katika michezo 58 ya kimataifa.

Idadi ya magoli aliyoyafunga mpaka leo ni kubwa kuliko ya mchezaji yeyote kabla na baada ya Nigeria kupata uhuru 1960.

Yekini alizaliwa Kaduna, Kaskazini mwa Nigeria katika familia ya waumini wasiotetereka wa Kiislamu, Oktoba 23, 1963 na kufariki dunia mjini Ibadan Mei 4, 2012 akiwa na miaka 48. Yekini aliyekuwa na umbo la miraba minne, urefu wa futi 6 na inchi 3 na uzito wa kilo 85 wakati wa ujana wake alikimbia kwa mwendo wa kasi na kupiga makombora hata alipokabiliana na nyavu baada ya kumpiga chenga kipa. Siku moja 1983 nikiwa Nigeria wakati Simba ilipokwenda kucheza na Raccah Rovers, katika Uwanja wa Surulere uliopo Lagos, nilikutana na Yekini aliyekuja kuwaangalia vijana wenzake wa Kaduna.

Wakati ule Yekini nilimfahamu miaka miwili kabla alikuwa amechomoza kama nyota wa Shooting Stars ya Ibadan, nilimuuliza angependa kufanya nini atapostaafu.

Huku akivuta uradi na tasbihi mkononi aliniambia: “Mimi ni kama (Omar) Mahadhi wa kwenu. Napenda mpira na Quran, na kwa hiyo nitafundisha chuo na kufundisha vijana kandanda kwa lengo la kujenga maelewano kati ya Wakristo na Waislamu kama tuliyonayo katika timu za mpira.”

Hayati Mahadhi wakati ule alikuwa kipa wa Tanzania na alikuwa anafundisha madrasa kwao Tanga. Tulizungumza mengi na nakumbuka alivyoshindwa kuamua yupi bora kati ya makipa wawili mahiri wa Tanzania zama zile, Athuman Mambosasa ambaye alikuwa mrefu na Mahadhi aliyekuwa mfupi. Miaka ikapita na Mei 2006 nilipokuwa katika boti kwa safari ya nusu saa kutoka Copenhagen, Denmark kwenda kuwasalimia rafiki zangu Malmo, Sweden nilikutana na Sunday Oliseh, mchezaji maarufu wa Nigeria na rafiki wa Yekini. Wakati ule Oliseh alikuwa katika mapumziko akimalizia mkataba na klabu moja ya Ubelgiji. Nilipomuuliza habari za Yekini alianza kulengwa na machozi na kuniambia “ni hadithi ya kusikitisha na kutisha.”

Aliniambia Yekini alikuwa fukara na anaugua maradhi ya akili yaliyotokana na mambo mengi, miongoni mwayo kutapeliwa na marafiki aliofanya nao biashara ya kubadilisha fedha za kigeni na kuuza mapambo ya dhahabu. Vilevile serikali na klabu za Nigeria na nje alizochezea hazikumjali na zilimgeuza tambara bovu. “Sio hayo tu, hata na sisi tuliocheza naye timu ya taifa tumemtupa. Inasikitisha,” aliniambia.

Mbali ya kudhulumiwa fedha nyingi katika biashara, serikali ya Nigeria mpaka alipofariki dunia ilishindwa kutimiza ahadi ya kumpa nyumba na gari kama tunzo ya mchango wake alipokuwa na timu taifa.

Hali hiyo ilimchanganya na matokeo yake katika miaka ya mwisho alizunguka katika barabara za Ibadan akiwa amevaa kaptula, anatembea peku na hataki kuzungumza na watu. Hakuwatambua hata rafiki zake.

Oliseh aliniambia Yekini alicheza mchezo wa mwisho 2005 akiwa na klabu ya Gateway United na kwa vile alicheza vibaya mashabiki walimzomea na hilo lilimuumiza kisaikolojia. Alitoka uwanjani akilia na kusema: “Masikini Yekini…leo anazomewa badala ya kushangiliwa.”

Takriban miaka miwili kabla ya kufariki dunia ilikuwa kawaida kumuona anajisaidia haja kubwa barabarani na kuomba mahindi ya kuchoma au ugali kwa mama ntilie.

Siku moja alimpora mkate polisi na baada ya kugundua aliyefanya kitendo kile ni Yekini yule askari sio tu alimsamehe, bali alimchukua hadi nyumbani kwake akampa chakula na kumuogesha.

Yekini aliteseka katika barabara za Abidjan hadi siku alipofariki dunia Mei 4, 2012. Mazishi yake yaliibua huzuni hasa kutoka kwa wachezaji wa zamani wa Nigeria. Watu walilia pale mmoja wa rafiki zake alipopiga kelele na wakati mwili wake ulipoteremshwa kaburini - “Rashid, nyumba na gari nzuri uliyoahidiwa na serikali na kutopewa utazikuta unakokwenda. Kwaheri kipenzi cha wanaojua thamani ya mtu. Mungu akulaze mahali pema.”

Sasa ni zaidi ya miaka 10 tangu alipoiaga dunia, lakini mchango wake hautasahulika kama yalivyo machungu aliyoyapata siku za mwisho za maisha yake.

Yaliyomkuta Yekini ni fundisho kwa wachezaji wengine wa Afrika.