Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 07 18Article 547369

Maoni of Sunday, 18 July 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Ligi Kuu inaisha na utamu wake

Ligi Kuu inaisha na utamu wake Ligi Kuu inaisha na utamu wake

PAZIA la Ligi Kuu linafungwa leo kwa timu zote kuwa viwanjani huku macho yote ya mashabiki wa soka yakitamani kujua nani ataungana na Mwadui kushuka Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Mabingwa watetezi Simba watacheza na Namungo na wanatarajiwa kukabidhiwa kombe lao baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin, Mkapa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.

Hii ni mara ya pili kwa mabingwa hao mara nne kukabidhiwa kombe mbele ya Namungo baada ya msimu uliopita kukabidhiwa ugenini kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi.

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes alisema wanahitaji kushinda mchezo huo ili washerehekee kwa furaha lakini kujiandaa na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga utakaochezwa Julai 25, mkoani Kigoma.

“Kuchukua taji haimaanishi kuwa hatupaswi kupata matokeo mazuri, tunahitaji kushinda kwa ajili ya sherehe yetu ya kukabidhiwa taji,” alisema.

Gomes alisema ikiwa watashinda mchezo huo utazidi kuwapa morali wachezaji kuelekea fainali ya FA.

Namungo watakuwa wanatafuta kulinda heshima, kwani tayari wameshindwa kumaliza nne bora za juu. Mzunguko wa kwanza Simba ilishinda mabao 3-1.

Yanga ambao wanashika nafasi ya pili watakuwa ugenini Dodoma kucheza na Dodoma Jiji katika Uwanja wa Jamhuri.

Mchezo huo ni wa kutafuta heshima kwa kuwa tayari Yanga inashika nafasi ya pili kwa pointi 73 katika michezo 33 ambazo hakuna mwingine atakayezifikia.

Pia, ushindi kwao ni muhimu kuelekea fainali ya FA dhidi ya Simba kwa ajili ya kujenga morali na hamasa.

Azam FC itakuwa ugenini katika Uwanja wa Mlandizi dhidi ya Ruvu Shooting, mchezo ambao kila timu itakuwa inatafuta kulinda heshima kwani wanalambalamba hao wamejihakikishia nafasi ya tatu na Ruvu wako katika nafasi nzuri kuendelea kuwepo katika ligi.

Kazi kubwa ipo kwa timu zinazoweza kushuka daraja ambazo ni Gwambina yenye pointi 34 ikishika nafasi ya 17, Ihefu yenye pointi 35 katika nafasi ya 16 ambazo zikipoteza michezo ya leo basi zitaungana na Mwadui.

Gwambina iliyoanza ligi msimu huu kwa kasi baadaye iliyumba na kuingia hatarini ikajiondoa kidogo lakini haikudumu kutokana na kukaa nafasi za chini kwa muda mrefu.

Mchezo wa Gwambina dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Nelson, Mandela, Sumbawanga hautakuwa rahisi kwa sababu wanakutana na timu isiyokubali kufungwa hasa inapokuwa nyumbani.

Iwapo itashinda bado haitakuwa salama kutokana na kuzidiwa na timu nyingine zilizopo juu yake, pengine wawaombee mabaya walioko juu ikiwemo JKT Tanzania na Coastal Union wapoteze au mabao yaamue waingie hatua za mtoano.

Wengine wenye presha ni Ihefu itakayochuana ugenini dhidi ya KMC Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mwenendo wa timu hiyo awali ulikuwa mzuri hasa mzunguko wa kwanza lakini kadiri siku zilivyosogea walishindwa kumudu ushindani na kuporomoka.

Ihefu ni miongoni mwa timu zenye presha kwani ikipoteza au kupata sare mchezo huo inashuka lakini ikishinda bado itategemea na walioko juu yake JKT Tanzania na Coastal watatokaje.

Timu nyingine zilizoko hatarini ni JKT Tanzania inayoshika nafasi ya 15 kwa pointi 36 ikifuatiwa na Coastal Union yenye pointi 37.

Hizi nazo hazikuwa bora msimu huu zilikua zinasuasua katika mechi tofauti, ukilinganisha na msimu wa mwaka juzi, kiwango chao kilipungua na kushindwa kuwa katika ushindani.

JKT itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar, wenyeji wakipoteza wanashuka lakini wakishinda itategemea na matokeo ya Coastal na Mtibwa kuamua kama watacheza mtoano au kubaki salama, kwa maana tofauti ya mabao inaweza kuangaliwa.

Mtibwa inayoshika nafasi ya 13 kwa pointi 39 pia, inahitaji matokeo ya ushindi au sare ili kubaki salama.

Coastal Union itawakaribisha Kagera Sugar katika Uwanja wa Mkwakwani na wenyeji wanahitaji ushindi na endapo watashinda huenda wakabaki kutegemea na matokeo dhidi ya wengine wanaokimbizana.

Kagera Sugar inashika nafasi ya 11 kwa pointi 40 kidogo unaweza kusema wako salama japo sio sana. Wanaweza wasishuke ila wakaangukia kapu la mtoano.

Mbeya City inayoshika nafasi ya 12 kwa pointi 39 nao wako salama kidogo ila wanahitaji ushindi kubaki salama zaidi.

Mbeya City itawakaribisha Biashara United kwenye Uwanja wa Sokoine, ambao tayari wamejikatia tiketi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.