Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 11Article 537187

Maoni of Tuesday, 11 May 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Kwa hili TFF haikwepi mzigo wa lawama

Kwa hili TFF haikwepi mzigo wa lawama Kwa hili TFF haikwepi mzigo wa lawama

KITENDO cha mechi ya watani wa jadi iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi kutofanyika baada ya Yanga kugomea kutokana na mabadiliko ya ghafla ya muda wa mchezo yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hapana shaka kinapaswa kuwa darasa kubwa kwa shirikisho hilo na mamlaka nyingine nchini zinazohusika na michezo.

Uongozi shirikishi, usimamiaji wa kanuni na mawasiliano mazuri kati ya mamlaka, klabu na wadau wa michezo hasa soka ni mambo ya msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa ustawi wa soka na michezo mingine.

Kitendo cha Yanga kugomea mechi hiyo kinafundisha TFF na mamlaka nyingine kujenga tabia ya kushirikisha wadau wake pindi inapochukua uamuzi badala ya kujiamria yenyewe, kusimamia kanuni zilizotungwa na kupitishwa na kamati yake ya utendaji lakini pia kujenga hulka ya kuwasiliana na wanafamilia wake pindi kunapotokea jambo la kidharura.

Laiti kama Yanga wangekuwa wameshirikishwa vyema katika uamuzi huo na kupewa taarifa sahihi na kwa wakati, pengine mechi hiyo ingechezwa au isingeleta taharuki iliyojitokeza.

Mazingira ya mechi kuahirishwa ndio yanayotoa uhalisia kuwa ushirikiano, mawasiliano na usimamiaji wa kanuni kwa shirikisho na wadau wake umekuwa duni, kadhalika TFF haiwezi kukwepa mzigo wa lawama cha kilichotokea, kwani walitangaza wao kuahirisha wakijua ni kinyume na kanuni na sheria ya soka, ikizingatiwa soka haliendeshwi kwa matamko na maagizo ila ni kanuni.

MAJI YALIKOROGEKA HAPA

Awali mchezo huo ulikuwa ufanyike saa 11;00 jioni lakini wakati mashabiki wengi wakiwa wameshaingia uwanjani tangu saa 3 asubuhi, ilipofika saa 8:00 mchana kulitolewa tangazo la kuhairishwa hadi saa 1:00 usiku huku ikielezwa ni agizo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Hali hiyo ilizuia kelele kwa mashabiki wa timu hizo mbili ambao wengi waligeuka na kulitazama jukwaa kuu na kunyoosha mikono kuonyesha kuwa hawakubaliani na mabadiliko haya.

Baada ya muda mfupi uongozi wa Yanga ulitoa tangazo la kutokubali mechi kuahirishwa kienyeji kinyume na kanuni ya soka inayoelekeza taarifa ya kuahirishwa inapaswa kutolewa saa 24 kabla ya muda wa mchezo husika.

Kanuni namba 15 (10) ya Ligi Kuu inayohusu utaratibu wa mchezo inasema “Mabadiliko yoyote ya muda wa kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa pande zote husika za mchezo angalau saa 24 kabla ya muda wa awali.”

Yanga, ilisema ingepeleka timu uwanjani kama kawaida na kufuata taratibu na kama mechi haitaanza kama ilivyopangwa wangeondoka uwanjani.

Baada ya tangazo hilo la Yanga kuenea kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki walikuwa wakisubiri je, uongozi wa klabu hiyo utatekeleza msimamo wao au ndio utalegeza kamba baadae.

Hata hivyo ghafla saa 10:15 jioni basi la Yanga lilifika na kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki wao timu iliingia kupasha misuli uwanjani kisha saa 10:41 na dakika nne baadae walimaliza na kurudi vyumbani.

Saa 10:58 timu hiyo ilirejea uwanjani ikiwa na jezi za mechi tayari kuanza mchezo na kisha kukaa ndani ya uwanja kwa dakia 15 na kisha kutoka na kuwapungia mikono ya kuwaaga mashabiki wao waliokuwa wakiwashangilia sana.

Saa 11:30 Yanga iliondoka kabisa uwanjani hapo ikisindikiza na mashabiki wao walioamua pia kuondoka na kupishana na Simba iliyokuwa ikiwasili muda huo.

Wachezaji wa Simba waliingia uwanjani kupasha misuli saa 12:06 na kuamsha shangwe kwa mashabiki wao na dakika nane baadae iliingia bendi ya jeshi ikipiga vyombo vyao hivyo mashabiki kuzidi kuwashangilia, lakini dakika mbili baada ya bendi kuingia lilitolewa tangazo la kuahirishwa kwa mchezo hadi itakapotangazwa tena na kufanya mashabiki hao kupigwa na butwaa huku wale wachache wa Yanga wakishangilia kwa furaha.

