Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 20Article 552748

Maoni of Friday, 20 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Ligi zimeanza Ulaya, Tutarajie majeraha haya

Nyota wa Chelsea, Hakim Ziyech akipatiwa matibabu Nyota wa Chelsea, Hakim Ziyech akipatiwa matibabu

Zile Ligi Kuu Bora za Ulaya zinazopendwa duniani ikiwamo ya England (EPL), Hispania (La Liga), Ujerumani (Bundesliga), Ufaransa (Ligue-1) na Italia (Serie A) zilianza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki iliyopita kwa msimu wa 2021/2022.

Wakati dunia ikiwa katika hekaheka za janga la Uviko-19, wimbi la tatu, hali ni tofauti kwani sasa hivi mashabiki wanajiachia viwanjani. Itakumbukwa msimu uliopita ligi nyingi duniani zililazimika kuchezwa bila mashabiki au kuhudhuriwa na mashabiki wachache wakitakiwa kuchukua hatua zote za kujikinga na ugonjwa huo.

Kujazana huko katika viwanja ni kutokana na mafanikio ya chanjo na hatua za njia za kujikinga dhidi ya ugonjwa ambao hivi sasa virusi vyake vimejibadili na kuwa hatari zaidi.

Kuanza kwa ligi hizo ambazo ndizo zinafuatiliwa sana duniani ni ishara pia ya wanasoka wanaoishiriki kujipanga vyema dhidi ya majeraha yanayoweza kuwapata. Mpira wa miguu unahusisha zaidi maeneo ya chini ya kiuno na pamoja kukumbana kimwili moja kwa moja wakati wa kucheza ndiyo maana ni vigumu kukosekana kwa majeraha.

Majeraha ya wanasoka pia yanasababishwa na kutumika sana. Hili halikwepeki kwani ligi za kulipwa zinawatumia sana wachezaji ili kupata mafanikio. Majeraha ambayo kwa wanasoka hayakosekani mara kwa mara pale ligi inapoanza huwa ni majeraha ya tishu laini ambayo huwa ni pamoja na yale ya misuli, maungio, nyuzi za ligamenti na tendoni.

Kwa wanasoka eneo la maungio ndilo huandamwa na majeraha hasa katika ungio la goti na kifundo cha mguu. Kutokana na soka kuhusisha pia kugongana kimwili ni kawaida pia kupata majeraha maeneo mengine ya miili kama ilivyotokea Jumatano iliyopita katika fainali ya Super Cup Ulaya (Uefa) kati ya Chelsea na Villareal baada ya mchezaji wa Chelsea kuteguka bega.

Hivyo kwa wanasoka wote ni vyema kujua mbinu zote za kupunguza hatari za kupata majeraha yasiyo ya lazima.

TISHU LAINI

Majeraha ya tishu laini yako hivi. Majeraha ya michezo yanaweza kuwa madogo, ya kati au makubwa na huainishwa katika makundi makuu mawili kuendana na aina ya tishu iliyojeruhiwa.

Kundi la kwanza ni majeraha ya tishu ngumu, yaani mifupa ikiwamo kuvunjika na kuteguka au kuhama kwa mfupa katika pango la ungio lake. Kundi la pili ni majeraha ya tishu laini ambayo aina ya kwanza kitabibu hujulikana kama strain ambayo ni ya vijinyuzinyuzi vinavyounda misuli na miishilio ya misuli ijulikanayo kama tendoni.

Aina ya pili ya majeraha ya tishu laini hujulikana kama sprain ambayo yanajitokeza katika nyuzi za ligamenti ambazo hujeruhiwa kwa kuvutika kupita kiwango chake, kuchanika au kukatika pande mbili. Majeraha ya vijinyuzinyuzi vya misuli hutokea kutokana na kuvutika kupita kiasi au kuchanika, wakati tendoni za misuli zinaweza kukatika au kufyatuka kutoka katika mfupa uliojipachika.

Kazi ya ligamenti ni kuunganisha mfupa na mfupa katika ungio wakati tendoni ni kuunganisha msuli na mfupa na vijinyuzinyuzi vya misuli kazi yake ni kuleta mjongeo kwa kujivuta na kukunjuka. Wakati wa kucheza yapo matukio yanayoweza kusababisha tishu laini kutanuka kupita kiasi au kutumika kupita uwezo, hivyo kusababisha majeraha.

Kwa kawaida tishu hizi zinaweza kuvutika na kurudi katika hali yake ya kawaida, ila pale mtanuko unapozidi ukomo ndipo hali ya majeraha hujitokeza ikiwamo kuchanika. Vilevile tishu laini hujeruhiwa kutokana na kutumika huku zikiwa na majeraha ya ndani kwa ndani, hivyo kadri zinavyotumika ndivyo majeraha yanavyozidi kuwa makubwa.

KUPUNGUZA MAJERAHA

Jambo la msingi la kupunguza majeraha haya ni kuhakikisha mwili unapashwa moto kabla ya kuingia katika mazoezi au mechi ili kuuandaa kwa ajili ya michezo kwa ufanisi.

Kupasha moto kunasababisha damu kutiririka kwa wingi katika misuli, hivyo kuifanya misuli kupokea virutubisho muhimu kwa ajili ya utendaji wa seli na kuvifanya viungo kuwa imara kiutendaji. Epuka kuingia ghafla uwanjani na kucheza au kufanya zoezi bila kupasha, kwani mtu aliyetulia viungo vya mwili vinakuwa havijajiandaa kufanya matendo uwanjani.

Tumia muda wa saa moja kupasha mwili moto kabla ya mechi ngumu au zoezi gumu na kwa wanaofanya mazoezi ya kawaida wanahitaji kupasha angalau dakika tano hadi kumi. Pendelea kufanya usingaji (massage) kabla na baada ya mechi au mazoezi, kwani husaidia kulainisha misuli na mishipa ya damu kufunguka na kutiririsha damu kwa wingi, hivyo kuondoa uchovu.

Virutubisho vya protini kabla ya kuingia au kuanza michezo migumu husaidia kupunguza majeraha ya misuli kwani protini ni moja ya vitu muhimu kwa misuli kufanya kazi. Uwepo wa uchovu na protini kidogo katika misuli husababisha misuli kukakamaa, hivyo kusababisha kupata majeraha kirahisi.

Kuepuka kuanza kucheza kabla ya majeraha ya zamani hayajapona vizuri. Hili ni muhimu pia. Zingatia lishe bora inayoelekezwa na wataalamu wa lishe za wanamichezo. Kumbuka ulaji holela na chanjo cha kuongezeka uzito huongeza hatari ya kupata majeraha kirahisi.

Unywaji maji kwa kuzingatia kiwango sahihi kama wataalamu wanavyoelekeza. Upungufu wa maji na madini mwilini humuweka mchezaji katika hatari ya kupata majeraha. Vilevile shikamana na mbinu za kiuchezaji kama walimu wanavyoelekeza ili kukwepa majeraha yasiyo na lazima. Mfano namna ya kuruka pale unapopigwa ngwala.

Matumizi holela ya dawa za maumivu pasipo kuzingatia ushauri wa daktari wa timu huchangia majeraha kutopona kwa wakati au kujirudia rudia baadaye. Ni kweli majeraha ya tishu laini hayakosekani katika soka, lakini ukishikamana na mambo haya angalau hatari ya kuyapata inapungua.