Baada ya tangazo la kuahirishwa kwa mchezo kutolewa mashabiki walianza kutoka nje ya uwanja huku wakiimba wakitaka kurudishiwa fedha zao huku viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi wakishindwa kuonekana.

Kabla ya sekeseke hilo Rais wa TFF, Wallace Karia alionekana uwanjani, lakini alishindwa kushuka chini kutokana na hofu ya mashabiki waliokuwa na hasira wakidai chao.

Mashabiki wa Yanga na Simba walionekana kuungana pamoja wakishinikiza kuwa hawatatoka uwanjani hapo mpaka warudishiwe pesa yao ya viingilio kabla ya kutakiwa kuondoka eneo hilo kwa amri ya askari polisi.

Hata hivyo mashabiki waliendelea kugoma kutoka ndipo polisi ikabidi watumie nguvu kwa kupiga mabomu ya machozi yaliyoleta taharuki kila mmoja akikimbia huku na kule kujiokoa.

WAAMUZI WAZUA SINTOFAHAMU

Katika hali ya kushangaza, licha ya Simba kufika uwanjani ndani ya muda uliopangwa baada ya mabadiliko hayo, waamuzi waliopaswa kuchezesha mechi hiyo hawakuonekana uwanjani kupasha wala kuwakagua Simba.

Lakini hata Yanga walipofika katika muda ule uliopangwa awali, bado waamuzi hawakuonekana.

Kikanuni kama waamuzi hawapo uwanjani, hakuna timu inayoweza kupata pointi za mezani au mechi kuchezwa.

MAXIME AIBUKA SHUJAA

Miongoni mwa watu waliogeuka gumzo kutokana na sakata hilo ni kocha wa zamani wa Kagera Sugar, Mecky Maxime aliyepewa kibarua cha kuwa kocha wa kituo cha kukuza vipaji cha Cambiaso Sports Center.

Hivi karibuni wakati akitambulishwa kuwa kocha wa Cambiaso, Mecky alisema; “Sisi Tanzania tunafeli kwa sababu viongozi wengi wasiojua mpira ndio maana mpira wetu hauendelei.

“Mpira wa Tanzania unaongozwa na watu wengi wasiojua ndio hao wanautufelisha kwenye mpira, hilo mkubali mkatae. Siku zote mpira unaongozwa na watu wa mpira,” alisema Mecky.

Baada ya kutangazwa kuahirishwa kwa mechi ya Simba na Yanga, kauli hiyo ya Mecky ilionekana kuchukua nafasi kwa watu kuchukua vipande vya video na kuvisambaa kwenye mitadao ya kijamii, pia hata mashabiki wengi waliofika uwanjani walipohojiwa na vyombo vya habari walisema kuwa kocha huyo aliongea ukweli kwani jambo hilo limetokea kweli siku hiyo kwa kuonyesha ubabaishaaji wa viongozi wa soka.

HISTORIA INAHUKUMU

Kuahirishwa kwa mechi hiyo ni muendelezo wa maamuzi ya ghafla ambayo TFF na bodi ya Ligi wamekuwa wakiyatoa pasipo ushirikishwaji wa timu na kufuata kanuni.

Iko baadhi ya mifano ya namna baadhi ya mabadiliko ya ratiba za muda na kiwanja cha mechi yalivyofanyika kinyume na kanuni.

Miezi kadhaa iliyopita, timu ya KMC ilijikuta ikilazimishwa kucheza katika uwanja tofauti na ule uliopangwa katika ratiba wakati ilipokabiliana na Ihefu ya Mbeya.

Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa katika Uwanja wa Sokoine na kinyume na kanuni, ndani ya muda usiozidi saa 24 walilazimishwa wakacheza katika Uwanja wa Highlands Estates huko Mbalali. Hivi karibuni, mchezo baina ya Simba na Mtibwa uliopangwa kuchezwa saa 10 jioni ulibadilishwa ghafla na kuchezwa saa 1 usiku.

Kadhalika mchezo wa Yanga na Azam uliopigwa Aprili 25, ulitangazwa kubadilishiwa muda kutoka saa 1 usiku hadi saa 2:15 usiku lakini ikiwa ni siku nne kabla ya kuchezwa, huku pambano la Yanga na Biashara United likigomewa na TFF kupigwa saa 10 jioni na kubaki saa 1 usiku licha ya Yanga kuomba kama ilivyofanya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar.

Join our Newsletter